Pemba. Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) – Zanzibar, Dk Mohamed Said Dimwa amesema tiketi ya kupiga kura ni kuwa na kitambulisho, hivyo amewahimiza wanachama na wananchi wenye vigezo kujiandikisha katika awamu ya pili ya uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapigakura ili wapate uhalali huo.
Kauli hiyo ameitoa leo Jumatano, Septemba 11, 2024 wakati akiweka jiwe la msingi kwenye Tawi la CCM Ngwachani, Wilaya ya Mkoani.
Dk Dimwa amesema njia pekee ya kuhalalishwa kupiga kura ni kuwa na kitambulisho.
“Ndugu zangu lazima tujitokeze kwa wingi, kila mwenye sifa ambaye ametimiza miaka 18 ahakikishe anajitokeza kujiandikisha ili utakapofika uchaguzi mwaka 2025 tuwe na sifa kupiga kura na tuwapigie wagombea wa CCM,” amesema.
Dk Dimwa kisiwa cha Pemba kitaendelea kupata maendeleo endelevu endapo wanachama na wananchi wa kisiwa hicho wataichagua CCM kwa kura nyingi katika uchaguzi mkuu ujao.
“Tumedhamiria kuhakikisha Pemba inapiga hatua kubwa za kimaendeleo na kuwa kituo kikuu cha kukuza uchumi wa nchi,” amesema.
Amesema kupitia ilani ya uchaguzi ya CCM, wataimarisha sekta zote za kiuchumi na kuhakikisha kila mwananchi anakuwa na maisha bora na kipato cha uhakika kinachoendana na hadhi ya Zanzibar kitaifa, kikanda na kimataifa.
Kupitia ziara hiyo amewakumbusha pia wanachama wasiokuwa na vitambulisho vya Mzanzibar mkazi (ZanID) na wana sifa za kisheria kuvipata wahakikishe wanafuata utaratibu kupata vitambulisho hivyo.
Amesema Serikali ya awamu ya nane imeendelea kutekeleza Ilani ya uchaguzi ya CCM ya mwaka 2020/25 kwa kuimarisha sekta za elimu, afya na barabara za kisasa.
Kadhalika, ujenzi wa bandari za kisasa, ujenzi wa uwanja wa ndege wa kisasa, kujenga viwanda katika maeneo huru ya uwekezaji na kupandisha thamani ya mazao ya mwani na karafuu.
Kupitia ziara hiyo Dk Dimwa amesema, Rais Hussein Mwinyi amefanya mambo mengi ya maendeleo na kuvuka malengo ya ilani na dira za maendeleo ya Taifa ya mwaka 2030, hivyo wananchi wanatakiwa kumuunga mkono kwa kuhakikisha anapata ushindi mkubwa katika uchaguzi mkuu ujao.
Pamoja hayo, ametoa wito kwa wananchi wote wanaoamini, kupenda na kuridhishwa na sera za CCM wajitokeze kujiunga na chama hicho ikiwa ni sehemu ya kudumisha demokrasia na maendeleo endelevu kwa wote.
Naye Katibu wa Kamati Maalumu ya NEC, Idara ya Organazesheni Zanzibar, Omar Ibrahim Kilupi,amesema CCM ina uwezo, nguvu na mtaji mkubwa wa kisiasa wa wanachama wenye sifa za kupiga kura zitakazoleta ushindi mkubwa na utakaovunja rekodi katika uchaguzi mkuu ujao.