Dar es Salaam. Wadau wa siasa nchini Tanzania wametaja sifa ambazo wananchi wanazopaswa kuzingatia wanapowachagua viongozi wa serikali za mitaa, ikiwemo kuwapata wale watakarudisha madaraka kwa wananchi.
Wadau hao wamesema uchaguzi wa serikali za mitaa utakaofanyika Novemba 27, 2024 ni muhimu lakini haupewi uzito mkubwa huku wakisisitiza kiongozi anayepatikana kwa kura za wananchi ndiye atakayewatumikia vyema na si yule anayepitishwa bila kupingwa.
Kuhusu wagombea wa nafasi hizo kwenye mitaa, wamesema wapo wa aina mbili, wanaoingia na wanaotaka kuendelea, ambao wanatakiwa wapimwe tofauti.
Hoja hizo za wadau wamezitoa leo usiku Jumatano Septemba 11, 2024 kupitia mjadala wa Mtandao wa X ulioendeshwa na Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL) na kushirikisha wadau mbalimbali.
Mjadala huo umeongozwa na mada isemayo “Kuelekea uchaguzi wa Serikali za Mitaa zipi sifa za viongozi watakaotufaa.
Akichangia mjadala huo, Ofisa Miradi wa Taasisi ya Wanasheria Watetezi wa Mazingira (Leat), Clay Mwaifani amesema kiongozi anayepaswa kuchaguliwa ni yule anayehitaji uongozi badala ya utawala.
Amesema katika uchaguzi huu watu wapimwe kwa utayari wao wa kutumika na huu uwe uchaguzi wa kujipima kuweka watu wanaorudisha madaraka kwa wananchi.
“Viongozi wanaotufaa katika chaguzi hizi ni wale wanaotokana na watu walio tayari kuwatumikia watu. Mambo ambayo yalitokea mwaka 2019 hatutaki kuyaona, watu kupita bila kupingwa hatutaki kuyaona,” amesema Mwaifani.
Mwanasheria huyo amesema viongozi wanaotakiwa ni wale watakaohakikisha usalama wa raia ni vipaumbele vyao na ni vyema kuwa na viongozi ambao wakiangaliwa usoni wanafanana na kile wanachokisema.
Pia amesema uchaguzi unaohitajika ni ule ambao utaifanya taswira ya serikali za mitaa kurudi kwa watu.
Kihusu sifa hizo, Mhariri wa siasa wa gazeti la Mwananchi, Peter Elias akichokoza mada hiyo ametaja sifa tano ambazo wananchi wanapaswa kuzingatia kumchagua kiongozi wa serikali za mitaa ikiwemo ya kuwa mtu anayetumwa na wananchi.
Amesema imezoeleka viongozi wa serikali za mitaa wanajihusisha zaidi na chama au Serikali na kujisahau ni mwakilishi wa wananchi, hivyo wananchi wanapaswa kuangalia sifa hiyo ya msingi.
Sifa nyingine ni mtu anayehudumia wananchi wake na kusimamia masuala ya usafi, kutatua kero na kusimamia masuala ya ulinzi na usalama.
Ametaja sifa zingine ni kiongozi awe anapatikana kwa urahisi katika sehemu yake, akisema “kumekuwa na changamoto unamtafuta kiongozi wa serikali ya mtaa humpati, hivyo wananchi wanashindwa kupeleka shida zao na kama unavyojua viongozi hawa ni muhimu kwenye jamii.”
Kitu cha nne wananchi wanapaswa kuzingatia wakati wa kumchagua kiongozi ni uadilifu na uzalendo.
“Pia kiongozi anayechaguliwa asimamie haki, awe katikati kwenye pande mbili awe anasikiliza migogoro ya kifamilia na kutenda haki,” amesema.
Akijadili hilo, Katibu Baraza la Vijana Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Bavicha), Mkoa wa Arusha, Clement Manang amesema kiongozi akipitia mchakato safi, akapigiwa kura na na kushinda ndiye atawatunikia vyema wananchi.
