NAIBU Waziri Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Dk.Festo Dugange anasema kuwa maboresho yaliyofanywa na Serikali kwenye madarasa ya awali yatasaidia watoto kupenda kusoma na kujifunza.
Maboresho hayo ni pamoja na kutengwa kwa bajeti kwa ajili ya utekelezaji wa programu hiyo ambapo fedha hizo zinatumika kujenga madarasa, kununua vitendea kazi na kuboresha miundombinu ya shule za kufundishia watoto hao wakiwamo wenye ulemavu ili waweze kupata elimu sawa na wale wasio na ulemavu.
Awali, Bunge lilipitisha bajeti ya Tamisemi kwa mwaka 2024/25 ambayo pamoja na mambo mengine, Wizara ilitenga fedha kwa ajili ya ununuzi wa vitabu na kuboresha kqa madarasa ya awali.
Bajeti hiyo ilisomwa na Waziri, Mohamed Mchengelwa ambapo amesema kuwa serikali imetenga fedha kwa ajili ya ununuzi wa vitabu na vifaa vilivyoboreshwa vya kufundishia na kujifunzia kwa elimu ya awali kwenye shule 4,500 pamoja na ununuzi wa vifaa saidizi kwa wanafunzi wenye mahitaji maalumu katika shule 130 za msingi na sekondari.
Mchengelwa amesema kuwa, lakini pia, serikali imepanga kutoa mafunzo endelevu ya walimu kazini (MEWAKA) kwenye shule za awali na msingi kwenye halmashauri 140, lengo ni kutekeleza mpango wa shule salama kwenye shule za awali na msingi 2,500.
Akizungumza hivi karibuni, Dk. Dugange amesema kuwa, kutengwa kwa bajeti hiyo kutasaidia utekelezaji wa Programu Jumuishi ya Malezi,Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto (PJT-MMMAM) kufanikiwa kwa sababu watahakikisha kuwa watoto wenye umri wa kuanzia miaka mitatu hadi minane wanasoma na kujifunza katika mazingira bora na salama kwenye madarasa yanayozungumza yaliyosheheni vitendea kazi, walimu waliopewa mafunzo maalum na mazingira bora.
Hata hivyo, programu hiyo inatekelezwa katika afua tano za elimu, afya, lishe, malezi yenye mwitikio na ulinzi na usalama, lengo ni kuhakikisha mtoto anakuja katika hali ya utimilivu.
Ni miaka mitatu sasa imepita toka kuzinduliwa kwa programu hiyo ambapo serikali imekua ikifanya maboresho katika sekta mbalimbali zinazohusu programu hiyo ikiwamo ya elimu.
Naibu Waziri Dugange anaendelea kueleza kuwa, pia Serikali imewajenga uwezo walimu wa madarasa ya awali na wakufunzi kwenye maeneo mbalimbali ya nchi ili kuhakikisha kuwa, watoto hao wanajifunza au kusoma kwenye mtaala ulioidhinishwa.
Amesema kuwa, lengo la kuwajengea uwezo walimu hao ni kuhakikisha kuwa, uelewa wa kuwafundisha watoto wadogo unaongezeka na wao waweze kuwajengea uwezo walimu wenzao.
” Mpango wa Serikali ni kuhakikisha watoto wanasoma katika mazingira bora na ya kisiasa ambayo yanaendana na uhalisia wa madarasa ya awali ikiwa ni pamoja na kuwepo kwa madarasa ya yanayozungumza, walimu wenyw sifa, vitwndea kazi ya kujifunza , miundombinu inayokidhi watoto watu pamoja na wale wenye ulemavu,” amesema Dugange.
Kwa upande wake Mtafiti Mshauri wa HakiElimu, Dk. Wilberforce Meena amesema toka Serikali kuzindua programu hiyo kumekuwa na maboresho mbalimbali katika sekta ya elimu ikiwamo ya madarasa ya awali katika baadhi ya shule hasa zilizopo maeneo ya mijini.
” Tumekua tukifanya tafiti mbalimbali katika sekta ya elimu za kuangalia miundombuni, walimu na vite dea kazi katika shule za mjini na vijini, licha ya kuwepo Kwa changamoto mbalimbali lakini pia kumeanza kuwa na maboresho katika baadhi ya shule ikiwamo kuboresha miundombinu ya madarasa ya awali yenye kuzungumza hali ambayo ni tofauti na miaka ya nyuma.
