Mwanza. Baada ya mbunge wa Kisesa, Luhaga Mpina kusimamishwa bungeni, sasa amegeukia jimboni kwake ambako amewavaa Mkuu wa Wilaya ya Meatu Fauzia Ngatumbura na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Meatu, Athuman Masasi kuhusu Sh50 milioni zilizodaiwa kuchukuliwa kwa wananchi waliotozwa faini kwa kutokuwa na vyoo.
Mpina amewaka wakuu hao warejeshe fedha hizo zilizodaiwa kuchukuliwa kwa wananchi hao, huku baadhi wakidai walitozwa fedha licha ya kuwa na vyoo.
Septemba 4, 2024, Halmashauri ya Meatu ilianza operesheni ya kukamata watu kwa madai ya kutokuwa na vyoo.
Wakizungumza jana Jumamosi Septemba 7 2024 na Mpina katika ziara yake ya kutembelea vituo vya uandikishaji wa daftari la kudumu la wapigakura, wananchi hao walidai kuwa, vyoo ambavyo havijapauliwa kwa bati pia vilitozwa faini.
Wananchi hao wamemuonesha Mpina risiti za faini zilizolipwa kati ya Sh50,000 hadi Sh150,000 huku wakidai hata watu waliokutwa hawana chanja au mabafu yaliyopauliwa kwa bati walikamatwa na kutozwa faini.
Samson Masele, mkazi wa Kijiji cha Mirongo, amesema operesheni hiyo imefanywa zaidi ya mara tano na watu wametozwa faini.
Amedai kuwa, hali hiyo imewafanya wananchi kushindwa kujitokeza kwenye vituo vya kujiandikisha kwenye daftari la kudumu la wapiga kura.
“Hata zoezi hili la kujiandikisha limekuwa la kusuasua kwa sababu watu wakiona gari wanakimbia kwenda kujificha wanajua ni watu wa vyoo,” amesema Masele.
Naye Pius Magembe mkazi wa Kijiji cha Mirongo, amedai kuwa, alitoa faini ya Sh100,000 bila kupatiwa risiti huku maofisa hao wakizikamata hata familia zenye wagonjwa.
“Mke wangu alikamatwa akiwa kwenye mkutano wa kijiji na walipofika kituoni wakanidai nitoe faini ya Sh100,000 bila lisiti,” amedai mkazi huyo.
Felista Mange, mkazi wa Kitongoji cha Nzanza, ameiomba Serikali kusitisha zoezi hilo wakati huu wa uandikishaji wa daftari la kudumu la wapiga kura.
“Nina choo na bafu, lakini nilikamatwa kwa sababu ya kutokuwa na chanja,” amedai Felista.
Akizungumza na wananchi katika kata za Nzanza, Mwabusalu na Tindabuligi, Mpina amesema mkuu wa wilaya na mkurugenzi wa Wilaya ya Meatu wanapaswa kurejesha fedha zilizochukuliwa kutoka kwa wananchi ndani ya siku saba.
Amesema atachukua hatua za kisheria endapo hicho alichokisema hakitatekelezwa.
“Naamini hizi fedha zimekusanywa kinyume cha sheria na ni uvunjifu wa sheria kuzikusanya kutoka kwa wananchi kwa makosa ya kuwasingizia na kuwaonea. Hii ni dhuluma.
“Naagiza mkurugenzi na mkuu wa Wilaya ya Meatu warudishe fedha kwa wananchi wote waliopigwa faini ndani ya siku saba kama hawatafanya hivyo, nitachukua hatua zaidi ambazo mimi nazijua,” amesema Mpina.
Amesema wananchi wanajiandikisha kwenye daftari la mpiga kura na operesheni ya kukamata wananchi ilianza Septemba 4, mwaka huu, huku akihoji mantiki ya hatua hiyo.
Amesema wananchi wanalazimika kukimbia kwa sababu wanakamatwa na kupigwa faini hata kama wana vyoo na mabafu.
“Kwa hiyo hawawezi kujitokeza kujiandikisha kwenye daftari la wapiga kura,” amesema mbunge huyo.
Amesema ataandika barua kwa viongozi husika, akiwamo Waziri wa Tamisemi, ili kufuatilia utekelezaji wa maagizo yake.
Pia, amesema atamuandikia barua Mkurugenzi wa Tume ya Uchaguzi kuomba muda uongezwe wa kujiandikisha kwa wananchi wa Meatu zifikie saba ili kutoa nafasi kwa wale waliokuwa wanakimbia.
Kauli ya Mkurugenzi na Mkuu wa Wilaya
Hata hivyo, Mwananchi imezungumza na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Meatu, Athuman Masasi aliyefafanua kuwa operesheni hiyo ilifanyika kwa lengo la kutekeleza sheria ya usafi na mazingira na kukabiliana na mlipuko wa kipindupindu.
“Hatujafanya kwa lengo la kumkomesha mtu yeyote, operesheni hii ilikuwa ya amani na hakuna mwananchi aliyepigwa au kutishiwa,” amesema Masasi.
Ameisema kama kuna mwananchi aliyepigwa faini akiwa katika hatua ya ujenzi wa choo, hilo ni kosa na fedha zake zitarudishwa.
“Tumeenda mbali zaidi na kusema watu ambao wameanza kuonyesha jitihada za kuwa na vyoo, kama vile kuchimba au kujenga, tunawapa muda wa kukamilisha,” amesema.
Mkuu wa Wilaya, Fauza Ngatumbura amekanusha madai ya kuwa, wagonjwa wanatozwa faini.
Amesema malalamiko hayo yana malengo ya kisiasa zaidi huku akisisitiza faini ya Sh50,000 inayotozwa ni kwa mujibu wa sheria kwa wale ambao hawana vyoo, wanachafua mazingira na kusababisha maambukizi ya kipindupindu.
Ngatumbura amesema hakuna fedha zilizochukuliwa kutoka kwa wagonjwa au waliokuwa kwenye foleni ya kujiandikisha katika daftari la wapigakura.
“Madai haya yana upotoshaji mkubwa wa kisiasa unaolenga kupata umaarufu kwa kuwashawishi wananchi kuwa wanalindwa dhidi ya sheria za afya na mazingira,” amesema Ngatumbura.
Baadhi ya madiwani wamedai mwamko wa uandikishaji wa daftari la kudumu la wapigakura ni mdogo katika maeneo yao kutokana na operesheni inayoendelea.
“Nimetembelea vituo vya kujiandikisha kwenye kata yangu, wananchi wanakimbia hawana amani kutokana na operesheni hii ya vyoo,” amesema Diwani wa Mwakisandu, Daudi Sollo.
Diwani wa viti maalumu Kata ya Mwanisenga, Madete Lugata amesema amepokea malalamiko kutoka kwa viongozi wa kata hiyo wakilalamikia operesheni hiyo.
Diwani wa Tindabuligi, Tabu Magembe ameishauri Serikali kuwekeza nguvu zaidi kwenye utoaji wa elimu na kuhamasisha ujenzi wa vyoo bora ili kukabiliana na mlipuko wa kipindupindu badala ya kutumia njia ya faini.