WAKATI kesho Alhamisi kikosi cha Yanga kikitarajia kusafiri kuelekea Ethiopia, kuna matumaini yapo kwao ya kufanya vizuri ugenini kabla ya kurudi nyumbani kumalizia kazi.
Kikosi hicho kinakwenda kucheza mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika hatua ya kwanza dhidi ya CBE SA ambao utachezwa Jumamosi ya wiki hii kwenye Uwanja wa Abebe Bikila uliopo Addis Ababa Ethiopia.
Yanga inakwenda Ethiopia kwa tahadhari huku benchi la ufundi la timu hiyo chini ya Kocha Mkuu, Miguel Gamondi likiwa na hesabu mkononi.
Gamondi anafahamu Yanga imekuwa na rekodi mbaya kila inapokwenda Ethiopia kucheza, lakini safari hii amekuja na mikakati anayoamini itawatoa kimasomaso katika dakika 180 za mechi zote mbili kwa maana ya 90 ugenini na 90 nyumbani.
Mipango ya Yanga iliyopo ni kama ilivyokuwa msimu uliopita kushinda ugenini na nyumbani kwani wakati wanatinga makundi baada ya kupita takribani miaka 25 walivuka kwa staili hiyo.
Msimu uliopita baada ya kuisambaratisha Djibouti Telecom kwa jumla ya mabao 7-2 mechi zote hatua ya awali zikichezwa Dar, hatua ya kwanza wakakutana na Al Merrikh ya Sudan mechi ya kwanza ugenini wakashinda 2-0, nyumbani wakashinda 1-0, wakafuzu makundi kwa mabao 3-0.
Ukiangalia msimu huu ni kama imejirudia hilo, mechi mbili za hatua ya awali wamecheza zote Dar dhidi ya Vital’O ya Burundi na kushinda 4-0 kisha 6-0. Hatua ya kwanza wanacheza na CBE wakianzia ugenini kisha nyumbani.
Katika kuhakikisha kila kitu kinakuwa sawa, tayari watu wawili wametangulizwa nchini Ethiopia kuyasoma mazingira na kuandaa sehemu ya timu kufikia.
“Mchezo huu tunauhitaji zaidi kwani tunataka kufanya vizuri ugenini kutengeneza mazingira mazuri ya kumalizia kazi nyumbani,” kilisema chanzo.
“Katika hilo, kuna watu tayari wamesafiri mapema kwenda Ethiopia kwa ajili ya kuweka mambo sawa kabla ya kikosi hakijasafiri. Lengo watu hao kwenda kuweka mazingira mazuri ya timu kufikia.”
Akizungumza na Mwanaspoti, Gamondi alisema ameuona ubora wa CBE baada ya kuwasoma kwenye mikanda ya video na kugundua udhaifu, huku akibainisha kwamba wapinzani wana timu nzuri inayocheza soka la kasi la kushambulia, pia wana wachezaji wenye vipaji na uwezo mkubwa.
“Nimeangalia timu yao ina wachezaji wachezaji ambao wamejiunga na timu ya Taifa ya Ethiopia tofauti na sisi ambapo tuna wachezaji kama 14 wanaoyatumikia mataifa yao.
“Hatua hiyo inaifanya timu yao nzima kubaki ikijiandaa vizuri kulinganisha na sisi, lakini hilo sio tatizo, tuna kikosi imara kitakachoweza kufanya vizuri endapo tu wachezaji wangu wote watarejea kwa wakati na wakiwa fiti,” alisema Gamondi
“Tunakwenda Ethiopia tukiwa tunafahamu kwamba tunahitaji kupata matokeo mazuri ambayo yatatupa nguvu zaidi tutakaporudiana nyumbani. Tunataka kuona tunashinda kwao na kwetu.”
Wachezaji wa kikosi cha Yanga waliopo katika timu zao za Taifa ni pamoja na Aziz Ki (Burkina Faso), Khalid Aucho (Uganda), Prince Dube (Zimbabwe), Djigui Diarra (Mali), Duke Abuya (Kenya), Clatous Chama na Kennedy Musonda (Zambia), Bakari Mwamnyeto, Dickson Job, Ibrahim Bacca, Nickson Kibabage, Clement Mzize, Mudathir Yahya na Aboutwalib Mshery wanaocheza Taifa Stars.
