Dar es Salaam. Licha ya kuwepo kwa juhudi za kuwashirikisha wenye ulemavu katika fursa na majukumu mbalimbali, watu wenye uziwi wamelalamikia kunyimwa baadhi ya haki ikiwmo ya kumiliki leseni ya udereva.
Haki nyingine wanazodai ni pamoja na kukosa huduma sahihi za afya, dini, uwakilishi mahakamani na upungufu wa wakalimani.
Hayo yameelezwa leo Jumanne Septemba 10, 2024 na Mkurugenzi wa Furaha ya Wanawake Wajasiriamali kwa Viziwi Tanzania (Fuavita), Aneth Gerana wakati wa uzinduzi wa mwongozo kwa vyombo vya habari katika kuripoti taarifa ya watu wenye uziwi nchini.
Amesema wanaponyimwa haki ya kumiliki leseni za udereva kwa sababu ya ulemavu, inasababisha ratiba zao kutegemea za wengine pindi wanapotaka kutekeleza majukumu yao, jambo linalowarudisha nyuma kiutendaji.
“Kila tukitaka kufanya majukumu inabidi tupange ratiba zetu ziendane na wale watakaokuendesha magari, jambo hili linaturudisha nyuma katika majukumu yetu, tunahitaji kupewa leseni za udereva.
“Kwenye runinga pia tunawekwa kwenye kiboksi kidogo hii inamaanisha lugha hii haikubaliki tunahitaji lugha hii ipitishwe na itumike kwa ukubwa,” amesema.
Gerana amesema wenye uziwi wanatamani lugha ya alama iwe lugha rasmi inayotumika na inayotambulika nchini na vyuoni kama ilivyo nchini Afrika kusini.
“Tunatamani tuwe na mwakilishi bungeni kama ilivyo kwa makundi mengine ya wenye ulemavu, ili watusemee yanayotuhusu,” amesema.
Amewaasa waandishi kutotumia majina yanayowadhalilisha kutokana na ulemavu walionao.
“Waandishi wa habari wamekuwa wakitumia jina bubu kuripoti taarifa za viziwi neno ambalo tafsiri yake ni jiwe au mti, kwa maana nyingine ni kitu ambacho hakina uhai.
“Hili linatuumiza na ndilo lililotusukuma kutoa mwongozo huu ambao unalugha nzuri kuliko zile zilizotumika hapo mwanzo,” amesema.
Ofisa Masoko Mwandamizi Mamlaka ya Udhibiti wa Mawasiliano Tanzania (TCRA), Joyce Paul aliyezungumza kwa niaba ya mkurugenzi mkuu wa mamlaka hiyo, Jabir Bakari, amesema: “Matukio ya ukatili kwa wenye uziwi hayaripotiwi kwa usahihi kama inavyostahili, hali hii inawanyima haki zao za msingi.”
Amewataka waandishi wa habari kupaza sauti za kundi hilo kwa kutoa taarifa hizi zenye lugha sahihi.
“Tunatoa wito kwa waandishi wa habari kuzingatia mwongozo na kuutumia kwa makini na kwa pamoja tunaweza kuleta mabadiliko katika jamii nakuhakikisha kuwa kila taarifa zinaripotiwa zitaleta haki na ulinzi kwa waathirika wa ukatili ambao ni wanawake, wasichana na watoto,” amesema.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa mwongozao huo, Kamishna Msaidizi wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Leah Mbunda amesema ukatili hauchagui wenye ulemavu au wasio na ulemavu.
“Polisi tumewapa kipaumbele wenye ulemavu ili kuhakikisha wanapata haki zao, japo kuna changamoto tunazipata kwa kukosa wakalimani, lakini tukikutana na mtu kama huyu tunahakikisha tunatafuta wakalimani ili watueleweshe.”