Utata kifo kada wa Chadema

Dar es Salaam. “Ni utata mtupu,” ndiyo maneno yanayoakisi tukio la kuuawa kwa Mjumbe wa Sekretarieti ya Chadema, Ally Kibao lililotokea siku moja baada ya kukamatwa akiwa kwenye basi kwenda nyumbani kwao mkoani Tanga.

Kinachojenga msingi wa utata ni mazingira ya kukamatwa kwake kulikofanyika Tegeta, mbele ya Jengo la Kibo Complex, jijini Dar es Salaam na watu waliokuwa na gari mbili zilizozuia basi hilo alilokuwa amepanda Kibao.

Hatua hiyo ilisababisha basi hilo la Kampuni ya Tashrif kusimamishwa na watu waliobeba silaha za moto na kuingia ndani hadi alikokaa Kibao na kumfunga pingu kisha kuondoka naye.

Baada ya kuripotiwa kwa tukio hilo, utata zaidi uliibuka siku moja baadaye, ziliposambaa taarifa katika mitandao ya kijamii, zikieleza kada huyo amekutwa Ununio jijini Dar es Salaam, ameshafariki dunia na usoni akiwa amejeruhiwa kiasi cha kutoonekana vema.

Mwili wake ulipelekwa Hospitali ya Rufaa ya Mwananyamala kwa taratibu za uchunguzi wa awali uliobaini kifo chake kilisababishwa na kipigo na kumwagiwa tindikali usoni, kama ilivyoelezwa na Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe alipotoa taarifa za uchunguzi wa hospitali hiyo.

Bado mazingira tata yanaendelea kugubika mauaji hayo, kwa kile kinachohojiwa na wadau, ni nani anayeweza kumteka mtu akiwa na mtutu wa bunduki na pingu.

Maswali zaidi yanaibuka hasa kutokana na ukweli kwamba, yaliyomtokea Kibao yanaongeza idadi kati ya raia wengine zaidi ya 80 wanaodaiwa kutekwa, kutoweka na baadhi yao kuuawa na wasiojulikana, kama ilivyoripotiwa Agosti 2024 na Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS).

Wito wa uchunguzi ili kuwabaini wahusika na kuundwa tume ya kijaji itakayochunguza matukio yote kwa jumla, ndiyo sauti inayoonekana kuwa moja kutoka kwa wadau wa haki za binadamu, wanasiasa na wanaharakati nchini.

Hata hivyo, wadau wanatoa wito huo wakati tayari Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB), ilishaanza uchunguzi wa matukio ya namna hiyo yanayohusisha zaidi ya watu 80.

Msemaji wa Jeshi la Polisi, David Misime  akizungumzia tukio hilo leo Jumapili Septemba 8 2024, amesema uchunguzi mkali unaendelea.

Amesema timu kutoka Ofisi ya Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai imetumwa kuongeza nguvu ili kuhakikisha waliofanya mauaji hayo wanapatikana na kufikishwa mahakamani.

“Jeshi la Polisi linaendelea na uchunguzi mkali na timu kutoka Ofisi ya Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai imetumwa kuongeza nguvu ili kuhakikisha waliofanya mauaji hayo wanapatikana na kufikishwa mahakamani,” amesema.

Alipotafutwa Waziri wa Mambo ya Ndani, Hamad Masauni simu yake iliita bila majibu na alipotumiwa ujumbe mfupi hakuujibu.

Heka heka za uchunguzi ‘Postmortem’

Awali, uliibuka mzozo katika Hospitali ya Rufaa ya Mwananyamala ulikopelekwa mwili huo, baada ya uchunguzi wa kitaalamu kubaini sababu ya kifo cha kada huyo kuonekana kuchelewa.

Ndugu wa marehemu, wafuasi na makada wa Chadema waliofurika katika hospitali hiyo, walitaka uchunguzi wa kina kubaini chanzo cha kifo cha Kibao na shinikizo lao lilikuwa uchunguzi huo ufanywe mbele ya wakili wa chama hicho, Hekima Mwasipu.

