Timu tano zatangulia nane bora BDL

WAKATI zimebaki mechi tatu ili kumalizika kwa michezo 30 ya Ligi ya Kikapu Mkoa wa Dar es Salaam (BDL) kwa kila timu, tayari klabu tano zimetinga hatua ya nane bora.

Timu hizo ni Dar City yenye pointi 51, UDSM Outsiders (51), Savio (49), Mchenga Star (50) na JKT (46).

Nafasi za timu hizo zimepatikana baada ya  matokeo mazuri ziliyoyapata katika michezo 27 ambazo tayari zimecheza.

Timu tatu ndizo zinazotakiwa kuungana na hizo tano na zenye nafasi kubwa ya kufanya hivyo ni ABC yenye pointi 41, Vijana ‘City Bulls’ (41), Srelio (40), DB Oratory (35) na Pazi (33).

Mmoja wa makocha wa kikapu jijini Dar es Salaam John Joseph alisema kati ya timu hizo zinazowania kucheza kucheza hatua ya nane bora yoyote inaweza kucheza hatua hiyo kutokana na namna itakavyochanga karata zake.

Akizungumzia kuhusu ligi hiyo, alisema upinzani wa timu shiriki umeongezeka na kwamba, hiyo ni ishara ya mchezo wa kikapu kuanza kurejea katika zama zake nchini.

Wakati huohuo Kamati ya Ufundi na Mashindano ya BDL imeeleza kuwa timu itakayoshika nafasi ya kwanza katika hatua ya nane bora itacheza na ile itakayoshika nafasi ya nane huku ile ya pili ikikutana na ya saba, ya tatu ikipepetana na ya sita, ilhali ya tano itakutana na ile itakayokamata nafasi ya tano.

Related Posts