UTAMU wa Ligi Kuu Bara unaendelea tena leo kwa michezo miwili, huku macho ya mashabiki yakiwa kwenye Uwanja wa Liti mjini Singida wakati Singida Black Stars itakapovaana na KMC, huku kocha Patrick Aussems akitamba kuendeleza ubabe.
Singida ilianza msimu kwa kishindo kwa kupata ushindi katika mechi mbili mfululizo ikiwa ugenini, ikianza kwa kuichapa KenGold jijini Mbeya kwa mabao 3-1 kisha kuifumua Kagera Sugar kwa bao 1-0 mjini Bukoba, na leo itacheza kwa mara ya kwanza nyumbani msimu huu dhidi ya KMC.
Ni mechi inayozikutanisha timu zinazofundishwa na makocha wa kigeni, huku zikiwa hazichekani katika mechi sita zilizokutana katika ligi hiyo tangu 2020 wakati Singida ikifahamika kama Ihefu SC.
Katika mechi hizo zilizopita kila moja imeshinda mechi tatu kukiwa hakuna sare na kila upande umefunga mabao manne na kufungwa manne, japo msimu uliopita katika mechi ya Kombe la Shirikisho, KMC ilicharazwa nyumbani kwa mabao 3-0 na Singida Black Stars ikitumia jina la Ihefu.
Kutokana na hali hiyo pambano la leo likipigwa saa 10:00 jioni linatolewa macho na kila upande ili kujiongezea heshima msimu huu ambapo Singida inataka ushindi ikae kileleni ikiing’oa Simba wakati KMC ikisaka ushindi wa kwanza kwani mchezo wa kwanza dhidi ya Coastal Union ilitoka sare ya bao 1-1.
Akizungumza na Mwanaspoti, Aussems alisema hawataki kufanya makosa kwenye uwanja wa nyumbani ambao watautumia vyema ili kuhakikisha wanapata matokeo mazuri na kuendelea kusonga mbele kuhakikisha wanafikia malengo yao ya msimu.
“Hautakuwa mchezo rahisi tutaingia kwa kuwaheshimu wapinzani wetu tukiwa na lengo moja la kupambania matokeo mazuri kwenye uwanja wetu wa nyumbani. Matokeo yaliyopita hayawezi kuwa sababu ya kujiamini tumekiandaa kikosi tayari kwa ushindani,” alisema kocha huyo.
Kocha wa KMC, Abdulhamid Moalin alisema amekiandaa kikosi chake vizuri tayari kwa ajili ya kusaka pointi tatu ugenini.
“Hatukuwa na matokeo mazuri kwenye mchezo wa mwisho wa ligi kabla ya ligi kusimama kupisha mechi za timu za taifa, tukiambulia sare dhidi ya Coastal Union. Nimefanyia kazi makosa naamini tutakuwa na mchezo mzuri mbele ya Singida Black Stars,” alisema Moalin.
Timu zote zitategemea nyota wao hatari, KMC ikimtegemea zaidi Ibrahim Elias, Daruwesh Saliboko, Kenny Ally, Rashid Chambo na Juma Shemvuni, huku Singida ikiwa na kina Elvis Rupia, Habib Kyombo, Emmanuel Keyekeh, ilhali ikiwa na nafasi finyu ya kuwapata nyota waliokuwa timu za taifa kama Marouf Tchakei, Mohammed Camara.