” Awali, tulifanya utafiti unaojulikana kwa jina la ‘Utafiti wa Elimu ya Awali (ECD)’ ambao ulianza Desemba 2023 na kuzinduliwa April Mwaka huu ambapo kulifikia kaya 1200 za Mkoa wa Dar es Salaam na kuonesha mambo mbalimbali yakiwamo ukosefu wa walimu wenye sifa pamoja na watoto wenye ulemavu kukosa haki sawa na wale wasio na ulemavu, lakini kadri siku zinavyokwenda kumekua na maboresho katika baadhi ya shule kwa kujengwa kwa madarasa ya awali yanayozungumza,” amesema Dk. Meena.
Naye Mkurugenzi wa Taasisi isiyo ya Kiserikali ya Kaya Foundation ambayo inajishughulisha na watoto wenye ulemavu, Anapili Ngome amesema katika baadhi ya shule Mkoa wa Dar es Salaam miundombinu ya watoto wenye ulemavu imeboreshwa ikiwamo kuweka njia ya kupitia kwa watoto hao pamoja na baadhi ya vitendea kazi ikiwamo vitabu na fimbo maalum za walemavu.
Hata hivyo, baadhi ya wananchi wamedai kuwa, kumekua na maboresho katika baadhi ya shule ikiwa ni pamoja na madarasa yanayozungumza ambayo usaidia watoto wa madarasa ya awali kujifunza.
“Kuna kamati za shule ambazo zinashirikisha wazazi katika shughuli mbalimbali zinazohusu watoto wetu, kuna wakati tunaitwa kwa ajili ya kutengeneza zana za kujifunza na wakati mwingine kuchangia kiasi kidogo cha fedha…
“Ili watoto waweze kupata uji, jambo ambalo linatoa matumaini kwa wananchi kuona wanajifunza katika mazingira rafiki,” amesema Omary Khamis ambaye ni mkazi wa Manzese wilayani katika Manispaa ya Wilaya Ubungo jijini Dar es Salaam.
Mkazi huyo ambaye mwanaye anasoma darasa la awali amesema ofisi za serikali za mtaa kuna Ofisa Elimu kata ambaye anasimamia masuala ya elimu katika mazingira husika.
Amesema hayo ni mafanikio makubwa ya kusogeza elimu katika jamii, tofauti na hapo Awali ambapo hakuna na mwamko wowote wa elimu kwa jamii.
” Tuna haja ya kuipongeza serikali katika hili, kwa sababu wameweza kuboresha mazingira ya elimu kwa watoto wa madarasa ya awali Ili kuhakikisha watoto wanasoma na kujifunza Katika mazingira bora,” amesema.
Mkazi wa Kawe iliyopo Manispaa ya Kinondoni katika Mkoa huo, Amina Musa amesema kuwa, kamati za elimu zimekuja zikishirikiana na walimu na wazazi kwa ajili ya kuangalia utoaji wa elimu kwa watoto wetu.
” Hapa kwetu (Kawe) kuna kamati za elimu ambazo zinaundwa na wananchi wenyewe Kwa kushirikiana na walimu, lengo la hizi kamati ni kuangalia utoaji wa elimu kwa watoto wetu, lishe pamoja na mahitaji mengine ya shule, jambo ambalo limesaidia kuongezeka kwa mwamko wa utoaji wa elimu nchini.
“Pia kamati hizo zimekuwa zikiangalia watoto wa madarasa ya awali pamoja na mahitaji yake kwa sababu watoto hao ni wadogo na kwamba wanahitaji uangalizi wa kipekee, jambo ambalo tumefanikiwa kutokana na kuwa tofauti na miaka ya nyuma ambayo watoto wanajilea wenyewe,” amesema Amina.
Ameongeza Serikali inapaswa kuendelea kushirikiana na wadau mbalimbali pamoja na wananchi wenyewe ilii kuhakikisha wanatatua changamoto zote zinazojitokeza kwa watoto wetu wakiwa shuleni au nyumbani.