Simba yafukua faili la Mpanzu

KAMA uliona bado mapema kwa Simba kutafuta mchezaji wa kumsajili dirisha dogo msimu huu, basi umekosea, kwani Wekundu hao wamegonga hodi tena kwa Winga Mkongoman Elie Mpanzu, huku mwenyewe akifunguka na kuwataja mabosi wa Msimbazi.

Winga huyo aliyekuwa akiichezea AS Vita kabla ya kutimkia Ubelgiji, aliwahi kuhitajika na Simba lakini aliamua kuwakacha kweupe akitoa sababu za kufanya hivyo ikiwamo ishu ya familia, lakini mabosi wa Msimbazi wameamua kumrudia tena huko huko Ulaya.

Mwanaspoti iliwahi kutaarifu kuwa, dili la Mpanzu kutua Simba lilikuwa kwenye utata, huku vigogo wa Klabu hiyo wakiendelea kumganda kabla ya AS Vita kupindua meza dakika za jioni, na Mpanzu kufikia maamuzi ya mwisho na kutimkia kikosi cha KRC Genk ya Ubelgiji. Sasa inaelezwa Simba imerejea tena kwa winga huyo, baada ya kuona kikosi hicho kinahitaji nguvu hasa eneo la kushoto, na mchezaji huyo kuonekana kama amechemka huko Ubelgiji.

Mwanaspoti hili lilipata taarifa za ndani kutoka klabu ya Simba zikieleza kuwa, hatua ya kumrudia Mpanzu imetokana baada ya kugundua kuwa kuna mahali panavuja hasa eneo la winga.

“Kuna mchezaji mmoja itabidi atolewe kama dili la Mpanzu litatiki ili kutimiza kanuni ya kuwa na wachezaji 12 wa kigeni. Hatuwezi tukasema atakuwa nani kwani bado ni mapema lakini kocha ndiye mwenye maamuzi juu ya hili, hivyo ataongea na uongozi juu ya nani apunguzwe,” kilisema chanzo hicho kutoka Simba.

Mwanaspoti lilimsaka Mpanzu na kumuuliza juu ya taarifa hizo naye alisema bado anasubiri hatma yake huko Ubelgiji, lakini viongozi wa Simba wamemtafuta tena kujua kama atakuwa tayari wamuongeze dirisha dogo la usajili.

“Viongozi wa Simba wamenitafuta tena, ila mimi siwezi kuongea chochote kwa sasa, kwani ninachosubiri huku ni hatma yangu tu, ila haina maana kuwa nimefeli.”

Hatua ya Simba kumrudia Mpanzu wanaona bado kikosi chao hakina nguvu kwa winga ya kushoto wakati mwenye asili ya kulia akiwa Joshua Mutale, huku kukiwa na wachezaji wengine kama  Kibu Denis, Ladack Chasambi na Edwin Balua ambaye kuna wakati anachezeshwa upande huo wa kushoto.

Related Posts