CCM wataja mambo matano yanayombeba Rais Mwinyi

Unguja. Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar, Dk Mohamed Said Dimwa ametaja mambo matano ya kujivunia na kuungwa mkono katika uongozi wa Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi tangu aingie madarakani Novemba 2020.

 Mambo hayo ni Zanzibar yenye kuheshimu, kulinda na kuenzi misingi ya demokrasia na siasa za maendeleo, yenye kuenzi na kulinda historia yake hasa ya Mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka 1964.

 Mengine ni Zanzibar yenye neema kwa wote, yajayo yametimia, salama na yenye maendeleo endelevu.

 Amesema hayo wakati akiwahutubia wanachama wa CCM na wananchi wa Wilaya ya Micheweni Pemba leo Jumanne, Septemba 10, 2024 katika mwendelezo wa ziara ya wajumbe wa sekretarieti ya Kamati Maalumu ya NEC, CCM Taifa Zanzibar kisiwani Pemba.

 “Haya ni mambo ambayo tunapaswa kujivunia kwa uongozi wa Dk Mwinyi na kila mmoja anaona jinsi tunavyopata mabadiliko makubwa,” amesema.

 Dk Dimwa amesema dhamira ya CCM ni kusimamia na kufuatilia kwa karibu utekelezaji wa Ilani yake ya uchaguzi unaotekelezwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ili wananchi wa makundi yote wanufaike na fursa ya maendeleo endelevu.

 Amesema Zanzibar inapiga hatua kubwa ya maendeleo katika nyanja za kiuchumi, kijamii na kisiasa.

 Dk Dimwa  amesema siri ya mafanikio hayo ni uwazi na uhuru uliowekwa na Serikali kwa kufungua milango ya uwekezaji sambamba na kuweka sera na sheria rafiki katika uendeshaji wa biashara huria kwa wawekezaji wa ndani na nje ya nchi.

 “Tumejipanga vizuri kuiweka Zanzibar katika nchi za visiwa zilizoendelea kiuchumi na kwa kasi hii ya Rais Dk Mwinyi ndani ya kipindi kifupi baada ya kukamilika kwa miundombinu ya bandari na viwanja vya ndege vya kisiasa basi tujipange sote kuvuna matunda ya Serikali yenu,” amesema Dk Dimwa

 Amewasihi wananchi wa Kisiwa cha Pemba kuendelea kujitokeza kwa wingi kujiunga na CCM ili waweze kunufaika na siasa zisizokuwa na ubaguzi wa rangi, dini, ukanda na ukabila.

 Amesisitiza wananchi wa kisiwani humo kupuuza kauli za uchochezi zinazotolewa na baadhi ya viongozi wa vyama vya upinzani akisema wengi wao tayari wanaona kasi ya maendeleo imekuwa kubwa, hivyo wanapotosha na kubeza Serikali ili kutafuta huruma kwa wananchi waliowasaliti kupitia ahadi zao zisizotekelezeka.

 Kupitia mkutano huo, zaidi ya wanachama 150 wanaodaiwa kutoka chama cha ACT-Wazalendo na CUF wamejiunga na CCM.

 Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Kaskazini Pemba, Mberwa Hamad Mberwa amesema mkoa huo unaendelea kutekeleza kwa vitendo kazi za chama na kuisimamia Serikali itekeleze vizuri Ilani ili wananchi wapete huduma bora.

 Akizungumza kwa niaba ya wanachama hao, Hamad Haji amesema ni haki yao ya kidemokrasia kila mmoja kuangalia sehemu yenye demokrasia ya kweli.

Related Posts