Ilionekana hali ya kutoelewana kati ya walinzi wa chumba cha kuhifadhia maiti na makada na wafuasi wa Chadema, kwa kuwa wakili huyo alizuiwa kuingia chumbani humo.

Hoja ya walinzi hao kuhusu sababu ya kumzuia Mwasipu ilijengwa na kile walichoeleza, itifaki zinaruhusu ndugu pekee kushuhudia uchunguzi huo na si mwingine.

Lakini wafuasi wa Chadema, walishinikiza Mwasipu awepo ndani, kwa kile walichodai, itawezesha kusikia uhalisia wa sababu za mauaji hao na baadaye aliruhusiwa kuingia.

Subira ilionekana kuwashinda wafuasi wengi wa Chadema waliokuwepo nje ya hospitali hiyo, kwa kuwa ilichukua muda mrefu kabla ya majibu ya awali ya uchunguzi huo kutolewa.

Kutoka saa 12:07 mchana uchunguzi ulipoanza hadi 8:50 mchana leo, ndipo Mbowe na Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika walipoitwa ndani kusikia majibu ya uchunguzi huo.

Akitoa taarifa ya awali ya uchunguzi huo mbele ya waandishi wa habari leo Jumapili Septemba 8 2024, wanachama wa Chadema, ndugu, jamaa na marafiki, Mbowe alidai kuwa pamoja na kipigo kikali, uso wa Kibao ulimwagiwa tindikali.

“Ni dhahiri ameuawa baada ya kupigwa sana na hata kumwagiwa tindikali katika uso wake,” amedai Mbowe akionekana mwenye majonzi.

Mbowe amesema wameshauriana na familia ya marehemu na kukubaliana kuwa, wanasheria wa Chadema washiriki katika kikao cha uchunguzi, kujua Kibao ameuawa kwa namna gani.

Kwa kuwa imeshindikana suala la utekaji kuzungumzwa bungeni, Mbowe alimuomba Rais Samia Suluhu Hassan kuunda tume ya kijaji ya kimahakama kuchunguza matukio yote.

Jinsi alivyochukuliwa, Mbowe amedai: “Katika gari hizo (za waliomteka) walishuka watu wa nne kati yao wawili walipanda kwenye basi wakiwa na bunduki na baadaye walienda kumchukua alipokuwa amekaa na wenye basi walipohoji waliambiwa wakae kimya.”

Amedai kuwa  Kibao alikuwa na utaratibu wa kutumia usafiri huo, wasimamizi wa basi hilo walitoa taarifa kwa familia yake.

“Baada ya kuwasiliana na familia na Chadema tulikuwa tumepata taarifa Kibao ametekwa tukaanza kutafuta huku na kule, kumbe walikuwa wanamtesa na kwenda kumtupa Ununio kabla ya Polisi wa Kawe kwenda kuuokota mwili kisha kuuleta hapa Mwananyamala,” ameeleza.

Hoja kama hiyo ilizungumzwa na Kiongozi mstaafu wa ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe kupitia ukurasa wake wa X (zamani Twitter) aliyelaani tukio hilo na kumtaka Rais Samia kuchukua hatua, ikiwamo kuunda Tume ya Kijaji ili kuchunguza tukio hilo la Kibao na matukio mengine ya watu wanaodaiwa kutekwa ama kupotea.

Katika hatua nyingine, Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM, Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM, Amos Makalla amelitaka Jeshi la Polisi kutimiza wajibu wake katika uchunguzi wa tukio hilo.

“Nimekuwa nikifuatilia toka asubuhi, sisi ni vyama vya siasa linapokuja suala la ubinadamu, siasa unaweka pembeni. Niliombe Jeshi la Polisi likatimize wajibu wake wa kuendelea na uchunguzi ili tupate taarifa baada ya uchunguzi,” alisema Makalla, akiwa ziarani mkoani Manyara.

