Arusha. Unaweza kusema umetumika ule usemi wa wahenga wa ‘Mchawi mpe mwana alee’, baada ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Paul Makonda kuwapa kibarua cha ulinzi vijana wa Arusha maarufu kama ‘Wadudu’.
Vijana hao wamekuwa maarufu kutokana na kuogopeka na wakazi wa Arusha kwa madai kuwa ni vibaka na wezi kwa kutumia vitu vyenye ncha Kali kama visu, mapanga na bisibisi. Pia aina za uvaaji wao wa mavazi yaliyowazidi ikiwamo nguo na viatu.
Akitoa salamu za mkoa katika maadhimisho ya kitaifa ya Mei Mosi, Makonda amesema kuwa amekubaliana na vijana hao sasa kulinda mkoa mzima na wakazi wake kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi, viongozi wa dini na Serikali.
Makonda ameyasema hayo leo Mei 1, 2024 kwenye maadhimisho ya kitaifa ya sikukuu ya wafanyakazi Mei Mosi yanayoendelea mkoani Arusha katika viwanja vya Sheikh Amri Abeid ambapo mgeni rasmi ni Makamu wa Rais Dk, Philip Mpango.
“Mheshimiwa Makamu wa Rais, naomba nitangaze rasmi Arusha ni shwari na ni sehemu salama sasa ya kuishi, kwani wale vijana waliokuwa wanaogopeka maarufu kama wadudu sasa hawang’ati tena maana tumekula nao kiapo usiku huu wa leo pale karibu na ofisini kwangu, cha kulinda mkoa wetu na watu wake” amesema Makonda na kuongeza;
“Hawa vijana sasa watatumia vipaji vyao ikiwemo michezo ya bodaboda kujipatia kipato na sisi kama mkoa tutaendelea kushirikiana nao kuhakikisha wanafanikiwa na kuchangia Pato la Taifa”.
Mbali ya hilo, Makonda amesema kuwa vijana hao waliandaa zawadi maalum kwa Rais Samia Suluhu Hassan aliyetarajiwa kuwa mgeni rasmi katika Sherehe hizo, lakini haijafanikiwa hivyo wataona namna ya kuiwasilisha kwake.
Awali kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Arusha, SACP Justine Masejo alisema kuwa vijana hao walishakaa nao kikao na walikubaliana kushirikiana na jeshi hilo kutoa taarifa zote za uhalifu.
Mmoja wa vijana hao, Ally Hamis maarufu kama ‘Husler’ amesema kuwa wameacha kila kitu kwa ajili ya kumuunga mkono Rais Samia na Mkuu wa Mkoa wa Arusha katika harakati za kukomboa vijana na uhalifu.
“Sisi tuna kipaji cha muziki na wengine wanaigiza na kucheza na pikipiki, hivyo tukiwezeshwa maisha yataendelea” amesema Husler.