Dar es Salaam. Wakati wazazi wakianza kuangalia sehemu ambazo watoto wao watakwenda kusoma masomo ya kujiandaa na elimu ya sekondari watakapomaliza mitihani ya darasa la saba kesho Septemba 12, 2024 wadau wa elimu wameeleza faida na hasara za kufanya hivyo.
Baadhi wamesema elimu hiyo itamfanya mtoto kujua namna ya kukabiliana na masomo ya sekondari, wengine wakieleza muda huo ni mzuri kwa mtoto kujifunza kazi za nyumbani, huku pia ikielezwa kuhudhuria masomo hayo haimaanishi mtoto atakuwa vyema darasani.
Hayo yameelezwa wakati wanafunzi zaidi ya milioni 1.2 wanatarajia kuingia mtaani baada ya kumaliza elimu ya msingi, watakaotumia zaidi ya miezi mitatu kuingia hatua nyingine ya elimu.
Kwa mujibu wa Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani la Tanzania (Necta), Dk Said Mohamed katika watahiniwa hao, 564,176 ni wasichana na wavulana ni 666,604.
Shule nyingi za binafsi zimekuwa zikiwachukua wanafunzi miezi michache kabla ya kuanza kwa ratiba rasmi ya muhula wa masomo wa Serikali, kwa ajili ya maandalizi ya elimu ya sekondari.
Miongoni mwa maandalizi hayo ni ufundishaji wa somo la Kiingereza na hasa kwa watoto wanaotoka shule za kawaida zisizo za mchepuo wa lugha hiyo.
Hata hivyo, kutokana na kutambua changamoto ya wanafunzi kushindwa kumudu lugha ya Kiingereza, Serikali ilizindua mkakati wa kuboresha elimu mwaka 2022 ambao pamoja na mambo mengine inalenga kuwaandaa wanafunzi kumudu lugha hiyo ya kujifunzia.
Mkakati huo umetenga muda kuanzia Januari hadi Mei kuwa maalumu kwa wanafunzi wanaojiunga kidato cha kwanza kujifunza Kiingereza, ili kumudu stadi za kuandika, kusikiliza, kusoma na kuwasiliana.
Tathmini iliyoifanya ndani ya miezi mitatu mwaka 2023 ilionyesha watoto wa kidato cha kwanza walionyesha umahiri wa lugha na sasa wanakaribiana na wale wa kidato cha pili.
“Masomo ya kujiandaa kuingia kidato cha kwanza yana faida lakini kwa wazazi wenye hela, kwani ndiyo wanaoweza kumudu, lakini haimaanishi kuwa mtoto asiposoma hatakuwa vizuri,” amesema Nichodemus Shauri, Mkurugenzi wa Taasisi ya Funguo.
Amesema mara nyingi masomo hayo hayana kitu kikubwa kinachoweza kumfanya mwanafunzi kushindwa kuelewa vyema pindi atapoanza kusoma na wenzake Januari mwakani, huku akieleza njia hiyo huenda ikawa namna ya shule binafsi kujipatia fedha.
Mtafiti wa Elimu, Muhanyi Nkoronko amesema kwa mwanafunzi ambaye uwezo wake ni mdogo, uwepo wa masomo hayo utamsaidia kutoka hatua moja kwenda nyingine.
“Tatizo ninalolioa ni namna ambavyo wanajifunza, vitu vinafundishwa kwa ujumla, wengi wanaofundisha wanatumia uzoefu ambao wakati mwingine unaweza kumfanya mtoto kurundikiwa vitu vingi ambavyo viko nje ya mtalaa na hawezi kuvitumia baadaye,” amesema Nkoronko.
Amesema ili kukabiliana na suala hilo, ni vyema kuhakikisha watoto wanaandaliwa vizuri katika ngazi ya msingi, ili wasipate shida wanapotaka kuingia ngazi nyingine ya elimu.
Amesema uwepo wa vituo vya kuwaandaa ni kama ishara kuwa lipo jambo linalopaswa kufanyika zaidi katika ngazi za msingi.
Mwenyekiti wa Chama cha Wamiliki wa Shule Binafsi (Tamongosco), Aman Lyimo amesema kitendo cha shule zao kuchukua watoto miezi michache kabla ya Januari hakilengi kuipa mapato shule, bali ni moja ya njia ya kuandaa wanafunzi wanaoweza kuwa wateja wao.
