Waendesha mashtaka wa mjini Munich wamesema kijana huyo anayedaiwa kuwa mfuasi wa itikadi kali za kiislamu amekamatwa kwa tuhuma za kupanga tukio baya la vurugu ambazo zingehatarisha usalama. Wameeleza kuwa hivi karibuni mtu huyo alinunua visu vikubwa viwili vyenye urefu wa karibu sentimita arobaini.
Kijana huyo anadaiwa kuwa alipanga kufanya tukio hilo katika mji wa Hof Kaskazini mwa jimbo la Bavaria wakati wanajeshi wakiwa kwenye mapumziko ya chakula cha mchana. Wameongeza kuwa mtuhumiwa alipanga kuwauwa wanajeshi wengi kadri ya uwezo wake na kuwatia hofu raia. Meya wa mji wa Hof, Eva Döhla amevishukuru vikosi vya ulinzi na usalama kwa kuzuia uhalifu huo usitokee.
Vikosi vya ulinzi na usalama vya Ujerumani vimekuwa katika hali ya tahadhari kubwa kutokana na kitisho cha mashambulizi ya itikadi kali za Kiislamu tangu vita vilipoanza katika Ukanda wa Gaza baada ya Kundi la Hamas kufanya mashambulizi ndani ya Israel Oktoba 7 mwaka uliopita.
Soma zaidi: Watu 6 wajeruhiwa katika shambulio jipya la kisu Ujerumani
Mapema mwezi huu, polisi walimuuwa mtu mmoja aliyewashambulia maafisa kwa risasi katika kile kilichodaiwa kuwa shambulio la kigaidi kwenye ubalozi mdogo wa Israel mjini Munich.
Tukio hilo lilijiri wakati wa kumbukumbu ya mauaji ya mwaka 1972 dhidi ya wanariadha wa Israel katika michezo ya Olimpiki iliyofanyika Munich yaliyofanywa na Wanamgambo wa Kipalestina.
Mtuhumiwa huyo wa shambulio la ubalozi huo wa Israel alikuwa kijana wa miaka 18 raia wa Austria. Kijana huyo katika siku za nyuma aliwahi kuchunguzwa na mamlaka za nchi yake kwa tuhuma za kujihusisha na ugaidi lakini kesi hiyo ikafutwa.
Uhalifu umeibua mjadala mkali kuhusu wahamiaji Ujerumani
Shambulio hilo lilifuatiwa na mkururo wa mashambulizi ambayo yamechochea hali ya ukosefu wa usalama nchini Ujerumani hali iliyoibua mjadala mkali kuhusu uhamiaji.
Itakumbukwa kuwa, watu watatu waliuwawa mwezi uliopita kwa kuchomwa visu katika tamasha kwenye mji wa Solingen magharibi mwa Ujerumani. Mtuhumiwa katika mkasa huo ambao kundi la dola la Kiislamu lilidai lilihusika, alikuwa kijana raia wa Syria aliyekuwa kwenye mpango wa kurejeshwa kwao.
Kisha lilifuata shambulio la kisu katika mji wa Manheim la mwezi Mei lililosababisha kifo cha askari mmoja na pia maafisa walilihusisha na kali za Kiislamu. Serikali ya Kansela Olaf Scholz tayari imeshatangaza kuweka vituo vipya vya ukaguzi katika mipaka yake yote na imeahidi kuharakisha kuwarejesha makwao wahamiaji wasio na haki ya kuishi Ujerumani.