Morogoro. Wakazi 12 wa Kijiji cha Malangali, Kata ya Tindiga wilayani Kilosa, Mkoa wa Morogoro, wanashikiliwa polisi na wengine wanane wanaendelea kusakwa wakidaiwa kuhusika na vurugu za wafugaji na wakulima.
Hata hivyo, Mkuu wa Oparesheni Maalumu za Jeshi la Polisi, Naibu Kamishina wa Polisi (DCP), Mihayo Msikhela amesema jeshi hilo halitamvumilia yeyote atakaye vunja sheria.
Akizungumza katika mkutano uliotishwa na Mkuu wa Wilaya ya Kilosa, Shaka Hamdu Shaka, kijijini hapo Mwenyekiti wa Kijiji cha Malangali, Seleman Mapala, amesema vurugu hizo zilitokea Septemba 8, mwaka huu baada ya wafugaji kudaiwa kuingiza mifugo katika mashamba ya wakulima.
Mapala amesema baada ya wafugaji kutenda kitendo hicho, inadaiwa wakulima waliamua kukamata mifugo na kuijeruhi kwa kukaikata kwa kitu chenye ncha kali jambo lililosababisha kuibuka kwa vurugu na uvunjifu wa amani.
Amesema kwa zaidi ya wiki tatu sasa kumekuwepo na mkakati wa wilaya hiyo kudhibiti mifugo na wafugaji wakorofi inayotekelezwa na vyombo vya ulinzi na usalama chini usimamizi wa Shaka.
Mapala amesema operesheni hiyo imeonesha mafanikio makubwa katika kipindi kifupi tangu ilipoanza kutekelezwa.
“Kuna kikundi cha watu baada kuona mkakati huu unafanikiwa, wanataka kuwaaminisha wananchi kuwa hili wanalifanya wao, hivyo wamewashawishi vijana wadogo nao kujihusisha katika ukamataji mifugo kinyume na utaratibu.
“Lengo lao ni kujijenga kisiasa jambo ambalo limesababisha kuchochea uvunjifu wa amani kijijini kwetu,” amesema Shaka.
Mwenyekiti wa Chama cha Wafugaji Kata ya Tindiga, Filimon Karao, akizungumza katika mkutano huo, amewasihi wananchi wa kijiji hicho kuwa wamoja na kuheshimiana kwa kuwa wao ni ndugu na baadhi ya wafugaji wamezaliwa katika eneo hilo.
“Tunashukuru sana jitihada za DC (mkuu wa wilaya) kutaka kutuunganisha kuwa wamoja tuishi kwa upendo na mshikamano, kinachosikitisha ni kuona baadhi ya viongozi wa kisiasa hususan upinzani kutaka kutumia kivuli chake kuaminisha watu mambo ambayo hawakuyafanya.
“Lengo lao ni kujitafutia umaarufu na kutaka kusababisha umwagaji damu baina wakulima na wafugaji, wanawashawishi vijana wadogo kuyafanya hayo,” amesema.
Kwa upande wake Shaka, amesema Serikali imejipanga vyema na haitaruhusu jambo lolote la uvunjifu wa amani au umwagaji damu kwa kisingizio cha mgogoro wa wakulima na wafugaji.
“Nimekuwa nikisema mara kwa mara wako watu ni wanufaika wa migogoro hii, hivyo wakiona jitihada zozote za Serikali kutaka kulimaliza kwao ni shida, operesheni tuliyoianzisha inakwenda vyema, yeyote atakayetaka kukwamishana atakumbana na mkono wa sheria.
“Hiki kinachofanyika ni utekelezaji wa maelekezo ya Rais Dk Samia Suluhu Hassan kutaka wafugaji na wakulima waishi pamoja kwa upendo na mshikamano bila kurudishana nyuma kiuchumi na kuleta uvunjifu wa amani nchini, hivyo kazi kubwa inayofanyika ni kujenga ustawi wa makundi hayo na kukomesha, kumaliza kabisa changamoto hiyo,” amesema Shaka. Amesema waliohusika na vurugu hizo wanaendelea kusakwa kwa lengo la kuchukuliwa hatua zaidi za kisheria ikiwamo kufikishwa mahakamani baada ya upepelezi wa polisi kukamilika.