EU yaja na mpango kununua mazao yasiyotokana na uharibifu wa mazingira

Moshi. Bodi ya Kahawa Tanzania (TCB) inakusudia kuanza kuwasajili wakulima wote wa kahawa nchini ili kukidhi matakwa ya sheria mpya ya soko la Jumuiya ya Ulaya (EU).

Sheria hiyo inataka mazao ya kahawa  yanayokwenda nchi za Ulaya  yasitokane na uharibifu wa mazingira.

Mkurugenzi Mkuu wa TCB, Primus Kimaryo akizungumza na waandishi wa habari mkoani Kilimanjaro leo Jumapili Septemba 8, 2024 amesema usajili huo umeshaanza na utakamilika Desemba 31, mwaka huu.

Lengo ni kuhakikisha mashamba yote ya kahawa nchini yanatambulika ikiwa ni hatua muhimu kwa kuendelea kutumia soko la EU linalochangia asilimia 50 ya mauzo ya kahawa ya Tanzania.

“Usajili unaanzia mkoani Kagera ambako kunazalishwa zaidi ya asilimia 40 ya kahawa nchini na baadaye utaendelea kwenye mikoa yote 17 inayolima zao hilo,” amesema.

Kimaryo amefafanua kuwa usajili huo utahusisha kuchukua taarifa muhimu za wakulima kama vile kitambulisho, picha, alama za shamba na historia ya kilimo.

Sheria mpya ya soko la EU inataka mazao kama kahawa, mbao, mpira, michikichi na kakao yasitokane na uharibifu wa mazingira.

Ametoa wito kwa halmashauri za wilaya zinazolima kahawa kutoa ushirikiano ili kuharakisha usajili, kwani ifikapo Januari 1, 2025, mazao yote yanayouzwa Jumuiya ya Ulaya yanapaswa kuthibitishwa kuwa hayajatokana na uharibifu wa mazingira.

Pia, Kimaryo amebainisha kuwa Wizara ya Kilimo itaendelea kujadiliana na Jumuiya ya Ulaya kuhusu masuala mengine kama matumizi ya viuatilifu, upatikanaji wa mbegu na uendeshaji wa mashamba.

Serikali imejipanga kutumia mifumo yake na kushirikisha wadau mbalimbali ikiwemo maofisa ugani, ushirika na wanafunzi wa vyuo vikuu katika shughuli ya  usajili.

Abertus Paschal kutoka chama kikuu cha ushirika Karagwe, amesisitiza umuhimu wa elimu kwa wakulima hususan wadogowadogo ili kufanikisha hatua hiyo na kukabiliana na uharibifu wa mazingira.

Related Posts