Geita. Watu wawili akiwemo mwanafunzi wa kidato cha nne wamepoteza maisha baada ya kudaiwa kuvamia kituo cha polisi Lulembela wakitaka kuwadhuru watu waliodaiwa kuwa wezi wa watoto.
Taarifa iliyowekwa na Msemaji wa Jeshi la Polisi usiku huu, David Misime, inasema vurugu hizo zimetokea leo Jumatano Septembe 11, 2024 Saa 8:30 mchana huko Lulembelea Wilayani Mbogwe mkoani Geita.
Amesema katika vurugu hizo, waliopoteza maisha ni mwanaume mmoja ambaye jina lake halijafahamika anaekadiriwa kuwa na miaka 18 -20 na mwanafunzi wa kidato cha nne wa Shule ya Sekondari Lulembela, Theresia John (18) ambaye nyumba yao inatazamana na kituo cha polisi.
Misime amesema chanzo cha vurugu hizo ni baada ya watu wawili kuonekana wakiwa wamebeba watoto wawili na wananchi waliokuwa kwenye mnada wa Lulembelea kuwahisi kuwa ni wezi wa watoto na kuanza kuwashambulia.
“Walipokuwa wanawashambulia alitokea ofisa mtendaji wa kata akawabeba kwenye pikipiki na kuwakimbiza katika Kituo cha Polisi Lulembela baada ya watu hao kwenye gari, akawapeleka kituoni, wananchi wanaokadiriwa kufika 800 walifika kituoni na kuwataka Polisi wawakabidhi watuhumiwa hao ili wawaue,” amedai Misime.
Amesema licha ya Askari Polisi kuwaelimisha na kuwaeleza ni kosa kujichukulia sheria mkononi, wananchi hao walikaidi na kuanza kukishambulia kituo cha polisi kwa mawe wakilazimisha kuwachukua watu hao wawili kwa nguvu ili wawaue.
Misime amesema baada ya askari kuona hali hiyo ya kuhatarisha maisha ya watu na mali za serikali, walilazimika kutumia mabomu ya machozi kuwatawanya watu hao, hata hivyo ilishindikana na wakalazimika kutumia silaha za moto kwa kupiga risasi hewani kwa lengo la kuwatawanya.
Kwa mujibu wa Misime mbali na kushambulia kituo cha polisi kwa mawe wananchi hao pia wamechoma moto gari lenye namba T440 ATW lililokuwa limeegeshwa nje ya kituo hicho.
Uchunguzi wa awali wa polisi umebaini watu waliokuwa wamebeba watoto hao ni Emanuel John (33) mkazi wa Kigamboni Lulembelea aliyekua na mwanawe aliyetambulika kwa jina la Emanuel mwenye mwaka mmoja na miezi kumi.
Mwingine ni Ng’amba Leornad (24) aliyekuwa amembeba mtoto aitwaye John Emanuel mwenye miaka miwili na miezi minane.
Kwa mujibu wa Misime, mama mzazi wa watoto hao, Rachel Luhende (22) amethibitisha kuwa watoto hao ni wake na walikuwa kwa wifi yake na baba yao mzazi pamoja na mjomba wao walienda kuwachukua.
Uchunguzi wa tukio hilo unaendelea ikiwa ni pamoja na kuwakamata watu waliohusika kwenye vurugu hizo.
Hili ni tukio la nne kutokea nchini kwa kipindi kifupi likitanguliwa na matukio matatu yaliyotokea Mkoani Manyara Agosti ,2024 kwa wanachi kuchoma magari moto wakihofia wahusika kuwa ni watekaji wa watoto wenye lengo la kutoa figo.