Nchi ipo masika. Mvua zinazonyesha zinatoa ujumbe unaoingia ndani zaidi. Tanzania haina uwezo wa kuhimili mvua mfululizo.
Kadiri miaka inavyosogea, ndivyo picha mbaya zaidi inajitengeneza kuhusu usalama wa nchi. Dar es Salaam leo, miundombinu ni mibovu. Zile hadithi kuwa watu wanaoishi mabondeni ndiyo hawapo salama, tafsiri inahama. Sasa, Dar es Salaam kila sehemu ni bondeni. Hata maeneo yaliyopo uwanda wa juu yanakumbwa na mafuriko.
Ujenzi holela, fedha zinazidi nguvu sayansi. Utatuzi wa matatizo kwa kutumia mawazo kidogo yenye mtazamo wa muda mfupi, badala ya kufikiria miaka mingi ijayo. Hapa ndipo nchi inaumizwa. Bila hatua za haraka tutarithisha watoto na wajukuu nchi mfu.
Mvua kidogo, barabara zinatengeneza matundu kila mahali. Dar, Arusha, Mwanza hadi Mbeya. Inadhihirisha namna ambavyo ujenzi unafanyika chini ya viwango mbele ya viongozi wanaoomba bajeti, wanaopewa na kuzisimamia. Wataalamu pia wapo.
Janga la taifa ni rushwa na ufisadi. Viongozi na wataalamu wanaotegemewa kuisaidia nchi, wanafuja fedha za miradi, matokeo yake miundombinu inajengwa nchini ya kiwango.
Makandarasi wanahonga kushinda zabuni. Vigezo vya kisayansi havina tija mbele ya mizengwe. Viongozi wanapaswa kuwaza kesho na siyo leo. Matatizo mengi Dar es Salaam ni ujenzi unaoingilia njia za maji. Mwenye fedha anahamisha uelekeo wa maji, matokeo yake madhara hutokea pale mvua zinaponyesha mfululizo. Maji yanapanda hadi kwenye miinuko.
Barabara ya Bagamoyo, Kunduchi, Dar es Salaam, lile eneo ni mwinuko mkubwa. Siku hizi maji yanajaa juu halafu yanatuama. Barabara inayotoka Africana kwenda Jangwani Sea Breeze, imegeuka mtaro wa kupitishia maji kila mvua zinaponyesha. Hili linaakisi ujenzi usio na viwango.
Kawe Beach nyumba nyingi zimebomolewa, wakati zamani maji yalipita kwenye mto kwenda baharini bila bughudha. Ukiuliza sababu ya mabadiliko, unaambiwa kuna kigogo alijenga, akahamisha njia ya maji, matokeo yake ndiyo hayo madhara. Wataalamu wako kimya, wanaogopa wakubwa.
Nilishaandika na hapa nasisitiza; nchi inahitaji mapinduzi ya maarifa. Ulaya waliketi na kuunda fikra za kujenga bara lao. Nyakati hizo za ujenzi wa kifikra waliziita Enlightenment Age (Zama za Maarifa). Tanzania inahitaji maboresho ya jinsi ya kufikiria kwanza. Enlightenment Age inajumuisha mitazamo na kazi za kifalsafa za Francis Bacon, John Locke mpaka Sir Isaac Newton, vilevile chapisho la “Discourse on the Method” la Rene Descartes mwaka 1637, lenye maana kuwa fikra za mtu ndiyo msingi wa mtindo wa kuishi.
Enlightenment ni majumuisho ya mawazo ambayo kitovu chake ni msingi wa furaha ya binadamu, msako wa maarifa yenye kupatikana kwa njia ya kuhoji na uthibitisho wa kifikra. Inakwenda mbele zaidi na kugusa sheria asilia, uhuru, maendeleo, uvumilivu, undugu, serikali ya kikatiba, vilevile mgawanyo wa dola na dini.
Mwaka 2020, nilifanya ziara maeneo ya mabondeni, hasa jimbo la Amani, Zanzibar. Niliongozana na aliyekuwa Mwakilishi, Rashid Ali Juma. Nikapata simulizi ya jinsi ambavyo mafuriko yamedhibitiwa kiasi ambacho hata mvua inyeshe kiasi gani, watu wanaoitwa wa mabondeni, wanabaki salama. Nini siri ya mafanikio hayo Zanzibar? Jibu ni ujenzi sahihi wa miundombinu.
Zanzibar hawakuona kama suluhu ya mafuriko na ghasia za mabondeni nyakati za mvua ni kusimanga wakazi wake, kuwahimiza kuhama au hata kuwahamisha. Walijua dawa ni kujenga njia nzuri za kupitisha maji chini.
Kupitia msaada wa Benki ya Dunia, Zanzibar walitengeneza mifereji mikubwa ya kupitishia maji chini ya ardhi. Ukubwa wake unatosha kabisa mabasi mawili makubwa kupishana chini na juu au ubavu kwa ubavu. Mifereji hiyo mikubwa ndiyo imekuwa suluhu ya kudumu huko mabondeni.
Mifereji hiyo mikubwa inapita chini ya barabara na nyumba za watu. Mvua inaponyesha, maji yanapita kwenye uelekeo wake, yanaingia ndani ya mifereje mikubwa na kusafirishwa hadi baharini. Maarifa ndiyo ambayo yamewezesha kuwa salama.
Tofauti ni jinsi ya kufikiria na kutatua matatizo. Zanzibar, kwa kuzingatia udogo wa ardhi, waliamua kushughulika na maji, badala ya kukimbizana na watu au makazi yao. Huku Bara tunashughulika na watu na makazi yao, ili kuyaacha maji yatawale.
Kama mapinduzi ya fikra hayatakaribishwa, ikapatikana tiba ya jinsi ya kutatua matatizo ya watu kwa usahihi, rushwa ikachukiwa kutoka ndani ya fikra na moyoni, suluhu zikatazamwa za kudumu na kujenga dhamira ya kuiacha nchi salama kwa vizazi vijavyo, historia itatoa hukumu mbaya kwa hiki kizazi cha sasa.
Wajibu wa kizazi cha sasa ni kujenga nchi na kuiacha ikiwa bora zaidi. Haitakiwi wanaokuja waanze kushughulika na makosa ya waliopita. Halafu makosa hayo yawe yanabeba hisia za rushwa na uzembe. Makaburi yatachapwa viboko.
Unapokuwa kiongozi katika eneo lako, jiulize kuhusu malengo yako ya kuiacha nchi ikiwa bora kuliko ulivyoikuta. Siyo akili yako yote iwe kwenye kuiboresha familia yako. Hakikisha unajenga maarifa sahihi, vilevile uchukie rushwa. Inawezekana kuijenga Tanzania bora na kuviachia vijavyo matunda mema ya urithi wa taifa.