MNAZI MMOJA: Kutoka shamba la mihogo, mpunga, minazi hadi siasa

Eneo hili maarufu kama viwanja vya Mnazi Mmoja lipo katikati ya Jiji la Dar es Salaam, lina historia ya aina yake kabla na baada ya uhuru.  Ndilo eneo ambalo mkutano wa kwanza wa TANU ulifanyika hapo mwaka 1954.

Ni eneo lililo katikati ya barabara za Nkrumah, Uhuru, Lumumba na Bibi Titi.

Kwa mujibu wa mwandishi Adeleaus Makwega wa iliyokuwa  Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, eneo hilo awali lilikuwa ni mashamba ya mihogo na mpunga chini ya bwanyenye aliyejulikana kwa jina la Mwinyi Gogo.

Baadaye aliuza eneo hilo kwa Mwarabu Suleiman bin Ahmed aliyepanda minazi eneo lote.

“Enzi ya himaya ya Wajerumani 1891-1916 uwanja ulitumika kama kambi ya wanajeshi waliotoka Sudani (Wanubi) waliohamishwa baada ya vita kuu ya pili ya dunia. Uwanja ulizungukwa na nyumba za matope zilikuwa ni za Waafrika. Palizuka moto mkubwa sana minazi yote iliungua moto ukabakia mnazi mmoja tu (kwa bahati haukuungua moto).Mnazi huo umeacha kumbukizi ya eneo la Mnazi Mmoja,” anasema Makwega katika andiko lake alilotoa katika mtandao wa Michuzi  mwaka 2021.

Anasema ujio wa Mwingereza baadaye na sera  yake ya kutaka mji kuwa na maeneo ya wazi, ukatoa amri ya kubomolewa kwa nyumba zote chakavu eneo hilo mwaka 1927.

Takriban nyumba 170 zikabomolewa na hivyo kulifanya eneo hilo kuwa la wazi na kuanza kuitwa eneo la wazi la Mnazi Mmoja.

Anasema mwaka 1949 serikali ya Mwingereza ilivyoupandisha mji na kuwa manispaa,  eneo hilo likawa linatumika kwa shughuli mbalimbali za kijamii.

Wakati wa vuguvugu la kudai uhuru eneo hilo lilitumika kama viwanja vya mikutano ya wapigania uhuru na wananchi.

Hapo ndipo miaka hiyo usingeweza kuwakosa mashujaa wa Taifa letu kama vile Dossa Aziz Ali, Abdulwahid Sykes, Mwalimu Julius Nyerere, Bibi Titi Mohamed, Thomas Mareale, John Rupia, Abbas Sykes na nduguze na wengineo wengi waliokuwa chachu ya Uhuru.

Eneo hilo kwa sasa lina alama mbalimbali, ukiwamo mnara wa Mwenge wa Uhuru uliojengwa mwaka 1960 na kukamilika mwaka 1961.

Pia kuna sanamu ya mtu anayepiga ngoma, ikiwa ni ishara ya mbiu ya mgambo.

Aidha eneo hilo  kulijengwa ukumbi wa Arnatoglo, uliotumiwa kama sehemu ya mikusanyiko ya kijamii, sherehe na burudani kwa Waafrika.

Ni enzi hizo ungeweza kwenda Arnatoglu na kukuta taarab asili ikitumbuizwa  na vikundi kama Alwatan Musical Club, Egyptian Musica Club na Bombay Musical Club.

Siku za mwisho wa wiki vijana walikwenda pia kucheza muziki wa Kizungu.

Kama una maoni kuhusu habari hii, tuandikie ujumbe kupitia WhatsApp: 0765864917.

Related Posts