Wakati huohuo, beki wa kulia wa Yanga, Yao Kouassi amerejea mazoezini baada ya kupona goti lililokuwa likimsumbua ambalo lilimfanya kukosekana katika mechi mbili za mwisho dhidi ya Vital’O na Kagera Sugar ambazo zote Yanga ilishinda. Wakati Yao alipokosekana, Gamondi alibadili mfumo kwa kuwatumia mabeki watatu nyuma, lakini kupona kwake na akiwa fiti kucheza, basi atarejea katika mfumo wake wa kuwatumia mabeki wanne.
Timu hiyo inayojulikana pia kwa jina la Ethiopia Nigd Bank, ni klabu ya soka kutoka Ethiopia yenye makao yake jijini Addis Ababa. Ilianzishwa mwaka 1982 ikiwa inajulikana kama Banks SC kabla ya kubadilishwa jina mwaka 2010 na kuitwa Commercial Bank of Ethiopia Sports Association (CBE SA), jina ambalo wanatumia hadi sasa. Msimu uliopita, timu hiyo ilitwaa ubingwa wa Ligi Kuu Ethiopia, huku pia ikiwahi kushinda taji la Addis Ababa City mwaka 2014. Wachezaji wa kutazamwa zaidi kwenye kikosi hicho ni kiungo Basiru Umar ambaye msimu uliopita alicheza mechi 30 za ligi kuu na kufunga mabao saba, beki Fetudin Jemal aliyecheza mechi 29 na kumaliza na mabao matatu, wakati mshambuliaji Kitika Jema akicheza michezo 29 na kufunga mabao sita, huku kiungo Fuad Fereja akicheza mechi 16 na kufunga bao moja.
Msimu huu CBE SA imeingia kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa mara ya kwanza katika historia yake, huku Yanga ikishiriki mara kwa mara na huu ni msimu wa pili mfululizo wanaisaka nafasi ya kucheza hatua ya makundi ya michuano hiyo. Msimu uliopita Yanga iliishia robo fainali.
CBE hapo awali imeshiriki michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika mara mbili mwaka 2005 na 2010 wakitolewa hatua ya awali, suala la kufika makundi kwao ni hadithi wakati Yanga katika Kombe la Shirikisho msimu wa 2022-2023 ilicheza fainali na kupoteza kwa kanuni ya bao la ugenini dhidi ya USM Alger. Nyumbani ilifungwa 2-1, ugenini ikashinda 1-0, matokeo ya jumla yakawa 2-2.
Yanga dhidi ya timu za Ethiopia katika michuano ya CAF ina rekodi ya kuzitoa mara tatu kati ya nne walizokutana huku yenyewe ikitolewa mara mmoja hatua ya mtoano. Yanga mbali ya kuzitoa timu hizo, pia inajivunia rekodi ya kufunga mabao mengi wanapocheza na Wahabeshi hao.
Hata hivyo pamoja na Yanga kuzionea timu za Ethiopia bado mabingwa hao wa kihistoria Tanzania hawajawahi kushinda Ethiopia wakitoka sare mbili na kufungwa mbili wanapocheza ugenini. Yanga ilikutana kwa mara ya kwanza na klabu ya Ethiopia 1969 katika Klabu Bingwa Afrika ikaitoa Saint-George kwa mabao 5-0.
Katika mchezo wa kwanza uliofanyika Ethiopia zilitoka suluhu na mechi ya marudiano Yanga ilishinda 5-0 na kusonga hadi robo fainali.
Kisha Yanga ilikutana na Coffee FC 1998 na kuitoa kwa mabao 3-8 katika hatua ya mtoano wa Ligi ya Mabingwa.
Katika mchezo wa kwanza uliofanyika Ethiopia Coffee FC ililazimisha sare 2-2 kisha mchezo wa marudiano Yanga ilishinda 6-1 nyumbani na kufanikiwa kucheza hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa.
Katika Kombe la Shirikisho mwaka 2011, Yanga ilitolewa kwa jumla ya mabao 6-4, ilianzia nyumbani na kulazimishwa sare 4-4 na Dedebit kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Katika mchezo wa marudiano uliofanyika Ethiopia wenyeji, Dedebit walichapa Yanga mabao 2-0.
Mwaka 2018, ilicheza dhidi ya Welaita Dicha katika Kombe la Shirikisho na kufuzu hatua inayofuata kwa jumla ya mabao 2-1. Mchezo wa kwanza nyumbani Yanga ilishinda 2-0, ilipoenda ugenini ikafungwa 1-0.