Ulimwengu waadhimisha Siku ya Wafanyakazi – DW – 01.05.2024

Viongozi wa mataifa mbali mbali huitumia siku hii katika kuahidi kuboresha mazingira kwa wafanyakazi wao, ikiwa ni pamoja na nyongeza za mishahara na marurupu.

Kauli mbiu ya maadhimisho hayo mwaka huu ni kuhakikisha usalama na afya kazini wakati dunia ikishuhudia mabadiliko ya tabianchi.

Nchini Ujerumani Kansela Olaf Scholz katika ujumbe wake wa kuadhimisha siku ya wafanyakazi kwa mara nyingine tena kwa uwazi amekataa wazo la kuongeza umri wa kustaafu.

Ujerumani umri wa pensheni kwa waliozaliwa baada ya 1964 ni miaka 67. Hata hivyo unaruhusiwa kustaafu mapema kuanzia miaka 63, lakini malipo ya pensheni yatapunguzwa.

Scholz alisisitiza kwamba wafanyikazi nchini Ujerumani hawajawahi kufanya kazi kwa saa nyingi kama walivyofanya mwaka jana.

Polisi wazuia maandamano Uturuki

Uturuki maandamano ya Mei Mosi mjini Istanbul
Wanachama wa vyama vya wafanyakazi wakizozana na maafisa wa polisi wa Uturuki walipokuwa wakiandamana wakati wa sherehe za Siku ya Wafanyakazi mjini Istanbul.Picha: Khalil Hamra/AP Photo/picture alliance

Nchini Uturuki, ambapo polisi wamefunga eneo la kati la Taksim la Istanbul ili kuzuia maandamano ya kuandimisha Mei Mosi huku Rais Recep Tayyip Erdogan akionya vyama vya wafanyakazi kujiepusha na hatua zozote za uchochezi.

Hatua hizo za kuimarishwa usalama zimejiri siku moja baada ya Waziri wa Mambo ya Ndani Ali Yerlikaya kusema mamlaka imetenga maeneo 40 kwa ajili ya sherehe za Mei Mosi isipokuwa eneo la Taksim.

Ofisi ya gavana wa Istanbul imetangaza baadhi ya barabara zitafungwa huku vikwazo vikiwekwa kwa usafiri wa umma kama sehemu ya hatua za usalama.

Katika hotuba yake Erdogan amesisitiza kufanya mkutano katika maeneo yaliyopigwa marufuku kunadhihirisha “kutokuwa na nia njema”.

Erdogan amedai kuwa upinzani na baadhi ya “makundi ” yalitaka kuharibu shamra shamra za kuadhimisha Mei Mosi kwa wito wao wa kulazimisha kukusanyika kwenye uwanja wa Taksim.

Soma pia:Maandamano yatawala siku ya wafanyakazi 

Jukwaa la kuwasilisha malalamiko jumla

Mei Mosi -Maandamano mjini Seoul
Wafanyakazi kutoka Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi nchini Korea (KCTU) wamehudhuria mkutano wa hadhara kuadhimisha Mei Mosi mjini Seoul, Korea Kusini.Picha: Kim Soo-hyeon/REUTERS

Nchini Korea Kusini maelfu ya wafanyikazi wamekusanyika katika maandamano ya amani kushinikiza haki zaidi za wafanyikazi. Matukio ya Mei Mosi pia yamewapa wengi fursa ya kuwasilisha malalamiko jumla ya kiuchumi pamoja na matakwa ya kisiasa.

Afrika mashariki, Maadhimisho ya siku ya wafanyakazi nchini Tanzania yanafanyika katika viwanja vya Sheikh Amri Abeid, jijini Arusha.

Wakizungumza na vyombo vya habari vya ndani baadhi ya wafanyakazi waliobeba mabango nyenye ujumbe mbalimbali ikiwemo suala la nyongeza za mishahara, wamesema wana matumaini ya kusikia habari njema kutoka kwa viongozi wao.

Soma pia: Wafanyakazi waandamana Ujerumani na Ufaransa kuadhimisha Mei Mosi

Nchini Kenya rais William Ruto ameongoza sherehe hizo katika bustani ya Uhuru.

Huku haya yakijiri shirika la kazi la umoja wa mataifa ILO, limesema kuwa Idadi kubwa ya wafanyakazi ulimwenguni kote wanakabiliwa na hatari nyingi za kiafya zinazohusiana na mabadiliko ya tabianchi, huku likionya kwamba kanuni zilizopo zinatoa ulinzi duni kwa wafanyakazi.

Soma pia: Mabadiliko ya Tabianchi yanavyoathiri wafanyakazi duniani

Katika ripoti yake iliyotolewa Jumatatu wiki hii shirika hilo limesema kuwa Idadi kubwa ya wafanyakazi tayari wanakabiliwa na hatari hizo na huenda idadi hiyo ikaongezeka huku ikibainisha kuwa waathirika wakubwa ni wafanyakazi wa mashambani na wengine wanaofanya kazi nzito katika maeneo yenye joto kali.

 

Related Posts