Wahudumu wa Afya DR Congo Wakabiliwa na Changamoto ya Kukosa Chanjo Dhidi ya M-pox – MWANAHARAKATI MZALENDO

Wahudumu wa afya Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) wameelezea wasiwasi wao mkubwa kutokana na kuchelewa kupokea chanjo ya ugonjwa wa Mpox, ambao umeendelea kuenea kwa kasi katika eneo hilo. Katika mahojiano na Shirika la Habari la BBC, wafanyakazi wa afya wa jimbo la Kivu Kusini wamesema wanakabiliana na upungufu mkubwa wa vifaa muhimu huku idadi ya wagonjwa ikiendelea kuongezeka, wengi wao wakiwa watoto wachanga.

Mpox, ugonjwa unaoambukizwa kwa urahisi, umeua watu 635 nchini DR Congo mwaka huu pekee. Huku chanjo zikitarajiwa kuwa suluhisho muhimu katika kudhibiti mlipuko huo, upatikanaji wake bado ni changamoto. Ingawa Tume ya Ulaya ilipeleka chanjo 200,000 nchini DR Congo wiki iliyopita, chanjo hizo bado hazijafikishwa katika maeneo yenye maambukizi makubwa kama Kivu Kusini. Usambazaji huo unatarajiwa kuchukua wiki kadhaa, hali inayoongeza hofu kwa wahudumu wa afya

wanaopambana na ugonjwa huo.

Emmanuel Fikiri, muuguzi anayefanya kazi katika kituo maalum cha kukabiliana na Mpox kilichopo Kivu Kusini, alielezea hali hiyo kwa uchungu, akisema, “Tumejua kupitia mitandao ya kijamii kwamba chanjo hizo tayari zinapatikana, lakini bado hazijafika huku.” Fikiri aliongeza kuwa ni mara yake ya kwanza kutibu wagonjwa wa Mpox, na kwamba kila siku ana hofu ya kuambukizwa na kupeleka ugonjwa huo nyumbani kwa familia yake.

Wahudumu wa afya katika maeneo yaliyoathiriwa wanakabiliwa na hali ngumu huku wakihitaji msaada wa haraka. Fikiri na wenzake wameiomba serikali kufanya juhudi za dharura kuhakikisha chanjo zinawafikia haraka kabla ya hali kuwa mbaya zaidi. Ongezeko la wagonjwa, hasa watoto, linazidi kuwa changamoto kubwa katika jitihada za kudhibiti maambukizi ya Mpox.

Changamoto kuu inayokwamisha usambazaji wa chanjo hizo ni hitaji la kuzihifadhi katika halijoto maalum ili ziwe na ufanisi, na pia ugumu wa kuzifikisha katika maeneo ya vijijini kama Kamituga, Kavumu, na Lwiro ambako mlipuko umeenea kwa kasi.

Wahudumu wa afya wanatabiri kuwa endapo chanjo zitasambazwa mapema, zitakuwa msaada mkubwa katika kudhibiti ugonjwa huo. Hata hivyo, mpaka sasa, juhudi zao zimegubikwa na hofu ya kuendelea kuenea kwa ugonjwa huo.

 

#KonceptTvUpdates

Related Posts