Wabunifu 10 wapatiwa milioni 250 kuendeleza bunifu za matumizi bora ya nishati.

Na Said Mwishehe,Michuzi TV

SERIKALI kwa kushirikiana na Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) wametoa ruzuku ya Sh.milioni 250 kwa vijana 10 wabunifu ili kutekeleza bunifu za miradi ya matumizi bora ya nishati.

Ruzuku iliyotolewa ni sehemu ya utekelezaji wa mpango mkakati wa Matumizi bora ya nishati unaotekelezwa na serikali kupitia Wizara ya Nishati na UNDP kwa ufadhili wa Umoja wa Ulaya( EU) na Ireland na kila kijana atapata sh.milioni 25.

Akizungumza na waandishi wa habari kwenye hafla ya kukabidhi vyeti na kusainishwa mikataba kwa washindi hao, Mtafiti Mwandamizi kutoka Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH), Haroun Makandi amesema tume hiyo imeshiriki kikamilifu katika mchakato wa kuwapata vijana 10 wabunifu kati ya washiriki 159 waliotuma maombi.

“COSTECH tumeshiriki katika mchakato huu wa kupata wabunifu kuanzia hatua za mwanzoni kabisa za maombi.Vijana wabunifu 10 kila mmoja atapata fedha kwa ajili ya kuendeleza bunifu yake,” alisema mtafiti huyo .

“Hili ni jambo zuri sana kwa kupata wabunifu hawa ambapo bunifu zao zitaonwa Tanzania nzima.Kwa utaratibu huu tutakuwa na jeshi kubwa la vijana ambao ni wabunifu watakaokuwa wakija na bunifu mbalimbali kwa ajili ya nchi yetu,”amesema.

Akifafanua zaidi amesema kinachofuata baada ya kupatikana washindi hao, watasaini mkataba na kupewa fedha chini ya usimamizi maalum ili kupata thamani halisi ya hizo fedha.

Kwa upande wake Mtalaam wa Miradi kutoka UNDP Abbas Kitogo amesema kuwa vijana hao wabunifu waliwasilisha mawazo yao na baada ya kupitiwa wameibuka washindi kwa bunifu zao kuchaguliwa na sasa wameonesha bunifu zao ambazo zinakwenda kusaidia katika kuangalia teknolojia inayosaidia kuwa na matumizi bora ya nishati.

Amesema kupitia bunifu zao, mtanzania anaweza kutumia nishati bila kuwa na matumizi makubwa na kwa gharama nafuu ikiwemo ya kutumia nishati ya jua kwa ajili ya matumizi katika maeneo mbalimbali ikiwemo majumbani.

“ Washindi wamepata vyeti pamoja na fedha Sh.milioni 25 kila mmoja kwa ajili ya kuendeleza bunifu zao. Vijana hawa wataendelea kusimamiwa na wamepata mafunzo mbalimbali ya kibiashara na kusimamia malengo yao,” amesema na kufafanua kuna mfumo maalum wa kuwa na vijana hao hadi mwisho.

Naye Naibu Balozi wa Ireland nchini Tanzania Mags Gaynor amesema wanajivunia kuwa sehemu ya kutekeleza wa mpango mkakati wa serikali ya Tanzania wa matumizi bora ya nishati.

“Ireland ni moja ya wadau maendeleo waliotoa msaada wa kifedha kupitia UNDP kwa serikali ya Tanzania ili kutekeleza Mpango huu ambao utaleta Mabadiliko makubwa ya Kiuchumi.”

Kwa upande wake mmoja ya vijana wabunifu Horrance Pius kutoka Kampuni ya H.O.P TECH amesema amekuja na kifaa cha MOI Power ambacho kazi yake ni kutatua changamoto ya kukosekana kwa umeme kwa watu ambao hawajaunganishwa na gridi ya Taifa.

“Kwa mfano katika vijiji ambavyo havina umeme basi watapata umeme kupitia kifaa hiki ambacho umeme wake unatokana na nishati ya jua. watakaotumia bunifu hii hawatatumia gharama kubwa ukilinganisha na nishati nyingine.

“Pia tunatamani kuona jamii inazingatia matumizi bora ya nishati, kwa mfano ukizima taa yako basi umeme ambao hautumiki kwako utatumika kwa mwingine anayehitaji.” aliongeza.




Related Posts