MCL, ATOGS, TZLPGA kuandaa kongamano la ‘Energy Connect 2024’

Dar es Salaam. Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL), Jumuiya ya Watoa Huduma za Mafuta na Gesi Tanzania (ATOGS) na Chama cha Waagizaji na Wasambazaji wa Gesi za Mitungi Tanzania (TZLPGA), wametia saini Mkataba wa Makubaliano kuandaa Kongamanano la Nishati Safi liitwalo ‘Energy Connect 2024.’

Kongamano hilo lenye kaulimbiu: “Ushirikiano wa kibunifu katika nishati safi ya kupikia, endelevu na mustakabali wa kijani,” litafanyika kwa siku tatu kuanzia Oktoba 16 hadi 18, 2024, jijini Dar es Salaam.

Lengo kuu la kongamano hilo ni kuwaleta pamoja wadau mbalimbali wa nishati na mashirika na kampuni katika sekta zingine zinazotambua thamani wa nishati safi kwa jamii.

Akizungumza baada ya utiaji saini, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa MCL, Victor Mushi amesema matumizi ya mkaa na kuni yanaathari kiafya hivyo wameona waungane na Serikali na wadau kuwakwamua watu wanaotumia nishati hizo wahamie katika nishati safi za kupikia.

“Tumejizatiti kwenye kuongeza uhamasishaji na kutoa uelewa mkubwa kwa jamii nchini, nishati safi ya kupikia, kupitia majadiliano na kuleta suluhisho za kibunifu ambazo zitatokea katika tukio hili.

“MCL tutashirikiana na Serikali pamoja na sekta binafsi na siziso binafsi kwenye kuelimisha jamii kwa njia bunifu kuhusu utumiaji wa nishati safi na salama kwa mazingira na afya,” amesema Mushi.

Amesema kongamano la ‘Energy Connect 2024’ ni uthibitisho wa kujitolea katika kuunga mkono vumbuzi endelevu na jitihada zinazofanywa mpaka sasa na wadau mbalimbali katika utekelezaji wa sera ya nchi ili kufanikisha malengo ya nishati safi ya Tanzania.

Kwa upande wake, Abdusamad Abdulrahim, Mwenyekiti wa ATOGS, amesema dhumuni la kongamano hilo ni kumtua mama kuni ambazo zinaathari kwa afya ikiwamo kupofua macho.

Amesema muunganiko huo ni kuleta nguvu pamoja kwa kuwa kidole kimoja hakivunji chawa. Pamoja na kumuunga mkono Rais Samia Suluhu Hassan kutaka asilimia 80 ya Watanzania watumie nishati safi hadi ifikapo 2034.

Aidha, tukio hili litakutanisha wadau muhimu kutoka kwenye mayororo wa thamani wa nishati ili kuchunguza suluhu za ubunifu zitakazounda mustakabali wa Tanzania.

“Tunaamini kuwa kwa pamoja, tunaweza kufanya maendeleo makubwa kuelekea kufanikisha mustakabali wa nishati endelevu kwa Tanzania,”amesema Abdulrahim

Amesema kipaumbele ni teknolojia na nishati safi kila kona ya Tanzania watu wapewe vitendea kazi na teknolojia waweze kukacha matumizi ya kuni na mkaa.

“Wito wangu kwa Watanzania kwanza lazima tuimbe wimbo mmoja lazima twende kwa pamoja hadi waliopo vijijini tushiriki kwa siku hizi tatu ili tukomboe Watanzania wanaotumia kuni na mkaa,” amesema.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa Chama cha Waagizaji na Wasambazaji wa Gesi za Mtungi, Mhandisi Amos Jackson, amesema kongamano hilo ni sehemu ya kutoa elimu na kuishirikisha na Serikali katika changamoto zilizopo.

Amesema LPG ina mchango mkubwa huku lengo la Serikali kuwataka Watanzania watumie nishati safi ya kupikia.

Related Posts