Iringa. Mkuu wa Wilaya ya Iringa, Kheri James ameeleza kutoridhishwa na hali ya uchafu katika Soko la Samaki la Kijiweni lililopo Kata ya Kwakilosa, Manispaa ya Iringa, huku akitoa wito kwa wahusika kuchukua hatua za haraka ili kuepusha magonjwa ya mlipuko.
Akijibu hoja ya mmoja wa wajumbe wa Halmashauri Kuu ya Chama cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Iringa Mjini, James amekiri kuwa hali ya soko hilo si nzuri na amewataka viongozi wa Manispaa ya Iringa kuimarisha usafi katika soko hilo ili kulinda afya za wananchi.
Viongozi wa Halmashauri Kuu ya CCM Wilaya ya Iringa Mjini, wakiongozwa na Mwenyekiti wake Saidi Lubuya, inafanyika kwa lengo la kukagua utekelezaji wa Ilani ya CCM (2020-2025) kwenye miradi ya maendeleo katika sekta za afya, elimu, maji, biashara na barabara.
Akizungumza leo Jumapili Septemba 8, 2024 katika ziara hiyo, James amesema; “Eneo hili linasumbua sana. Wanazalisha takataka kutoka kwenye utumbo na magamba ya samaki na taka hizo zinaweza kukaa hadi siku tano bila kusafishwa, zikitoa harufu kali.”
Ameongeza kuwa baadhi ya wahusika husubiri halmashauri ije isafishe eneo hilo, licha ya kuwa ni sehemu yao ya kujipatia riziki.
Mkuu huyo wa wilaya amesisitiza umuhimu wa wahusika kuchukua hatua za usafi wao wenyewe badala ya kusubiri Serikali ikawafanyie.
“Kama tungeamua kutumia sheria, tungepafunga, maana wanahatarisha maisha ya raia. Wanasubiri manispaa ije kusafisha eneo ambalo wanapata riziki, wakati wanashindwa kusafisha wenyewe,” amesema James.
Ametoa wito kwa viongozi wa Halmashauri ya Manispaa ya Iringa kutoa elimu kwa wananchi kuhusu usafi wa mazingira, akibainisha kuwa manispaa hiyo ni ya kwanza kwa usafi nchini, ikifuatiwa na Njombe.
Kuhusu biashara holela, James amewashauri wafanyabiashara wadogo kufuata maeneo waliyopangiwa ili kuepuka kuchangia ajali za barabarani, akitoa mfano wa mji wa Moshi ambapo biashara zinafanywa katika maeneo yaliyopangwa vizuri.
Hata hivyo, Mwananchi imefika sokoni hapo na kutaka kuzungumza nia viongozi wa soko hilo ambao wamesema hawako tayari kuzungumzia suala hilo.
Mwenyekiti wa CCM Iringa Mjini, Said Lubeya akizungumzia utekelezaji wa Ilani hiyo ya CCM, amesema inaridhisha kwa kuwa miradi mingi ya maendeleo katika halmashauri yao inaendelea vema.