Katika matokeo ambayo yaliwashangaza waangalizi wachache kimataifa na hata ndani ya Algeria kwenyewe, tume huru ya uchaguzi nchini humo ilitangaza Jumapili kwamba Tebboune ameshinda asilimia 94 ya kura, akiwazidi wapinzani wake, mgombea wa chama cha Kiislamu, Abdelali Hassani Cherif, aliyepata asilimia 3 pekee na msoshalisti Youcef Aouchiche, ambaye aliambulia asilimia 2.1.
Maafisa wa uchaguzi wameripoti kuwa chini ya milioni sita kati ya wapiga kura milioni 24 nchini humo walijitokeza kupiga kura siku ya Jumamosi, na kuendeleza viwango vya chini vya wapiga kura ambavyo viliathiri muhula wa kwanza wa Tebboune na kuibua maswali kuhusu uungwaji mkono wake wa umma.
Soma pia: Raia wa Algeria wanapiga kura leo katika uchaguzi wa rais
Jumla ya mgao wa kura za Tebboune ulikuwa zaidi ya asilimia 87 ambazo Vladimir Putin alishinda katika uchaguzi wa Machi wa Urusi na asilimia 92 ambayo Ilham Aliyev alipata katika uchaguzi wa Februari nchini Azerbaijan. Waangalizi huru hawakuruhusiwa nchini Urusi wala Algeria.
Tofauti ya ushindi wa Tebboune imepita kwa mbali ushindi wake wa 2019, aliposhinda asilimia 58 ya kura na mpinzani wake wa karibu akipata asilimia 17. Maafisa walikuwa bado hawajatangaza idadi rasmi ya waliojitokeza kufikia Jumapili alasiri, ingawa jumla ya awali haikulingana na takwimu za muda zilizotangazwa Jumamosi usiku, ambapo tume ya uchaguzi ilisema waliojitokeza kupiga kura walikuwa asilimia 48 ndani ya Algeria na asilimia 19.6 kwa maeneo ya nje ya nchi.
Algeria ndiyo nchi kubwa zaidi barani Afrika kwa eneo la kijiografia na, kwa idadi ya watu karibu milioni 45, ndiyo taifa la pili kwa idadi kubwa ya watu baada ya Afrika Kusini kufanya uchaguzi wa rais mwaka huu wa 2024 – mwaka ambao zaidi ya chaguzi 50 zinafanyika kote ulimwenguni, zikijumuisha zaidi ya nusu ya idadi ya watu duniani.
Mazingira ya ukandamizaji kuelekea uchaguzi
Katika wakati wote wa kampeni, wanaharakati na mashirika ya kimataifa, ikiwa ni pamoja na Amnesty International, walikosoa mazingira ya ukandamizaji ya msimu wa kampeni na unyanyasaji na utesaji wanachaa wa vyama vya upinzani, mashirika ya vyombo vya habari na mashirika ya kiraia. Baadhi walipuuza uchaguzi huu wakiutaja kama zoezi la kukamilisha tu ratiba, ambalo inaweza tu kuendeleza na kuimarisha hali iliyopo.
Lakini Tebboune na wapinzani wake wawili kila mmoja alihimiza ushiriki wa kisiasa na hasa kufanya mabadiliko kwa vijana wa Algeria, ambao ni sehemu kubwa ya wakazi na wanaoteseka kwa wingi kutokana na umaskini na ukosefu wa ajira.
Soma pia: Algeria yamuapisha rais mpya anayepingwa na waandamanaji
Takriban nusu ya wapiga kura katika taifa hilo lenye utajiri wa gesi Kaskazini mwa Afrika walipiga kura, Tume Huru ya Uchaguzi ilisema saa chache baada ya uchaguzi kufungwa. Idadi ya awali iliyoripotiwa inazidi ushiriki wa waliojitokeza kupiga kura kutoka miaka mitano iliyopita, wakati Abdelmadjid Tebboune aliposhinda uchaguzi wake wa kwanza, katika kinyang’anyiro kilichosusiwa kwa sehemu kubwa na waandamanaji wa kudai demokrasia, ambao maandamano yao ya kila wiki yalipelekea kupinduliwa kwa mtangulizi wake.
Ushiriki wa juu zaidi lilikuwa lengo lililotangazwa sana kwa Tebboune na wapinzani wake wawili. Kila mmoja wa wagombea hao watatu alihimiza ushiriki wa kisiasa huku wanaharakati wengine na vyama vya siasa wakitoa wito wa kususia tena, wakihofia uchaguzi huo ungeimarisha tu hali ya sasa.
Kabla ya maafisa kutangaza ushindi huo mkubwa wa Tebboune, wapinzani wake walinung’unika kuhusu ucheleweshaji na kudai kuwa kulikuwa na kasoro za jinsi rekodi zilivyoripotiwa kwa umma na ofisi za kampeni za wagombea.
Katika taarifa ya Jumapili, Ahmed Sadok, meneja wa kampeni wa mgombea wa Kiislamu Abdelali Hassani Cherif aliangazia ratiba hiyo na kudai kuwa kumekuwa na kushindwa kuwasilisha rekodi za kupanga kura kwa wawakilishi wa wagombea.
Alisema Movement of Society for Peace, chama cha Cherif chenye msimamo wa wastani wa Kiislamu kilirekodi matukio ya upigaji kura wa vikundi vya uwakala na shinikizo lililowekwa kwa wafanyakazi wa uchaguzi ili kuongeza idadi fulani, ambayo hakikuiainisha.