Kila ninapowasikia viongozi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) na wanasiasa wakihubiri umuhimu wa amani na utulivu ili maisha ya watu yawe salama na wapate maendeleo, huwa najiuliza maswali mengi.
Miongoni mwayo ni hayo yanayozungumzwa yanatoka moyoni au ni ya mdomoni tu, kwa vile kinachofanyika ni tofauti na kinachopigiwa debe.
Siku zinavyozidi kwenda kuuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2025, hali ya kisiasa inazidi kuzorota na maneno yanayozungumzwa hata misikitini hayaendani na yanayotokea mitaani.
Watu wanapigwa ovyo na sisikii Jeshi la Polisi likiwashughulikia wanaofanya hayo, kana kwamba waliopigwa ni paka shume waliofumaniwa wakila chakula cha masikini.
Tumezisikia kauli mbaya zilizokosa heshima na utu kutoka kwa baadhi ya wanasiasa, lakini ninachokifahamu ni Polisi kuwahoji viongozi wa upinzani tu na wa upande mwingine wanaoamini nchi inaongozwa na ilani ya CCM na siyo Katiba na sheria, hawaguswi.
Wazanzibari nawaambia tena, huko mnakoelekea sio kuzuri na kama leo hamtawajibika, basi huko mbele mtaingia katika kumbukumbu za kutoitendea haki Zanzibar na watu wake.
Nawahurumia wajukuu zenu kwa sababu wapo watoto na wajukuu wa watu waliotesa na kuua ambao leo yanapoelezwa waliyoyatenda ya kutesa watu, kama katika kituo cha Ba Mkwe kilichokuwepo Maisara na nilishuhudia kilipovunjwa mwaka 1985, leo hawana raha wakisikia ujahili uliofanywa na wazee wao.
Maovu waliyotenda watu hawa katika miaka ya 1960 na 1970, yaliwapatia majina kama ya Ba Mkwe, Sancho, Mamba na mengineyo.
Tukumbuke kwa vile ipo leo, basi kesho inakuja na lisilowekwa hadharani leo litawekwa wazi kesho, wiki ijayo au baadaye.
Tatizo la binadamu anapopanda ngazi husahau alikotoka na wakati mwingine badala ya kuteremka kwa ngazi, yaani hatua baada ya hatua, huteremka kwa lifti au kuporomoka kama nyumba ya ghorofa iliyolipuliwa na roketi kama tunavyoona kule Palestina.
Mapashkuna wa kisiasa wa Visiwani wanaoneemeka na kufarijika na siasa za chuki na uhasama, kwa vile zinawanufaisha na sio utumishi kwa jamii, hivi sasa wanashadadia siasa za chuki na uhasama.
Wapo tuliowasikia hata Bara kwamba ushindi kwa CCM katika uchaguzi ni lazima, kama vile wananchi hawana uamuzi. Narejea kusema hii ni hatari.
Baadhi utasikia wanasema Mungu akitaka au asitake, ushindi ni lazima. Kama ni hivyo, kuna haja gani ya kuwa na mfumo wa vyama vingi vya kisiasa?
Wazanzibari wanajua yaliyomkuta mwanasiasa aliyediriki kuwaambia wenzake katika kikao cha ndani kuwa ushindi wa CCM lazima na anayemuogopa Mungu kufanya lolote lile ili ushindi upatikane atoke kwenye ukumbi wa mkutano.
Hee…Mungu hachezewi, kwani dakika sio zaidi ya tatu baada ya kutoa kauli hiyo, alianguka na kuwa marehemu.
Namuomba Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi na siyo kwamba ninamshauri kwa vile amezungukwa na washauri anaowaamini, aitafakari kwa makini hali ya kisiasa Visiwani na akumbuke ahadi alizozitoa yeye na wenzake wa ACT Wazalendo walipounda Serikali ya Umoja wa Kitaifa.
Uamuzi wake wa kuacha kuwa na mikutano na waandishi wa habari kama njia ya kupata habari zaidi, ninadhani umesababisha kutopata habari za ziada za hali halisi iliyopo Visiwani hapa.
Hivi sasa upo wasiwasi na wahka mkubwa Visiwani juu ya kitachotokea katika uchaguzi ujao, kwani chaguzi zote zilizopita zimezalisha mauaji na watu kuwa vilema, yatima na vizuka.
Kila siku unapata taarifa za watu kupigwa ovyo na habari hizi kusambaa mitandaoni, lakini badala ya kusikia waliofanya hayo wamekamatwa, kinachoelezwa ni za watu kuiba simu, kuendesha pikipiki kwa mwendo wa kasi.
Hata kwa kauli zinazosemekana ni za siasa za chuki waliohojiwa ni viongozi wa upinzani tu kisiwani Pemba, kama vile wenzao wa CCM wanayo haki ya kutukana na kuingilia maisha ya faragha ya watu wengine.
Sasa umebakia mwaka mmoja na mwezi mmoja. Ni vizuri pakatafutwa mwafaka ili Zanzibar isirudi ilikotoka na moja ya njia hizo ni kuwapa nafasi waandishi wa habari wamueleze kinagaubaga kinachoendelea mitaani na vijijini.
Wazanzibari, ole wetu. Mti na macho na tusije kujilaumu kwa kisingizio cha “poo simo, umo na hutoki”.
Kama mamlaka hazitaziba ufa siyo tu watajenga ukuta, bali nyumba itaporomoka na kuanza upya kujengwa, wakati uwezo haupo.
Masikini Wazanzibari, hawajijui na hawajitambui, wanadhani siasa za chuki na uhasama ndizo zitawapatia maendeleo. Nawapa pole.