Wananchi Sirari watumia ndui kuhakiki wanaojiandikisha daftari la mpigakura

Tarime. Wakazi wa Kata ya Sirari wilayani Tarime, Mkoa wa Mara, wametumia alama ya chanjo ya ndui kudhibiti uandikishwaji wa watu wasiokuwa raia katika daftari la kudumu la mpigakura.

Hatua hii imechukuliwa kwa kuwa kata hiyo iko mpakani na Kenya na kuna mwingiliano mkubwa wa makabila, mila na desturi kati ya wakazi wa pande zote mbili.

 Kwa ushirikiano na vyombo vya dola, wananchi hao wanataka kuhakikisha kwamba daftari hilo linakuwa la kweli bila udanganyifu.

Akizungumza na Mwananchi Digital leo Jumapili Septemba 8, 2024, Diwani wa Sirari, Amos Sagara amesema wameamua kuwashirikisha wakazi hao kuwatambua watu wenye sifa na kuwabaini wale wanaotaka kutumia fursa hiyo  kujiandikisha kwenye daftari ilihali si Watanzania.

“Hapa kuna namna nyingi ya kuwatambua lakini zaidi tunatumia alama ya chanjo ya ndui ambapo kama kuna mtu anatiliwa shaka basi atakaguliwa kama ana alama ya ndui iliyopo  kwenye bega la kulia tunayo sisi pekee, majirani zetu hawana,” amesema Sagara.

Amesema uamuzi huo unalenga kuongeza nguvu kwa vyombo vya dola ambavyo vinatumia mbinu za kitaalamu zaidi kuhakikisha kila kitu kinakwenda sawa.

“Sio kwamba hatuna imani na vyombo vyetu vya usalama lakini sisi kama wananchi pia tumeona tuna jukumu katika  hili, na ndio  maana uongozi wa kata tulikutana na uongozi wa vijiji na tukaweka mipango sawa kwa kushirikisha na mawakala wa vyama vya siasa,” ameongeza.

Baadhi ya wakazi wa kata hiyo wamesema uchaguzi ni moja ya nyenzo muhimu katika kufikia maendeleo ya wananchi na nchi kwa ujumla, hivyo ufanisi wake unaanzia katika suala zima la kujiandikisha kwenye daftari la kudumu la mpigakura.

Mbasa Paul amesema kutokana na unyeti wa shughuli ya uboreshaji wa daftari wameamua kutoa ushirikiano kuhakikisha hakuna mtu asiyekuwa na sifa anaandikishwa, kwani kutokana na mwingiliano uliopo upo uwezekano wa watu kutoka nchi jirani kujiandikisha.

“Mbali na chanjo ya ndui tunaweza kuwatambua pia kwa lugha hasa namna ya kusalimiana lakini pia tumekubaliana tusitumie nafasi hii kuwanyima watu fursa ya kujiandikisha,  kwa kuwa  wengine wanaweza wakawazuishia wenzao kuwa sio Watanzania kwa sababu tu ya tofauti zao,” amesema Nyangi Wegesa.

Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Edward Gowele amesema mbali na kuhamasisha wananchi wenye sifa kujitokeza kwenye vituo kujiandikisha na kuboresha taarifa zao kwenye daftari, lakini vyombo vya usalama wilayani humo pia vinahakikisha wote wanaoandikishwa ni raia wa Tanzania.

Amesema hadi sasa hakuna changamoto yoyote iliyojitokeza huku mwitikio wa watu ukiwa ni mkubwa.

Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi inafanya maboresho ya daftari la kudumu la mpigakura mkoani Mara kwa muda wa siku saba ambapo uboreshaji huo unatarajiwa kukamilishwa Septemba 10, 2024 huku zaidi ya wapiga kura wapya 195,000 wakitarajiwa kuandikishwa katika wilaya sita za mkoa huo.

Related Posts