Tanzania yaiomba EU kuongeza muda mradi uchumi wa buluu

Dar es Salaam. Serikali ya Tanzania imetoa wito kwa Umoja wa Ulaya (EU), kufikiria mpango wa kuongeza muda wa utekelezaji wa mradi wa uongezaji mnyororo wa thamani katika sekta ya uchumi wa buluu (Fish4ACP) nchini humo.

Mradi huo unaotekelezwa katika mataifa 12 ya Afrika, Karibea na Pasifiki, unahusisha uongezaji mnyororo wa thamani wa sekta ya uvuvi.

Kwa Tanzania mradi huo ulioanza mwaka 2021, unatekelezwa katika mikoa ya Kigoma, Rukwa na Katavi inayoguswa na Ziwa Tanganyika.

Hatua ya Serikali kuomba kuongeza muda wa utekelezwaji wa mradi huo, imetokana na kile kubaki mwaka mmoja, uishe muda wake (2025).

Hayo yameelezwa leo Alhamisi, Septemba 12, 2024 na Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega alipozungumza katika mkutano wa mataifa 17 yakiwamo yanayotekeleza mradi huo, uliofanyika jijini Dar es Salaam.

Ulega amesema hatua ya kuomba kuongezwa muda wa utekelezwaji wake, imetokana na manufaa yaliyoshuhudiwa katika mnyororo wa thamani wa sekta ya uvuvi nchini.

Sambamba na kuongezwa muda wa utekelezaji, amesema pia usiishie kufanyika katika Ziwa Tanganyika pekee, bali uhusishe na vyanzo vingine vya maji na mikoa mbalimbali nchini.

“Tanzania tuna vyanzo vingi vya maji, tungetamani mradi uongezewe muda, lakini utekelezwaji wake uhusishe vyanzo vingine kama Ziwa Victoria na bahari zetu,” amesema Ulega.

Ameeleza changamoto kubwa inayoikabili sekta ya uvuvi nchini ni uvuaji wa samaki wachanga na mabadiliko ya tabianchi, lakini mradi huo umekuwa mwarobaini wa hilo.

Kwa sababu hiyo, amesema ni vema uendelee kutekelezwa ili kusaidia upatikanaji wa  suluhu ya changamoto zinazowakabili wavuvi na wasindikaji wa samaki.

Kunachoelezwa na Ulega kinachochewa na mafanikio yaliyoshuhudiwa katika mradi huo, unaotekelezwa kwa kuhusisha wadau wa uvuvi 500 ambao karibu robo tatu yao ni wanawake.

Mafanikio hayo ni kupatikana kwa teknolojia mpya za ukaushaji samaki aina ya sato, sangara na migebuka kutoka siku tatu hadi saa tatu kisha kuwapeleka sokoni.

Mafanikio mengine ni kuongezeka kwa uzalishaji wa samaki waliokaushwa kwa asilimia 10, huku upotevu wa samaki baada ya uvuvi ukipungua kwa asilimia 90.

Waziri wa Uvuvi na Uchumi wa Buluu Zanzibar, Shaaban Ali Othman amesema pamoja na mambo mengine, mradi huo umewezesha upatikanaji wa samaki wa kutosha.

Si hivyo tu, amesema pia maisha ya jamii zinazoishi eneo ambalo mradi unatekelezwa, yameimarika kutokana na shughuli zao kuboreshwa.

Ameeleza mkutano huo ni jukwaa muhimu la kuleta mageuzi ya sekta ya uvuvi katika mataifa husika.

Wito wa kuongezwa kwa muda wa utekelezwaji wa mradi huo, umetolewa pia na Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Profesa Rizik Shemdoe akisema hilo litaiboresha sekta hiyo.

Kwa Tanzania mradi huo, unasimamiwa na Shirika la Chakula na Kilimo Duniani (FAO).

Akizungumza katika mkutano huo, Mkurugenzi Mkuu wa Masuala ya Bahari na Uvuvi wa EU, Charlina Vitcheva amesema bahari inakabiliwa na mabadiliko ya tabianchi, upotevu wa baionuai na uchafuzi wa mazingira.

Amesema ushirikiano wa pamoja, kitaifa na kimataifa ni hatua njema ya kujenga mustakabali bora.

Related Posts