Kupitia ukurasa wake wa mtandao wa X, Rais Samia Suluhu Hassan ameeleza kusikitishwa na tukio hilo, huku akiviagiza vyombo vya uchunguzi kumpelekea taarifa za kina.

Katika taarifa yake hiyo, alitoa pole kwa viongozi wa Chadema, wanafamilia wa Kibao na marafiki, akisisitiza Serikali anayoiongoza haitavumilia vitendo vya kikatili vya namna hiyo.

“Nimeagiza vyombo vya uchunguzi kuniletea taarifa ya kina kuhusu tukio hili baya kabisa na mengine ya namna hii haraka. Nchi yetu ni ya kidemokrasia na kila raia ana Haki ya kuishi.

“Serikali ninayoiongoza haivumilii vitendo vya kikatili vya namna hii,” ameandika katika ukurasa wake wa X.

Mdogo wa marehemu huyo, Sharif Ally amesema wameshtushwa na taarifa za kifo cha ndugu yao na tayari mwili huo umepelekwa nyumbani Morocco jijini Dar es Salaam kwa ajili ya taratibu za kuusafirisha kwenda Tanga kwa ajili ya maziko.

Sharif alisema maziko yatafanyika kesho saa 7 mchana, maeneo ya Sahale nyumbani kwa marehemu, njia ya kuelekea Pangani.

Aidha, Mwananchi limefika nyumbani kwa marehemu Mtaa wa Usagara kata ya Mzingani jijini Tanga na kuzungumza na msemaji wa familia Muhsin Ally ambaye ni baba mdogo wa marehemu, alisema kwa imani ya dini yao ya Kiislamu baada ya mtu kufariki dunia la msingi ni maziko tu.

Alisema mazishi yanatarajiwa kufanyika leo katika Kijiji cha Tarigube, Kata ya Togoni mkoani humo.

“Kwa sasa msiba upo nyumbani kwa marehemu Mtaa wa Usagara Kata ya Mzingani Tanga, hivyo ndugu na jamaa wote watakutana eneo hilo.”

“Taratibu za mazishi ni kama ifuatavyo, mwili utapokewa leo usiku na maziko yatafanyika kesho saa saba mchana kijijini kwetu Tarigube, Kata ya Togoni Mungu atujaliye,” alisema Ally

Tukio hilo, limeibua mijadala mikali mitandaoni na wadau mbalimbali wamekuwa wakitoa taarifa za kuomboleza na kulaani. Miongoni ni Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), kilichoisihi Serikali ifanye uchunguzi wa kina na haraka kubaini wahusika na wachukuliwe hatua.

Kituo hicho kimesisitiza uchunguzi huo unapaswa kuwa wa wazi ili kuondoa sintofahamu na kurudisha imani ya wananchi kwa vyombo vya ulinzi na usalama.

Kadhalika, kimezitaka mamlaka husika zielekeze juhudi kudhibiti matukio ya namna hiyo ili kupunguza taharuki kwa jamii.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo iliyosainiwa na Mkurugenzi Mtendaji wake, Anna Henga imemtaka Waziri wa Mambo ya Ndani, (Hamad Masauni), ajitathmini na kuwajibika kwa madhila yanayowakumba wananchi.

Kituo hicho, kilitoa wito kwa Rais Samia atoe tamko la kukemea matukio hayo ya utekaji na mauaji yanayoendelea nchini.

Chama cha ACT-Wazalendo nacho, kimelaani tukio hilo, kikisema kunaongeza hofu juu ya usalama na amani na kuchafua imani iliyopo kwa wananchi.

“Maswali tunayojiuliza hivi ni nani anayeweza kufanya matukio haya siku zote hizo bila kukamatwa? Je, vyombo vyetu vinazidiwa uwezo na watekaji? Tunajiuliza utekaji unafanyika kwa maslahi ya nani? Na kwa lengo lipi?” kimehoji.

Related Posts