Manang amesema kupita bila kupingwa kunaweka ugumu katika kuchukua hatua inapohitajika kufanya hivyo na uwajibishwaji, hata kama viongozi wanakiuka kanuni na taratibu na hata ubadhirifu wa mali.
“Hawa viongozi wasipopatikana katika mchakato safi, tunaweza kupiga kelele hapa na kule lakini hawana watakachofanya kwa sababu hawana kura za wananchi.
“Kiongozi yoyote ambaye ni bora hata kwenye kusoma mapato na matumizi anajiamini na kiongozi bora ni yule anayechaguliwa na watu na akichaguliwa na watu kiburi kinaondoka,” amesema Manang.
Hoja nyingine kwenye mjadala huo imeibuliwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Dk Anna Henga kuwa uchaguzi huo ni muhimu lakini kwa bahati mbaya huwa hauchukuliwi kwa uzito wake.
Dk Henga amesema mpaka sasa imetajwa tarehe ya uchaguzi lakini haijasemwa nani anatoa elimu, mwangalizi ni nani na bado kuna kesi zilizofunguliwa na wanaharakati mahakamani hazijaisha.
“Bado, ni wananchi wachache wanajua kuhusu uchaguzi huu, uandikishaji wa wakazi bado ni changamoto kwa sababu kumbukumbu hazitunzwi kielektroniki na hii inaweza kufanya mtu akapiga kura eneo ambalo si lake,” amesema Dk Henga.
Hata hivyo, amewataka wananchi kuhakikisha viongozi watakaochaguliwa wawe wawakilishi wa kweli na kuhudumia watu wote bila kubagua kwa sababu ya chama, ukabila au namna yoyote.
“Kiongozi awe na maono badala ya kusubiri kugonga mihuri au watu wakihitaji barua, awe na ilani yake kuonyesha tutafanya moja, mbili, tatu kwa namna hii na hii, lakini wapo wanaosubiri matatizo yatokee ndiyo washughulike,” amesema.
Amesema viongozi hao pia wawe watu wanaosimamia misingi ya haki za binadamu na kutohusu watu bila kusikiliza pande zote ili aweze kutenda haki, japokuwa yeye si mahakama, bali kutatua zile changamoto za ndani ya jamii.
Mhadhiri wa Sayansi ya Siasa kutoka Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom), Cornad Masabo amesema watu wanaokwenda kuomba ridhaa ya kuwa viongozi wa serikali za mitaa wapo wa aina mbili na wanatakiwa kupimwa tofauti.
Kundi la wanaogombea wapo ambao si viongozi wa siasa kwa sasa na wako nje ya uongozi na wapo wale waliopo katika serikali za mitaa na wanaomba ridhaa za kurudi tena.
“Hawa wanapaswa kupimwa kwa sifa tofauti na si kutumia sifa moja. Wale ambao hawamo katika uongozi kwa sasa wapimwe kwa kuangalia ahadi zao na kwa kiasi gani zinaweza kutekelezeka,” amesema Masabo.
Masabo amesema watu walio nje ya uongozi pia wanapaswa kupimwa kwa namna ambavyo si wapokeaji pekee bali waweze kufikiri watafanya nini. Pia kiongozi anayefaa lazima ahadi zake ziwe na uhalisia na si ambazo hazitekelezeki.
“Awe anayefikika kirahisi ili aweze kusikiliza watu na kusaidia, kuangalia kiwango chake cha ushiriki katika mambo yanayohusu jamii katika raha na shida, pia namna anavyoweza kuleta watu pamoja na si kuwagawa,” amesema Masabo.
Kwa wale ambao wapo ndani, mbali na vigezo vya awali wao wapimwe zaidi kuangalia muda aliokuwa kiongozi ameleta nini katika nafasi hiyo na kama alichokifanya kinaridhisha na anafaa kupewa dhamana tena.
Pia kiongozi huyo aangaliwe kwa namna gani alitumikia wananchi kuliko taasisi yake anayohusika nayo.
“Pia tuangalie anaweza kuleta nini zaidi, kama alikuwa na miaka mitano anaweza kuleta nini zaidi, sifa hizi ndiyo zitumike kuwapima viongozi hawa,” amesema Masabo.
