Aweso atoa agizo mfumo wa malipo jumuiya za watumia maji  

Chato. Waziri wa Maji, Jumaa Aweso  amemuagiza Katibu mkuu wa wizara hiyo kwa kushirikiana na Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira  Vijijini (Ruwasa), kupitia upya mfumo wa malipo kwa jumuiya za watumia maji (GPG) ili kutatua changamoto zinazosababisha  wananchi wakose huduma kwa wakati.

Akizungumza leo Jumanne Septemba 10, 2024 wakati wa uwekaji wa jiwe la msingi mradi wa maji Bwanga uliogharimu Sh1.6 bilioni, Aweso amesema tofauti na ilivyokuwa awali, kwa sasa jumuiya za watumia maji zinapouza maji fedha zinaingia kwenye mfumo wa GPG ambao hawana mamlaka ya kuzitoa endapo kutatokea dharura.

Amesema Ruwasa imeweka mfumo mpya wa malipo kwa jumuiya za watumia maji ambao fedha wanazolipa huingia kwenye mfumo wa GPG.

Pia, amesema lengo la kuweka ankara za maji kwenye Jumuiya za watumia maji ni watu kuchangia na kupata huduma bora.

Hata hivyo, amesema hawawezi kuzitumia hadi wapate kibali kutoka Ruwasa makao makuu, jambo linalosababisha wananchi wakose huduma kwa wakati.

“Mfumo mliouweka ni mrefu, jumuiya zinapopata hitilafu kama umeme kuisha au kifaa kimeharibika inawabidi wapeleke taarifa kwa mkurugenzi wa jumuiya kisha meneja wa mkoa halafu iende makao makuu mchakato ni wa muda mrefu na unaleta adha kwa wananchi,” amesema  Aweso.

Waziri amesema hakuna sababu ya kuweka mifumo ambayo badala ya kuleta ahueni, inaleta changamoto na chuki kwa taasisi.

“Changamoto zilizojitokeza kwenye mfumo wa malipo zishughulikieni, wekeni mfumo rahisi ili pindi fedha zinapohitajika kwa ajili ya marekebisho au kutoa huduma zipatikane kwa urahisi, msiweke mifumo badala ya kuleta ahueni inalete chuki kwenye taasisi, wananchi wanapaswa waendelee kunufaika na huduma wakati wote,”amesema Aweso.

Akisoma taarifa ya utekelezaji mradi wa majisafi na salama Bwanga utakao hudumia wananchi 27,000 Meneja wa Ruwasa Chato Avitus Exavery amesema, hadi sasa mradi umekamilika kwa asilimia 99 na tayari wananchi wameanza kupata huduma.

Amesema mradi huo utahudumia vijiji viwili kati ya vinne vilivyopo Kata ya Bwanga huku chanzo cha maji katika mradi huo kikiwa ni visima viwili vyenye ujazo wa kuzalisha lita 15,000 kwa saa.

Mbunge wa Chato, Merdad Kalemani amesema mradi huo ni miongoni mwa miradi minane mipya inayotekelezwa wilayani humo.

“Hapa kulikuwa na kero kubwa ya maji wananchi kazi yao kubwa ilikuwa kwenda bondeni kutafuta maji ambayo sio salama lakini kulikuwa na hatari ya kuumwa na nyoka,” amesema Kalemani.

Getruda Amos mkazi wa Bwanga, amesema awali changamoto ya maji kwenye kijiji chao ilikuwa kubwa na kulazimika kununua ndoo ya lita 20 kati ya Sh200 hasi Sh500.

Related Posts