GGML yajizatiti kuisaidia Tanzania kufikia Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs)

Kampuni ya Uchimbaji Madini ya Geita Gold Mining Limited (GGML) imesisitiza dhamira yake ya kuendelea kushirikiana na Serikali pamoja na wadau wengine ili kuhakikisha Tanzania inapiga hatua katika kufikia Malengo ya Maendeleo Endelevu ya Umoja wa Mataifa (SDGs), ifikapo mwaka 2030.

Dhamira hiyo ya GGML imewekwa wazi na Meneja Uhusiano na Mawasiliano wa kampuni hiyo, Stephen Mhando kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa kampuni hiyo wakati akizungumza kwenye hafla ya utoaji tuzo maalum za utambuzi wa biashara na mashirika ambayo yanaongoza katika kuendeleza malengo ya SDGs na kuleta matokeo chanya kwa jamii na mazingira.

Hafla ya utoaji wa tuzo hizo zilizoandaliwa na Mtandao wa Kimataifa wa Compact Tanzania (GCNT), ilifanyika mwishoni mwa wiki jijini Dar es Salaam huku GGML ikinyakua tuzo mbili muhimu ikiwa ni ishara ya utambuzi wa kampuni hiyo katika kutekeleza na kufanikisha ufikiwaji wa malengo hayo ya maendeleo endelevu.

“Kwa kutambua umuhimu wa malengo ya SDGs, GGML pamoja na kuwa mstari wa mbele katika kutekeleza mambo yote muhimu kwenye malengo haya, tumeendelea kudhamini utoaji wa tuzo hizo ili kutambua na kusherehekea mchango wa watanzania katika kufikia malengo hayo endelevu,’’ alisema Mhando.

Kwa mujibu wa Mhando, malengo hayo ya SDGs yanawiana na maadili ya mpango kazi wa GGML ambao unalenga uendelevu, ubora na ushirikiano.

“Hii ni moja ya sababu muhimu GGML, tumetoa mchango wa maana katika kufanikisha malengo kadhaa muhimu ya SDGs, likiwemo lengo namba sita linalohusu Maji Safi na Usafi wa Mazingira ambapo kupitia miradi kama mradi wa maji wa Geita, GGML tumewekeza fedha kiasi cha dola za Marekani milioni 6 ili kufikisha maji safi kwa zaidi ya wakazi 150,000 wa mkoa wa Geita na kuboresha upatikanaji wa maji safi kwa asilimia 70 mkoani humo,’’ alibainisha

Zaidi, alisema kampuni hiyo imetekeleza lengo namba 8 la SDGs ambalo linahusu kazi zenye staha pamoja na ukuaji wa uchumi, kwa kutoa maelfu ya ajira, kusaidia biashara za ndani na kuchangia maendeleo ya uchumi wa Tanzania.

“SDG 4 ambalo linalozungumzia Elimu Bora, GGML imewekeza katika ujenzi wa shule na kuibua programu za elimu zinazowezesha kizazi kijacho cha viongozi.

“SDG 13 ambalo linazungumzia namna ya Kuchukua Hatua Dhidi ya Mabadiliko ya Tabia Nchi, kwa upande wa GGML imehakikisha kwamba shughuli zake zinakidhi viwango vya juu zaidi vya mazingira na kwa kuwekeza katika teknolojia endelevu zinazoboresha uhifadhi wa kama vile uzinduzi wa hivi karibuni wa Kituo Kidogo cha 33/11KV ambacho ni alama ya kipekee kwa kampuni kuanza kutumia umeme wa Gridi ya Taifa ya Umeme unaotolewa na TANESCO,” aliongeza

Akizungumzia tuzo hizo alisema, zinaashiria zaidi ya uwajibikaji wa shirika kwa kuwa zinatambua kazi kubwa inayofanywa na mashirika yote Tanzania kuelekea mustakabali endelevu.

“Tunaposherehekea mafanikio haya tunalenga kuthibitisha dhamira yetu ya kufanya kazi bega kwa bega na wadau wote ili kuhakikisha kwamba hatumwachi mtu nyuma katika safari hii ya kuelekea maendeleo endelevu.

“Ni kwa sababu hii kampuni ya GGML ambayo ni kampuni tanzu ya AngloGold Ashanti tunaunga mkono Kanuni za Mkataba wa Kimataifa wa Umoja wa Mataifa kuhusu haki za binadamu, kazi, mazingira na mapambano dhidi ya rushwa’’ alisema.

Kwa mujibu wa Mhando, Julai 2024 kampuni hiyo ilithibitisha upya nia hiyo kupitia maombi yake kwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ili kujiunga rasmi na Mkataba wa Kimataifa wa Umoja huo kupitia Mtandao wa Global Compact Tanzania.

Akizungumza katika hafla hiyo, Naibu Katibu Mtendaji – Biashara na Ubunifu kutoka Tume ya Mipango, Dk. Lorah Madete alipongeza uazishwaji wa tuzo hizo na kueleza kuwa zimekuwa chachu katika kuiwezesha Tanzania pamoja na kampuni mbalimbali nchini kutambua namna zinavyopiga hatua kufikia malengo hayo ya maendeleo endelevu.

“Tutaendelea kushirikisha sekta binafsi kuhakikisha biashara zao zinaleta matokeo chanya katika kutekeleza malengo ya SDGs kwa jamii. Hivyo basi, ni wito wangu kwa kampuni mbalimbali kuendelea kujiunga na Mtandao huu wa GCNT ili kutanua biashara zao, kujulikana na kuwa na ushindani,” alisema.
Mwisho.

.

Related Posts