BAADA ya kupotea kwa muda mrefu uwanjani, kiungo mshambuliaji wa Tanzania Prisons, Tariq Simba anatarajia kuanza mazoezi mepesi, huku akikiri vita ya namba kikosini.
Nyota huyo alijiunga na Maafande hao dirisha dogo msimu uliopita akicheza mechi tano pekee na kuwa nje ya uwanja kufuatia operesheni aliyofanyiwa ya jino.
Kwa sasa nyota huyo anaendelea kuuguza majeraha hayo na anatarajia kuanza mazoezi mepesi baada ya wiki tatu zijazo kisha kusubiri hatma yake iwapo atamshawishi Kocha Mkuu, Mbwana Makatta.
Akizungumza na Mwanaspoti, Simba alisema kwa sasa afya yake inazidi kuimarika na baada ya mchezo wao dhidi ya Tabora United, Septemba 14 ataungana na wenzake kwa mazoezi mepesi.
Alisema kwa muda aliokaa nje ya uwanja inampa wakati mgumu kupambania namba kutokana na upinzani uliopo kikosini, akieleza kuwa yote anayepanga ni Mungu.
“Baada ya mechi dhidi ya Tabora United nitaungana na wenzangu kuanza mazoezi mepesi, itanipa wakati mgumu kufika na kupata namba kwakuwa ushindani ni mkali ila yote ni mipango ya Mungu” alisema nyota huyo.
Kuhusu matokeo waliyoanza nayo msimu huu, staa huyo alisema siyo mabaya kwani timu inaonesha uimara na ushindani akieleza kuwa suala la ushindi ni la muda tu.
“Pamoja na kwamba hatujapata ushindi, lakini timu inaonesha upinzani na soka safi, kimsingi tutapambana kwa mechi zinazofuata na tutafanya vizuri, mashabiki watupe sapoti” alisema nyota huyo.