Ugonjwa wa asubuhi ‘morning sickness’ uko hivi

Katika maisha ya kila siku kwa upande wa kinamama katika huduma za afya ni kawaida kuwahi kukutana na neno la kingereza ‘morning sickness’ kwa Kiswahili ugonjwa wa asubuhi.

Ni hali ambayo huwa ni kawaida kuwapata kinamama wajawazito wakati mimba iliyotungwa ikiwa change, yaani kwenye muhula wa kwanza katika wiki ya sita tangu mimba kutungwa.

Ugonjwa wa asubuhi ni hali ya kuhisi kama kutapika au kichefuchefu au kujisikia hovyo hovyo mara baada ya kuamka. Hali hii hutokana na mabadiliko yanayotokea mara tu mimba inapotungwa.

Pamoja na kuitwa hivyo lakini dalili zake zinaweza kuathiri wakati wowote wa siku au usiku au kujisikia mgonjwa mchana kutwa. Ni hali isiyofurahisha inayoweza kuathiri maisha ya kila siku.

Kwa kawaida hali hii huwa hovyo zaidi katika wiki ya tisa na huisha katika wiki ya 16 hadi 20 ya mimba, ni tatizo ambalo halimweki mtoto aliye katika nyumba ya uzazi katika hatari yoyote ya kiafya.

Ingawa hali hii inaweza kuwa mbaya na kuleta aina ya ugonjwa wa ujauzito inayoitwa ‘hyperemesis gravidarum’ inayoweza kusababisha upungufu wa maji mwilini au kutopata virutubishi vya kutosha kutoka kwa lishe.

Hii ikitokea inahitaji matibabu ya kitaalam, wakati mwingine mjamzito anahitajika kulazwa katika huduma za afya.

Wakati mwingine maambukizi ya mfumo wa mkojo UTI yanaweza pia kusababisha kichefuchefu na kutapika. Hivyo ni muhimu kufika kituoni kwa ajili ya huduma ya kwanza ili kubaini sababu.

Ikiwa una dalili za ugonjwa wa asubuhi, mwambie daktari wako au mtoa nuduma wako wa afya mapema.

Dalili za ugonjwa wa asubuhi hujitokea zenyewe mara kwa mara lakini pia zinaweza kusababishwa na baadhi ya vyakula, harufu, joto, mfadhaiko na mambo mengine.

Jinsi ugonjwa wa asubuhi unavyohisi unaweza kuanzia kuwa na wasiwasi kidogo, kama vile kuwa mgonjwa kidogo, hadi kichefuchefu na kutapika zaidi.

Kichefuchefu kwa wajawazito nyakati za asubuhi ni dalili ya kawaida. Na mara nyingi sababu inaweza kuwa ni uchovu, njaa au upungufu wa maji mwilini.

Hali zingine za kiafya ambazo zinaweza kusababisha kichefuchefu ni pamoja na sukari ya juu au ya chini ya damu, kujaa kwa asidi na hali ya afya ya akili.

Ukiona viashiria na dalili kama kuwa na mkojo wa rangi nyeusi sana au hujakojoa zaidi ya saa 8, kujisikia dhaifu sana, kizunguzungu au kuzimia wakati wa kusimama au kuwa na maumivu ya tumbo. Kuwa na joto la juu, kutapika damu na kupoteza uzito fika haraka kituo cha afya.

Kwa bahati mbaya hakuna matibabu ambayo yatafanya kazi haraka kwa kila mtu, kwa ugonjwa wa asubuhi kwani kila ujauzito una ustahimilivu wake dhidi ya dawa za matibabu.

Yapo baadhi ya mabadiliko yanaweza kufanywa katika lishe na maisha ya kila siku ili kujaribu kurahisisha dalili hizi ikiwamo kupumzika sana kwani uchovu unaweza kufanya kichefuchefu kuwa juu zaidi.

Vile vile epuka vyakula au harufu zinazokufanya kuhisi hali hiyo na kula vyakula vikavu kavu kama kwakwaru za viazi au mihogo au biskuti. Ingawa ugonjwa wa asubuhi si tishio, fika katika huduma za afya kwa ushauri, uchunguzi na matibabu zaidi.

Related Posts