Watetezi haki za binadamu wataka tume huru kifo cha Kibao

Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam

Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC) umeiomba Serikali kuunda tume huru ya kiraia itakayochunguza matukio yote yanayohusisha kutekwa na kupotea kwa watu mbalimbali nchini ili kumaliza changamoto hiyo.

Mtandao huo pia umependekeza kuridhiwa kwa mikataba miwili ambayo imejikita katika kupambana na matukio hayo yaani ule unaopambana na masuala ya utekaji, upoteaji wa watu na mkataba wa masuala ya uteswaji.

Akizungumza Septemba 9,2024 Mratibu Taifa wa THRDC, Onesmo Olengurumwa, amesema Rais Samia Suluhu Hassan ana nia njema ya kupambana na matukio hayo na kumshauri aunde tume huru ya kiraia.

Olengurumwa alikuwa akizungumza kufuatia Kifo cha Mjumbe wa Sekretarieti ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Ally Kibao, aliyefariki baada ya kudaiwa kuuawa na watu wasiojulikana.

“Uongozi wa Rais Samia utaonekana unajali haki za binadamu, haki za Watanzania pale ambapo matukio kama haya yakitokea anakuwa mkali na kuchukua hatua kwa vyombo ambavyo vilipaswa kuzuia lakini vikashindwa na kwa watu ambao wamehusika.

“Pamoja na kwamba rais ametoa kauli tunadhani tunapaswa kwenda mbali zaidi ili kutokomeza matukio kama haya ambayo yanatokea katika sura nyingi, ni vema aunde tume ya kiraia itakayohusisha makundi ya kiraia kwa ajili ya uchunguzi.

“Kwa kauli ya mheshimiwa rais ambaye ameonyesha kuguswa tunaona kwa kuanzia ni hapo, kwa sababu matukio yamekuwa mengi na mheshimiwa rais ndiye mwenye mamlaka ya kulinda amani, usalama wa raia na mali zao kwa mujibu wa katiba,” amesema Olengurumwa.

Olengurumwa amesema hata kama Kibao angekuwa na hatia lakini vitendo alivyofanyiwa vya kikatili hakustahili na kwamba matukio hayo yanaumiza, yanaleta hofu, simanzi kwa taifa ambalo ni la kidemokrasia na linaloendeshwa kwa misingi ya utawala bora.

Amesema matukio hayo yanawagusa kwa sababu kazi zao zinatambulishwa pale ambapo kuna matukio yanayokiuka haki za binadamu na wao wakiwa sehemu ya kuyatatua na kuhakikisha kwamba hayatokei.

“Mtanzania yeyote mwenye nia njema na taifa na mwenye kuitatia mema Tanzania iendelee kuwa na amani na utulivu, matukio kama haya lazima yamguse, yapo matukio yanayohusisha watetezi wa haki za binadamu, wanaharakati na wanasiasa…Watanzania waongeze umakini na kulindana pindi inapotokea wanaona kuna hali ya hatari,” amesema Olengurumwa.

Related Posts