Wakati mwingine wachezaji wanafanya vituko vya ajabu, hadi wao wenyewe wanajishangaa, pindi wanapopata utulivu wa kujitathimini baada ya majukumu yao, kuona walifanya vitu vya ajabu.
Mwanaspoti limezungumza na wachezaji mbalimbali kujua wanakuwa wanapatwa na nini hadi wakati mwingine hufanya matukio ya kushangaza uwanjani na majibu yao yatakuchekesha na kukushangaza.
Beki wa Mashujaa, Said Makapu anasema wakati yupo Ihefu walicheza dhidi ya Mbeya City kabla haijashuka daraja. Siku hiyo alianzia benchi, sasa badala ya kutazama kinachoendelea uwanjani, akawa anaangalia jukwaani.
“Kocha akaniambia nyanyuka ukaisaidie timu, ilikuwa dakika kama ya 80 hivi, nilipata shida kujua nikafanye nini, maana sikuangalia mwenzangu alikuwa anapatia wapi ama alikwama wapi, hadi naingia uwanjani nilikuwa sielewi nifanye kitu gani, ninachoshukuru hatukufungwa mechi,” anasema na kuongeza;
“Baada ya kufika kambini, nilijitafakari na kujihoji hivi timu ingefunga ama kutokee sintofahamu uwanjani, kiukweli ni tukio la kijinga ambalo sijawaji kulirudia tena na yapo mengi yanayokuwa yanafanyika kwa wachezaji.”
Beki wa zamani wa Azam FC, Agrey Morris anasema anakumbuka mwaka 2011 wakiwa chini ya Kocha Stewart Hall, walikuwa wanafanya mazoezi ya mechi kushindana mabeki na washambuliaji.
“Nikaleta mbwembwe za kutaka kupiga mpira kwa tikitaka badala ya kufunga kwa wapinzani nikaifunga timu yangu ya mabeki na mimi nikaanguka chini, makocha, wachezaji wakaanza kunicheka hata mimi nikajikuta nacheka, halafu nikajiuliza hivi ingekuwa mechi ya mashindano si ningekuwa nimeigharimu timu,” anasema Morris ambaye kwa sasa anasimamia kituo chake cha soka.
Beki wa zamani wa Yanga, Oscar Joshua anasema kuna mchezaji mwenzake kabla ya kuondoka Jangwani, alimkopesha simu hakumlipa pesa zake wakati, alipokutana naye uwanjani wakati mechi inaendelea akaanza kumdai.
“Katikati ya mechi nikakumbuka namdai pesa, nikamsogelea na kumwambia naomba unilipe deni langu, alicheka sana na kuniambia sasa nitambea na pesa kwenye mechi, ikapita kama wiki akaja akanilipa, ila hadi leo huwa najiuliza akili mbaya kama ile niliitoa wapi,” anasema.
Mshambuliaji wa FC Lupopo, Mtanzania George Mpole ambaye msimu wa 2021/22 alimaliza kinara wa mabao 17 ya Ligi Kuu Bara naye aliwahi kufanya kitu cha kustaajabisha.
Anasimuliwa “Wakati nacheza Mbeya City 2016, tulicheza na timu moja kutoka Njombe mchezo wa FA, tukapata penalti dakika ya 90, tungefungwa tungekuwa tumeondolewa kwenye michuano hiyo.
“Wakati nakwenda kupiga, nikapiga kwa dharau nikakosa, bahati nzuri mwamuzi alisema irudiwe ndio akili timamu ya kwenda kupiga ikanijia, nikapiga nikafunga nadhani ilikuwa ni hatua ya makundi na tukasonga mbele.”
Msimu wa 2015/16 wakati Malimi Busungu anacheza Yanga anakumbuka kituko alichowahi kukifanya Uwanja wa Benjamin Mkapa kipindi hicho ukiitwa Taifa, timu hiyo ilicheza dhidi ya Toto Africans ya Mwanza.
Anasema “Beki wa pembeni Juma Abdul aliumia hakuweza kuendelea na mchezo, kocha Hans Pluijm akanirudisha kucheza namba yake, Simon Msuva akapelekwa acheze namba saba ambayo nilikuwa nacheza.
“Winga mmoja wa Toto akawa anakuja kwa kasi kufunga, ili kuokoa mpira nikamkwatua yeye na mpira tena ndani ya boksi, ile ilikuwa penalti, uzuri mwamuzi akafunika, baada ya mechi mashabiki wa Yanga waliniambia Busungu pale ilikuwa penalti, ila hatukulaumu ile siyo nafasi yako.”
Reliants Lusajo (Mashujaa)
Anasimulia tukio alilowahi kulifanya akiwa Dodoma Jiji kabla ya kupanda “Nilicheza nikiwa siku nne nimetoka kufiwa na mtu wa karibu, niliambiwa nipike penalti ya maamuzi, sikutaka, baada ya kung’ang’anizwa, nikaipiga ovyo ili tusiendelee na mashindano, hicho kitu nikikumbuka najuta, kuona niliigharimu timu.”
“Wakati nacheza Toto Afrika, tulicheza dhidi ya JKT Ruvu, tulipata faulo wakati nipo na mpira mguuni, sikujua kama mwamuzi ameruhusu nipige, nikausukumiza kwa mguu kidogo, akaja winga kwa kasi akaunyang’anya na akatambaa nao, ilibakia kidogo tufungwe, wachezaji wenzangu wakawa wananisema ulitaka kuzingua wewe, hilo tukio silisahau,” anasema.
Mwanasaikolojia Charles Nduki anasema “Wachezaji wanakuwa wanapitia changamoto nyingi, hivyo klabu zinatakiwa kuwaajiri wanasaikolojia wa kuzungumza nao, kabla, wakiwa mchezoni na baada ya mchezo.
“Kuna wakati mwingine wanafanya vituko vinavyoonyesha kabisa kuna shida ya afya ya akili, hivyo wanaweza wakawa wanaona kawaida kumbe wanapaswa kujengwa ili wake sawa.”
KOCHA, MKONGWE WANASEMAJE
Kocha Abdul Mingange ambaye ni Meja Mstaafu, anasimulia baadhi ya vituko vya wachezaji “Kuna mmoja nikiwa Ndanda FC, tulicheza na Yanga, aliumia badala ya daktari awasiliane na mimi akavua viatu akatoka nje, tena nilikuwa nimemaliza sabu na mwingine alikuwa amepigwa kadi nyekundu, hivyo hiyo mechi ilicheza na wachezaji nane, ila tulitoka suluhu.
Anaongeza “Mwingine anajua mechi kesho akatoroka usiku, akarudi amelewa, nikamuuliza inakuaje nataka kukutumia kwenye mechi, akasema akilewa ndio anacheza vizuri na akacheza vizuri, kifupi makocha wana mengi kuhusu wachezaji.”
Nahodha wa zamani wa Yanga, Fredy Mbuna aliwahi kusema “Mchezaji kukaa benchi kuna maana kubwa, ili asome mchezo, pindi anapohitaji anapaswa kwenda kutatua tatizo, ila wengi wao wanakuwa wanajitoa mchezoni.”