Mbarawa akagua ujenziwa matenki ya kuhifadhia mafuta TPA

 

WAZIRI wa Uchukuzi Profesa Makame Mbarawa ametembelea mradi wa ujenzi wa matenki maalum ya kuhifadhia mafuta (Oil Terminal) wa TPA unaofanyika katika wilaya ya Kigamboni jijini Dar es Salaam. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea). 

Mradi huo unahusisha ujenzi wa matenki makubwa 15 yenye uwezo wa kuhifadhi ujazo wa lita 378000 za mafuta pindi yanapoingizwa nchini na kuumwagia sifa utekelezaji wake.

Akizungumza wakati wa ziara hiyo katika eneo la ujenzi lililopo katika kata ya Tundwi, Profesa Mbarawa amesema kuwa ujenzi huo utakaochukua muda wa miaka miwili utasaidia katika kuboresha ufanisi wa bandari na kupunguza foleni ya meli za kupakua mafuta ambapo meli moja hutozwa wastani wa faini ya Sh milioni 50 kwa siku moja wakati ikiwa katika foleni ya kupakua mafuta hayo.

Kwa mujibu wa Profesa Mbalawa, ufinyu wa matenki ya kuhifadhia mafuta ulisababisha wasafirishaji kutozwa kiasi kikubwa sana cha pesa na mwisho wa siku gharama hizo pia ziliwagusa wananchi.

“Wakati mwingine meli hulazimika kusubiri kupakua mafuta hata zaidi ya wiki moja, hii inaonyesha ni kwa kiasi gani wasafarishaji wa mafuta wanaumia na faini hii,” amesema Profesa Mbarawa.

Amesema ili kuifanya bandari ya Dar es Salaam kuwa moja ya bandari zenye ushindani duniani, Serikali imeamua kufanya ujenzi huo wa matenki 15 ambao sasa meli hizo zitatumia masaa machache kupakua nishati hiyo na kuondoka.

Pia ujenzi huu utafanya kazi ya usambazaji wa mafuta hayo kwenda kwa wateja ( makampuni ya kuuza mafuta) kwa urahisi sana na kukabiliana na uhaba wa mafuta unaoweza kutokea.

Pia amesema kuwa ujenzi wa matenki hayo utaifanya Serikali kuwa na hifadhi ya kutosha ya nishati hiyo kwa ajili ya usalama wa nchi.

“Nikiwa kama Waziri wa Uchukuzi, nimefurahi sana kuona mradi huu hatimaye unatekelezwa na naupongeza sana uongozi wa TPA kwa hatua hii,”

“Tulijaribu mara kadhaa huko nyuma lakini tulishindwa, ila mipango thabiti ya bodi na uongozi wa TPA umepelekea kutekelezwa kwa mradi huu,” amesema Profesa Mbarawa.

Akizungumzia mradi huo, meneja wa mradi huo Mhandisi Hamis Hassan Mbutu amesema mradi huo unategemewa kumalizika kwa wakati na kuwa na tija kwa bandari hiyo na Serikali kwa ujumla katika kukusanya ushuru.

Awali, akiongea kabla ya kumkaribisha Profesa Mbarawa, Mkurugenzi Msaidizi wa TPA Juma Kijavara amesema mkataba wa ujenzi huo wenye thamani ya shilingi bilioni 678.6 ulisainiwa rasmi Februari 26, 2024 ambapo tayari Mkandarasi China Railway Major Bridge Engineering Group ameshalipwa kiasi cha Sh bilioni 9.9 kuanza ujenzi huo.

Akimuelezea Profesa Mbarawa hatua za utekelezaji wa mradi huo, Mhandisi Wen Hongyuan kutoka China Railway amesema kuwa mradi huo kwa sasa upo katika asilimia 5 ya utekelezaji ambapo tayari kazi ya kusafisha eneo la ujenzi na ofisi za wajenzi zimekamilika.

Akifafanua mgawanyo wa matenki hayo, amesema ujenzi huo utahusisha matenki 6 kwa ajili kuhifadhia mafuta aina ya Diesel, matenki 5 ya kuhifadhia Petroli na matenki matatu kwa ajili ya kuhifadhia mafuta ya kuendeshea ndege.

About The Author

Related Posts