Wasichana rika balehe wawezeshwa vifaa vya Sh500 milioni

Mbeya. Wasichana zaidi ya 40,000 wa rika balehe walio katika hatari ya kupata maambukizi ya Virusi vya Ukimwi (VVU) katika mikoa ya Mbeya na Songwe, wamekabidhiwa mashine mbalimbali zenye thamani ya Sh500 milioni.

Vitendea kazi hivyo ni pamoja na mashine za kuoka mikate na keki kibiashara, majokofu ya keki, kutengeneza vyakula vya mifugo, kuchanganyia saruji, mitambo ya kupanda na kuvunia mpunga, vifaa vya muziki, vyerehani vya kushonea mawigi pamoja na mashine za kutengeneza viatu.

Akikabidhi vifaa hivyo leo Jumanne, Septemba 10, 2024 katika ziara yake mkoani Mbeya, Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Wenye Mahitaji Maalumu, Dk Doroth Gwajima amesema mashine hizo ni maalumu ili kuwawezesha kuwa na vyanzo vya kudumu vya mapato na kuondokana na tabia hatarishi.

Mashine hizo amezitoa kwenye kituo cha Tumaini kinachosimamiwa na Shirika la HJFMRI kupitia ufadhili wa Mfuko wa Dharura wa Rais wa Marekani (PEPFAR) kikijihusisha na matunzo kwa vijana na mabinti balehe walio katika hatari ya kupata maambukizi ya VVU.

“Ufadhili wa mashine hizi ni sehemu ya utekelezaji wa mradi katika kuibua na kuimarisha ubora wa bidhaa wanazotengeneza kama sehemu ya kujikwamua kiuchumi, ambapo shughuli hizo za kiuchumi zinawaondoa kushiriki au kuwa katika mazingira hatarishi yanayoweza kuwaingiza katika janga la Ukimwi,” amesema.

Waziri Gwajima amesema Serikali itaendelea kushirikiana na HJFMRI kwenye mapambano dhidi maambukizi ya VVU katika uwezeshwaji mabinti na vijana balehe kiuchumi.

“Niwahakikishie kuwa wizara inatambua jitihada za makusudi na nguvu iliyowekezwa katika kuhakikisha suala hili linafanikiwa.

“Nawaelekeza wakurugenzi wa halmashauri zote za Mkoa wa Mbeya kuweka nguvu za makusudi kusimamia mradi huu kupitia wataalamu wenu hususan maofisa maendeleo ya jamii na ustawi wa jamii katika kuhakikisha wanawafikia mabinti wengi hata ambao hawapo katika mpango wa Dreams,” ameagiza.

Aidha, ameagiza kupitia mikopo ya 4:4:2, ni muhimu mabinti hao nao wakawa sehemu ya wakopeshwaji ili waweze kuongeza mitaji yao na kukuza biashara zao.

“Nimepokea taarifa kuwa, Serikali imetoa mikopo ya Sh28 milioni kwa vikundi vinne vya mabinti wa Dreams. Hongereni sana mabinti kazi iendelee, halmashauri ongezeni pia na mikopo kwa vikundi vingine.”

Gwajima pia ameagiza maofisa maendeleo ya jamii kuwasilisha orodha za taarifa za wadau walio katika maeneo yao kwa lengo la kuisaidia wizara yake kuwasilisha mahitaji ya makundi ya ngazi ya jamii katika uwasilishaji kwenye vikao vya Bunge.

Amesema ukosefu wa taarifa sahihi kutoka kwa maofisa maendeleo ya jamii ngazi za kata kunakwamisha uwasilishaji wa masuala mbalimbali yanayohusu VVU ngazi ya jamii, bungeni jijini Dodoma.

Mnufaika wa mradi wa Dreams kutoka Wilaya ya Mbalali, Janeth Mwakitega (22) amesema aliingia katika mradi huo baada ya kukutana na muelimishaji rika akiwa na miaka 19 lakini tayari alishaathirika na VVU.

“Sikuwa na desturi ya kupima afya wala kwenda kituo cha afya, nimepata huduma tiba, nimewezeshwa kiuchumi, nina genge nauza, namiliki duka nauza nguo za kike na kiume. Usingekua huu mradi nisingefika hapa nilipo.”

Mnufaika mwingine kutoka Wilaya ya Kyela, Dorcas Binala amesema familia yake ilisambaratika baada ya wazazi na dada zake watatu kufariki baada ya kupata maambukizi ya VVU.

Kaka zake wawili nao walichanganyikiwa baada ya kuvuta bangi, hivyo alilazimika kuwalea na yeye kujikimu, hivyo aliingia katika biashara ya kuuza mwili.

“Nilijiingiza huko matokeo yake nikapata mimba aliyenipa alikataa na nilikuwa na wanaume wengi. Nilivyojifungua nikakutana na muelimisha rika akaniunganisha na Dreams.

“Nikapata huduma mbalimbali wakanipeleka kujifunza lugha ya Kiingereza ambayo imeniwezesha kujua lugha, nawawakilisha wenzangu nchi mbalimbali ikiwemo Marekani katika vikao vya maamuzi,” amesema Dorcas.

Mkurugenzi wa HJFMRI Tanzania, Sally Chalamila amesema lengo la mradi wa Dreams ni kutengeneza wasichana rika balehe na kinamama wadogo walio na uchumi imara ili kuwaepusha na maambukizi ya VVU.

“Hatutafikia malengo ifikapo 2030 kama hatutakuwa na wanawake wanaojua afya zao, kujilinda na kulinda kizazi chao, lazima tuwafikie ili wabaki salama katika njia sahihi mojawapo ni kuwanyanyua kiuchumi.

“Wamepata ujuzi na sasa wamejiajiri, mashine hizi mbalimbali zitawasaidia kwa kiasi kikubwa kuzalisha sabuni, mafuta ya alizeti, siagi, mawese, viatu vya ngozi, kusindika kokoa na sasa kuna shamba na jengo wamepewa ili kuchakata zao la kokoa na kutengeneza chocolate lengo tuwe na bidhaa hiyo ambapo tutaiuza mpaka Marekani,” amesema Chalamila.

Mkurugenzi wa WRAIR DOD, Dk Alick Kayange amesema mradi wa Dreams ulikuwa ni wazo lililotolewa na Marekani miaka 10 iliyopita  ambapo ulianzishwa katika nchi 10 zilizoathirika zaidi na VVU na miaka miwili baadaye ukaanzishwa nchini.

Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii, Fatma Toufiq amesema waathirika wakubwa wa ukatili ni watoto na ambao uwezo wa kujitetea hawana, hivyo kuna kila sababu ya kuwawezesha kwa kuwajengea uelewa kuhusu ukatili na pia uwezo wa kiuchumi.

“Wasichana wengi hupata VVU kutokana na hali zao duni za kiuchumi. Tunatamani mabinti wengi hapa nchini wapate maarifa, mafunzo na mabadiliko ya tabia ili pia wanufaike kiuchumi,” amesema Fatma ambaye pia ni Mbunge wa Viti Maalumu.

Related Posts