Moshi. Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Kaskazini (KCMC) inapokea watu 40,000 wenye matatizo ya macho kwa mwaka ambapo miongoni mwa wanaobainika kuwa na tatizzo la ukungu kwenye lenzi ya jicho (cataract), ni wenye umri mkubwa.
Hayo yamesemwa leo Mei Mosi, 2024 na Daktari bingwa wa macho, hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Kaskazini (KCMC), Dk William Makupa wakati akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kutembelewa na wadau wa Chama cha Kusaidia Vipofu Tanzania (CBM) kutoka mataifa mbalimbali duniani.
Dk Makupa amesema tatizo la ukungu wa lenzi ya jicho limekuwa kubwa na kadri umri unavyosogea jicho hupoteza hali yake ya uangavu na kuanza kupata ukungu.
Amesema hospitali hiyo kwa kushirikiana CBM wamekuwa wakiwasaidia watu wasio na uwezo kugharamia upasuaji wa macho kwa waathirika hao.
“Ukungu wa lenzi ya jicho una sababu nyingi ikiwemo umri, kadri umri unaposogea lenzi inapoteza ile hali yake ya uangavu na kuanza kupata ukungu, lakini si watu wazima wote wanakuwa nalo, mwingine anaweza kufikisha miaka 100 na asiwe nalo, huku mwingine mwenye miaka 55 anakuwa nalo,”amesema Dk Makupa.
Amesema kufuatia tatizo hilo, hospitali hiyo kwa mwaka imekuwa ikipokea watu wenye matatizo ya macho 40, 000 ambao husaidiwa kupatiwa matibabu ikiwamo kufanyiwa upasuaji.
“Hapa KCMC kwa mwaka tunaona watu 40,000 wenye matatizo mbalimbali ya macho, na tatizo kubwa kuliko yote ni ukungu wa lenzi ya jicho ambapo wagonjwa husaidiwa kwa njia ya upasuaji, uhitaji wa miwani,”amesema Dk Makupa
Amesema Shirika la CBM limekuwa likifadhili huduma za upasuaji wa ukungu wa jicho kwa watu ambao hawana uwezo wa kulipia, pia wamekuwa wakifadhili huduma hizo kwa watoto.
Naye, Mkurugenzi Mkazi wa CBM Tanzania, Nessiah Mahenge amesema wamelenga kupunguza athari za ulemavu wa macho na kuzuia upofu.
Amesema wamekuwa wakitoa zaidi ya Sh1 bilioni kila mwaka katika Hospitali ya KCMC ili kukabiliana na tatizo la macho kwa mikoa ya Kanda ya Kaskazini.
Amewataka wananchi kuwa na tabia ya kupima afya hasa macho kwa kuwa magonjwa mengi ya macho yanazuilika kwa kiwango kikubwa.
Samwel Muna, Mmoja wa wananchi aliyefika hospitalini hapo kupatiwa huduma ya macho kwa mtoto wake, Samwel Said Muna, amesema Shirika hilo limekuwa ni msaada mkubwa kwao.
“Nilipofika hapa KCMC niliambiwa upasuaji wa retina ni Sh750, 000 hadi Sh1 milioni, wakati huo nilikuwa sina hela na nilikuwa nimetoka kwetu Ikungi, lakini baada ya kawaambia sina hizo pesa zote walinitia moyo, kwa kweli nilitafuta fedha kidogo na mpaka mtoto wangu amepatiwa huduma nimetoa Sh450,000 pekee badala ya Sh750, 000,”amesema.