Jaji Mihayo afunguka mapya matukio ya utekaji, mauaji

Dar es Salaam. Wakati wadau wakitaka kuundwa tume ya kijaji kuchunguza matukio ya utekaji na mauaji, Jaji mstaafu Thomas Mihayo ameshauri iwepo Mahakama Maalumu ya Uchunguzi wa vifo vyote vyenye utata nchini.

Hoja hizo zimetolewa kutokana na matukio yanayojitokeza nchini ya watu kutekwa na kuuawa, likiwamo la aliyekuwa kada wa Chadema, Ally Kibao.

Kwa mujibu wa wadau hao, tume maalumu ya kijaji inapaswa kuundwa na Rais Samia Suluhu Hassan kuchunguza matukio hayo pamoja na kulichunguza Jeshi la Polisi.

Kibao alitekwa na watu wasiojulikana jioni ya Septemba 6, 2024, eneo la Kibo Complex, Tegeta jijini Dar es Salaam akiwa ndani ya basi la Tashriff akielekea nyumbani kwake, mkoani  Tanga.

Mwili wa Kibao ulikutwa Ununio, Dar es Salaam na ulizikwa Jumatatu Septemba 9, katika Kijiji cha Tarigube Kata ya Togoni, mkoani Tanga.

Uchunguzi utakaofanywa na chombo huru ni wito uliotolewa na wadau wengi kama njia ya kupata jawabu la matukio hayo. Ubalozi wa Marekani na Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) ni miongoni mwa wadau waliotoa wito huo.

Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Boniface Mwabukusi pia alisema uchunguzi huo haupaswi kufanya na Jeshi la Polisi bali tume maalumu itakayoundwa na Rais Samia.

Mwanazuoni wa Sheria Profesa Gamaliel Mgongo-Fimbo akizungumza na Mwananchi ametaka kuundwa kwa tume ya kijaji itakayofanya uchunguzi wa jumla.

“Inawezekana wakati polisi wanafanya uchunguzi kuhusu tukio la Kibao, kukawa na chombo kingine cha uchunguzi kwa sababu kuna wanaohisi kwamba watendaji wa mambo haya ni polisi,” alisema Profesa Mgongo-Fimbo.

Mwenyekiti wa Shura ya Maimamu Tanzania, Sheikh Issa Ponda pia alipendekeza kuundwa kwa tume ya kijaji kwa ajili ya kuchunguza matukio ya utekaji na mauaji.

Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe naye aliungana na wadau wengine kutaka tume ya kijaji ichunguze matukio hayo na vyombo vya dola kwa ujumla.

Jaji Mihayo akizungumza na Mwananchi leo Septemba 10, 2024 ofisini kwake jijini Dar es Salaam amesema kwa mtazamo wake, utaratibu wa Mahakama Maalumu ya Uchunguzi, kuchunguza vifo vyote vyenye utata ndilo suluhisho na siyo kuundwa tume ya kijaji.

Amesema kwa utaratibu wa Sheria ya Uchunguzi Maalumu wa Vifo Sura ya 24 (The Inquests Act) iliyofanyiwa marejeo mwaka 2019 vifo vya watu vinavyotokea gerezani, kituo cha polisi au sehemu nyingine yenye kutia shaka, vinachunguzwa na mahakama inayotafuta ushahidi.

Jaji Mihayo amesema kwa mujibu wa sheria hiyo, Mahakama hiyo inayojulikana pia kama Mahakama ya Korona chini ya hakimu, itachunguza kwa kuwahoji watu na ikijiridhisha kwamba kuna jinai itawasilisha kwa Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) kwa hatua zaidi za mashtaka.

Jaji Mihayo aliyewahi kufanya uchunguzi huo akiwa hakimu mwaka 1970 hadi 1976 katika wilaya za Same na Korogwe, amesema hakimu hatasema ni nani ana kosa, bali ataeleza kulingana na mazingira ya kifo kinaweza kusababishwa na watu kadhaa, hivyo kuwezesha polisi kuendelea na upelelezi na kukamata wahusika.

“Imekuwa kawaida yanapotokea mambo kama haya kumtaka mkuu wa nchi kuunda tume, hii ni hatari. Tume haiwezi kuwa na jibu, Sheria ya Uchunguzi Maalumu wa Vifo Sura ya 24 (The Inquests Act) ndiyo suluhisho,” amesema.

Kuhusu Mahakama ya Korona

Waziri wa Katiba na Sheria aliwahi kujibu bungeni swali la aliyekuwa mbunge wa viti maalumu mwaka 2015 hadi 2020, Upendo Peneza kuhusu Mahakama hiyo, akieleza uchunguzi wa vifo vinavyotokea katika mazingira yenye utata ambayo sababu zake hazijulikani, hufanywa kwa uchunguzi maalumu (inquest) na mchunguzi aitwaye korona kwenye Mahakama Maalumu ya Uchunguzi.

Utaratibu huo umekuwa ukitumika hata kabla uhuru chini ya Sheria ya Uchunguzi Maalumu (Inquests Ordinance) Sura ya 24.

Sheria hiyo ilifutwa na kutungwa upya kuwa Inquests Act No. 17 ya 1980 ili kuendana na mazingira mapya ya haki jinai nchini baada ya uhuru.

Sheria hiyo mpya iliridhiwa na Rais wa Kwanza wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, hayati Mwalimu Julius Nyerere Mei 21, 1980, chini ya kifungu cha 5(1) Waziri wa masuala ya Sheria wa wakati huo alitangaza sifa za uteuzi za kuwa korona na chini ya kifungu cha 5(2) na (3), Jaji Kiongozi kwa kushauriana na Jaji Mkuu, aliwateua Mahakimu Wafawidhi wa Mahakama za Wilaya na za Hakimu Mkazi kuwa makorona.

Kwa tangazo la Serikali Na. 252 la Julai 16, 2004, Mahakama za Wilaya na za Hakimu Mkazi ziliteuliwa kuwa Mahakama za Korona pale zinapoketi kwa uchunguzi wa vifo vyenye utata.

Related Posts