Arusha. Vijana kutoka mikoa mbalimbali nchini wanatarajiwa kujadili ushiriki wao katika michakato ya kidemokrasia kwenye maadhimisho ya sita ya Asasi za Kiraia (Azaki), yanayotarajiwa kuanza kesho jijini hapa.
Maadhimisho hayo ya wiki ya Azaki yatafanyika kuanzia Septemba 9 hadi 13, 2024 na yanatarajiwa kuhudhuriwa na washiriki zaidi ya 500.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Jumapili, Septemba 8, 2024, Mkurugenzi Mtendaji wa HakiElimu, John Kallage, amesema kutakuwa na mjadala maalumu kwa vijana kutoka maeneo mbalimbali nchini watakaopata fursa ya kujadili ushiriki wao katika masuala ya kidemokrasia, ikiwa ni pamoja na Uchaguzi wa serikali za mitaa unaotarajiwa kufanyika mwaka huu na uchaguzi mkuu wa mwakani.
“Tofauti na mijadala mingine, mjadala huu umelenga kutambua umuhimu wa vijana kushiriki katika mchakato wa kidemokrasia, maana tafiti mbalimbali zinaonyesha ushiriki wa vijana nchini Tanzania ni hafifu,” amesema Kallage.
Amesema wanataka vijana wajadili namna wanavyoweza kutumia fursa zilizopo, ikiwemo kuwania nafasi za uongozi na kuchagua viongozi watakaowaletea maendeleo.
Mkurugenzi huyo ameongeza kuwa masuala mengine yatakayojadiliwa ni pamoja na mchango wa vijana katika uandaaji wa Dira ya Maendeleo ya 2050, kwani kutoshiriki kwao kunaweza kusababisha dira hiyo kutokidhi matakwa yao.
“Tunategemea kupata majibu juu ya vikwazo vinavyokwamisha ushiriki wa vijana katika mchakato wa kidemokrasia na kusikiliza mawazo yao ili kuwapa fursa ya kushiriki kikamilifu,” amesema.
Mkurugenzi wa Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP), Lilian Liundi amesisitiza kuwa maadhimisho ya mwaka huu yamebeba kauli mbiu isemayo ‘Sauti, Maono na Thamani’, ikilenga kutoa fursa zaidi kwa wananchi kupaza sauti zao ili kurahisisha mchakato mzima wa upatikanaji wa dira hiyo.
Pia, Liundi amesisitiza umuhimu wa ushiriki wa wanawake katika maendeleo, hasa katika maeneo ya sokoni na jinsi ya kuwalinda dhidi ya matukio ya ukatili, huku akiwakumbusha pia watoto wa kiume.
Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la Kimataifa linalojishughulisha na kuwawezesha watu wenye ulemavu wa macho nchini (CBM), Nesia Mahenge, ambaye pia ni Mwenyekiti wa kamati ya maandalizi ya wiki ya Azaki, amesema maandalizi yamekamilika na wadau zaidi ya 500 wanatarajiwa kushiriki.
Aidha, amebainisha kuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo anatarajiwa kuongoza majadiliano wakati wa ufunguzi wa maadhimisho hayo kesho.