Kuhusu ajenda ya maendeleo, mwananchi aliyejitambulisha kwa jina moja la Samuel amesema ni vyema kuhakikisha viongozi wanaochaguliwa hasa wa vijiji wawe na uwezo wa kutumia rasilimali walizonazo ikiwemo watu na mistu kuleta maendeleo.
Samuel amesema katika baadhi ya vijiji wapo vijana ambao wabunifu na wasomi lakini kukosekana kwa kiongozi wanaoweza kuwatumia ipasavyo kuleta kuleta maendeleo chanya katika vijiji vyao ni changamoto.
Baadhi ya viongozi badala ya kuwatumia wamekuwa wakishia kuwasema na kuwaita wasomi badala ya kutumia.
“Pia kutumia rasilimali misitu, vijiji vingi wanatumia mapori ya akiba kukata mkaa badala ya kuelewa yana faida gani kwenye kuwaletea maendeleo wananchi na si kuyamaliza, vyema kuwa na viongozi wenye uchungu wanaoweza kusaidia kutumia rasilimali hizi kwa ajili ya vizazi vijavyo,” amesema.
‘Tufanye uchaguzi uwe wa maana’
Hoja nyingine inaibuliwa na mchambuzi wa siasa, Bubelwa Kaiza akisistiza ni muhimu kufanya uchaguzi uwe na maana kwa watu hivyo ni ngumu kufanya uchaguzi bila mpango wa maendeleo au kuuvalisha sera za kimaendeleo.
“Lazima tuhakikishe sera zilizopo katika maendeleo na mipango iliyopo inaendana na uchaguzi wenyewe,” amesema.
Kaiza amesema kupitia uchaguzi unaofanyika ni vyema kuhakikisha wanaopewa dhamana wanajua vitu wanavyokwenda kuvisimamia akitolea mfano wa vijiji ambavyo mara zite vinajitegemea katika mambo mengi ya utendaji tofauti na Serikali za mitaa za mijini zilizo na wakuu wa wilaya na wakurugenzi.
Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Nteghenjwa Hosseah amesema maboresho makubwa yamefanyika katika uchaguzi wa serikali za mitaa utakaofanyika Novemba 27, 2024 ikilinganishwa na miaka iliyopita.
Maboresho yaliyofanyika ni katika kanuni na mifumo na kuwa siku za usoni uorodheshaji wapiga kura utakuwa wa kidijitali, jambo ambalo hata hivyo amesema ni la gharama kubwa.
“Kuna mmoja alizungumzia uchaguzi huu unadharaulika, ni kasumba tu ya watu lakini uchaguzi huu una hadhi sawa na chaguzi nyingine au zaidi kwa sababu ya idadi kubwa ya viongozi wanaochaguliwa na hili limeonekana kupitia mwamko mkubwa wa watu ulioshuhudiwa tangu tangazo limetoka hadi sasa,” amesema.
Akizungumzia mamlaka ya serikali za vijiji amesema vijiji vyote vipo kisheria na pia ni Serikali kamili ambayo inaongozwa kwa mujibu wa sheria.
Kufuatia hilo, amesema kila baada ya miezi mitatu serikali za vijiji huwa zinafanya vikao mara moja jambo ambalo pia hufanyika ila mwamko wa watu kushiriki ndiyo imekuwa changamoto.
Nteghenjwa amesema kitu cha msingi katika uchaguzi huu ni wananchi kumchagua kiongozi wao, jambo ambalo limezungumziwa sana na hatimaye kipengele cha kupita bila kupingwa kilikwishaondolewa.
“Sifa nyingine kubwa ya kiongozi serikali za mitaa lazima awe na uwezo wa kushirikisha wananchi katika mipango na bajeti ili waweze kuamua vitu vyao vyote wanavyotaka katika maeneo yao, kuviwasilishwa ngazi za juu ili wapate bajeti ya utekelezani,” amesema.
Amesema ushirikishaji huo utafanya wananchi kuwa na uwezo wa kulinda kile ambacho wamekiomba.