Timu ya Fountain Gate imeendeleza ushindi ndani ya Ligi Kuu Bara baada ya hii leo kuitandika mabao 2-1 Ken Gold, ikicheza kwa mara ya kwanza kwenye Uwanja wa Tanzanite Kwaraa katika mechi za Ligi.
Ushindi huo wa pili mfululizo, licha ya kuiweka pazuri timu hiyo katika msimamo pia imekuwa ni kama zawadi kwa wapenzi wa soka Mkoa wa Manyara ambao tangu Mkoa wao ulivyogawanywa kutoka Arusha mwaka 2002 haijawahi kushuhudia mchezo wa Ligi Kuu.
Katika mchezo huo uliopigwa kwenye uwanja huo wa Tanzanite Kwaraa uliopo katikati ya mji wa Babati, timu zote zilianza kwa kasi, kila moja ikilisakama lango la mwenzake ili la kusaka bao la mapema.
KenGold ndio iliyokuwa ya kwanza kuandika bao kwenye uwanja huo mapema tu dakika ya tisa kupitia Joshua Ibrahim baada ya kumaliza maridadi pasi mpenyezo kutoka kwa naodha wake Mishamo Daud.
Hata hivyo, Fountain Gate ilisimama vyema na kusawazisha goli ilo dakika ya 42 kupitia AbalKassim Suleiman aliyemalizia vyema mpira wa pili uliotemwa na kipa wa KenGold baada ya shuti la William Edger kumpalia.
Dakika ya 57 Selemani Mwalimu alipeleka furaha kwa wakazi wa mitaa ya Bonga, Kona Nakwa, Sigino, Kiru, Mkoani, Sawe, Mrara, Ngarenaro, Oysterbay, Maisaka, Singe na maeneo mengine ya mji wa Babati kwa kupachika bao la pili na la ushindi kwa Fountain.
Ushindi huo sasa imeifanya timu hiyo kufikisha pointi sita baada ya mechi tatu ikishinda mbili na kupoteza moja, huku ikifunga mabao manne na kufungwa tano.
Kwa KenGold huo ni mchezo wa pili mfululizi kupoteza katika ligi hiyo inayoicheza kwa mara ya kwanza tangu ipande daraja msimu huu, sambamba na Pamba Jiji baada ya awali kulala nyumbani 3-1 mbele ya Singida Black Stars.