Dar es Salaam. Mataifa mbalimbali duniani yameeleza kusikitishwa na taarifa za vitendo vya ukatili, kupotea, vifo dhidi ya wanaharakati wa haki za binadamu na kisiasa nchini, huku yakisisitiza uchunguzi wa haraka kubaini wanaohusika.
Masikitiko ya mataifa hayo 15 yanayounda Umoja wa Ulaya (EU) yaliyotolewa na balozi zao zilizopo nchini, yameisihi Serikali kuhakikisha ulinzi wa wapinzani ili kuendana na falsafa ya R4 kama alivyoahidiwa na Rais Samia Suluhu Hassan.
Falsafa hiyo yenye tafsiri ya maridhiano, ustahimilivu, mageuzi na kujenga upya, ilitambulishwa na Rais Samia mapema baada ya kuapishwa kuwa Rais Machi mwaka 2021, kama msingi wa utendaji wake.
Mataifa hayo 15 ni Ubelgiji, Uingereza, Canada, Denmark, Ufaransa, Finland, Ujerumani, Ireland, Italia, Uholanzi, Norway, Poland, Hispania, Sweeden na Uswisi.
Hata hivyo, tamko la mataifa hayo linakuja muda mchache tangu alipozikwa kada wa Chadema, Ali Kibao aliyekutwa ameuawa Ununio jijini Dar es Salaam, siku moja baada ya kukamatwa na wasiojulikana akiwa kwenye basi.
Kuuawa kwake kulimuibua Rais Samia Suluhu Hassan kupitia mitandao ya kijamii, akiandika kusikitishwa na tukio hilo, huku akiviagiza vyombo vya uchunguzi kufanya uchunguzi wa kina na kuwasilisha taarifa kwake.
Katika taarifa yake hiyo, mkuu huyo wa nchi, alisisitiza Serikali chini yake haitavumilia vitendo vya namna hiyo.
“Nimeagiza vyombo vya uchunguzi kuniletea taarifa ya kina kuhusu tukio hili baya kabisa na mengine ya namna hii haraka. Nchi yetu ni ya kidemokrasia na kila raia ana haki ya kuishi. Serikali ninayoiongoza haivumilii vitendo vya kikatili vya namna hii,”aliandika Rais Samia Septemba 8, 2024.
Katika tamko la pamoja na mataifa hayo, lililotolewa leo Jumanne Septemba 10, 2024, nchi hizo zimeisihi Tanzania kulinda haki za msingi wa wananchi ukiwemo uhuru wa kujieleza.
“Jumuiya ya Umoja wa Ulaya unasikitishwa na taarifa za hivi karibuni za vitendo vya ukatili, kupotea kwa watu na vifo vya wanaharakati wa kisiasa na haki za binadamu,” linaeleza tamko hilo.
Umoja wa nchi hizo, umetaka uchunguzi wa kina wa matukio hayo, huku ukiwapa pole wanafamilia wote walioathiriwa na vitendo hivyo.
“Tunakaribisha wito wa Rais wa kuanzisha uchunguzi wa haraka ili kubaini wahalifu waliohusika na kuhakikisha kuna uwajibikaji,” imeelezwa katika tamko hilo.
Tamko hilo limetoa wito wa ulinzi wa upinzani ili kuakisi falsafa ya R4 ya Rais Samia.
“Tunatambua kwa wasiwasi mkubwa kwamba matukio haya ya hivi karibuni yanatishia misingi ya kidemokrasia na haki za wananchi wa Tanzania.
“Katika nchi inayoheshimika kimataifa kwa amani na utulivu, tunaungana na wito wa kulinda amani na utulivu wa nchi,” linaeleza tamko hilo.