‘Ukienda buchani usikubali kuwashiwa feni, unapigwa’

Dar es Salaam. Mamlaka ya Vipimo Tanzania (WMA), imesema kuna namna wafanyabiashara wa nyama kwenye baadhi ya mabucha wanatumia feni katika kuwaibia wateja wao.

Ofisa Mtendaji wa wakala huo, Alban Kihulla ameyasema hayo leo Jumatano, Septemba 11, 2024 alipokuwa akizungumza na waandishi na wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari jijini Dar es Salaam kuhusu majukumu mbalimbali yanayofanywa na wakala huo.

Kutokana na hilo, amewataka wateja kuwa makini nazo au la kutokubali kuwashiwa feni wanapofika buchani.

Akifafanua namna wafanyabiashara hao wanavyoiba, Kahulia amesema feni inapowashwa huwa inaongeza uzito kwenye mizani kutokana na ule upepo.

“Mara nyingi katika kuufanya mchezo huu, huweka mizani sambamba na feni hivyo inapowashwa tu inacheza na hapo ndipo ukifika nyumbani unaona kipimo cha kilo ya  nyama uliyonunua hakifanani na uhalisia,” amesema.

Kutokana na hilo, amewasihi watu wasikubali kuwashiwa feni wanapifika kupata huduma katika mabucha ambapo baadhi hudhani ni katika kujaliwa mteja kumbe wanapigwa.

Hata hivyo, Kahulla amesema pamoja na kuwepo kwa hali hiyo, wanaendelea kutoa elimu kwa jamii pamoja na wafanyabiashara kuhusiana na kupima bidhaa hiyo sahihi.

Kuhusu WMA, amesema imekuwa na majukumu mbalimbali ikiwemo kuhifadhi vipimo vyenye usahihi, kulinda jamii kuepukana na madhara yatakanayo na matokeo ya upimaji usio sahihii.

“Jingine ni kuhakiki vipimo vyote vinavyotumika kwenye sekta za biashara, afya, usalama na mazingira,” amesema mtendaji huyo.

Pia amesema wamekuwa wakitoa ushauri wa kitaalamu kuhusiana na vipimo kwa serikali, mashirika, taasisi na wadau wengine.

Akielezea kuhusu mafanikio, amesema kutokana na tozo mbalimbali kwenye vipimo, wakala huo umeweza kuchangia mfuko mkuu wa Serikali kutoka Sh4 bilioni katika mwaka wa fedha 2018/2019 hadi kufika Sh4.3 bilioni kwa mwaka 2022/2023, huku matarajio yao katika mwaka huu wa fedha ni kuchangia Sh7.7 bilioni.

Kwa upande wa vipimo, Kahulla amesema idadi imeongezeka kutoka kuwa na vipimo 837,306 vinavyohakikiwa hadi kufika vipimo 949,565 kwa mwaka wa fedha 2022/2023.

“Aidha mafanikio mengine tumeendelea kusimamia kwa karibu shehena ya mafuta yaingiayo nchini na ndani ya miaka minne tulipima lita bilioni 27 kati ya hizo lita bilioni 14 zilikuwa kwa matumizi ya hapa nchini na lita bilioni 13 zilisafirishwa nje ya nchi.

Kuhusu changamoto, Kahulia amesema kumekuwepo na maboresho ya mazingira ya ufanyaji biashara nchini, mabadiliko ya teknolojia na ongezeko la uelewa na matakwa ya sheria ya vipimo.

Pia, mtendaji huyo amesema wana uhaba wa watumishi wa ajira za kudumu ambapo mpaka sasa wanao 267 huku mahitaji yakiwa ni watumishi 581.

Wakati matarajio yao ni kuingia kwenye maeneo mapya ya uhakiki wa vipimo, kuendelea kutoa elimu na kuboresha mifumo ya utendaji kazi.

Akizungumza kwa niaba ya waandishi, Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Deodatus Balile, ameitaka WMA, kutumia vyombo vya habari katika kutoa elimu ya vipimo kwa kuwa bado inaonekana wananchi wengi hawana uelewa nayo.

Related Posts