Mchenga yatamba kuwanyoosha wapinzani BDL

BAADA ya Mchenga Star kupata ushindi wa pointi 84-64 dhidi ya Ukonga Kings katika mchezo wa Ligi ya Kikapu Mkoa wa Dar es Salaam (BDL), kocha mkuu wa timu hiyo, Mohamed Yusuph amesema kwa sasa nguvu wamezielekeza katika   michezo mitatu iliyobaki akiahidi ushindi.

Akizungumza na Mwanasposti katika Uwanja wa Donbosco Oysterbay, alisema mkakati wao kuhakikisha wanatoa  vichapo kwa timu hizo kwa lengo la kusafisha njia ya kukamata nafasi mojawapo kati ya nne za juu.

“Kwa kweli lengo letu ni kushika nafasi ya nne za juu zitakazofanya tucheze na timu itakayoshika nafasi ya tano  katika hatua ya nane bora,” alisema.

Yusuph alizitaja timu wanazojifua ili kuzipelekea moto kuwa ni JKT, Jogoo na Mgulani JKT.

Awali, katika mchezo dhidi ya Ukonga Kings, kocha huyo alisema ulikuwa ni mzuri na timu yake ilimridhisha namna ilivyocheza.

Mchenga Star iliongoza katika robo ya kwanza kwa pointi   24-20, 20-15, 22-10, 18-19, ikimshuhudia supastaa Amin Mkosa akiongoza kwa kufunga pointi 24 huku akidaka mipira ya ‘rebound’ mara saba na kutoa asisti saba.

Mchezaji huyo alifuatiwa na Jordan Jordan aliyefunga pointi 13, ilhali upande wa Ukonga Kings aliyeongoza alikuwa ni Stanley Mtunguja aliyetupia 25.

Related Posts