“Wakiingia mapema maana yake Januari inapofika ule woga wa masomo ya sekondari unakuwa umewatoka, mazingira ya shule wamezoea na baadhi ya mada katika masomo wamejifunza japokuwa wakija tutaanza upya.
“Hii haitusaidii sisi tu, inawasaidia pia wazazi kuwa na uhakika wa shule watakazopeleka watoto wao muhula unapoanza asihangaike,” amesema.
Wataalamu wa saikolojia wamesema muda huu ni wa mtoto kujifunza vitu vingine tofauti na darasani.
Wamesema umri wa watoto wengi wanaomaliza darasa la saba ni ule wa balehe, hivyo mzazi anapaswa kuhakikisha anamfundisha mwanaye vitu muhimu na kumuweka tayari kwa hatua nyingine ya kielimu ambayo huenda atakuwa huru zaidi, kwani baadhi huwa ndiyo mara yao ya kwanza kukaa bweni.
“Elimu haipo katika mfumo wa darasani pekee, kipindi cha miezi hii mitatu ni muda wa kumtambua kijana wako, ukuaji wake uko hatua gani kisaikolojia, biolojia na kijamii,” amesema John Ambrose, mtaalamu wa saikolojia.
Amesema muda huu ndiyo mzazi anapaswa kujua imani ya mtoto wake imeimarika kwa kiwango gani, kumfundisha mambo ya dini na kuhakikisha anakuwa imara, ili imsadie mbeleni.
Amesema kwa hali ilivyo sasa elimu ya darasani imepoteza udhibiti wa malezi kati ya wazazi na watoto.
“Darasa la saba ni kipindi cha ukuaji, baadhi wanavunja ungo, waaanza kuona mabadiliko hivyo anahitaji kuona malezi na makuzi ya dhati ya mzazi yanaongezeka.
“Ni kipindi cha kumfundisha mtoto maandalizi ya nyumbani yako hivi, jamii iko hivi, kilimo kiko hivi anatakiwa kukaa na kujifunza kwa sababu mtoto anahama kutoka hatua moja ya kielimu kwenda nyingine ambayo huenda itamfanya kuwa huru zaidi,” amesema.
Muda huu pia amesema ndiyo wazazi wanashauriwa kuwafanyia vipimo vya afya watoto wao, ili kujua hali ya afya zao hata anapochagua shule baadaye iwe rahisi kujua anampeleka wapi.
“Kwenye hili la vipimo shule nyingi huwa zinatoa ile fomu ya kuwataka wazazi wamfanyie vipimo mtoto, watu wengi sidhani kama zile taarifa hujazwa sahihi, matokeo yake mtoto anakwenda shule akipata tatizo taarifa za mwalimu na alizonazo mtoto hazifanani, mtoto anaingia katika matatizo kwa ajili ya jambo hili,” amesema.
Ameshauri wakati huu ni muafaka kwa watoto kutembelea maeneo mbalimbali, ikiwemo mbuga za wanyama na kuangalia uzuri wa nchi.
Sarah Mziray, amesema katika kipindi hiki ambacho kelele za ukatili zinasikika kila kona, anashindwa kujua nini afanye kwa ajili ya mwanaye.
“Hayuko salama, si nyumbani wala shuleni, hii miezi mitatu naiona kama mwaka maana hata nguvu za kumwambia akawasalimie ndugu sina,” amesema Sarah.
Si yeye tu, Yvonna Mapunda amesema kumpeleka mtoto kusoma haimaanishi anakimbia majukumu ya malezi, bali anatamani kutafuta kitu kilicho salama kwake.
“Nikiwa kazini siwezi kumuangalia mtoto muda wote, akiwa shuleni angalau akipata tatizo najua kwa kuanzia, mambo yanayotokea yanaogopesha,” amesema.
Katika siku za hivi karibuni kumekuwa na ripoti kadhaa kwenye vyombo vya habari na mitandao ya kijamii kuhusu matukio ya ubakaji na ulawiti kwa watoto, baadhi yakiwahusisha ndugu wa karibu.
Ripoti ya Takwimu za Msingi Tanzania – 2023 iliyotolewa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) inaonyesha matukio ya ulawiti yaliyoripotiwa mwaka 2023 yalifikia 2,488 ikilinganishwa na kesi 1,586 zilizoripotiwa mwaka 2022.
Kwa upande wa ubakaji, matukio yalikuwa 6,827 mwaka 2022 na kuongezeka hadi kufikia 8,691 mwaka jana.