Dar es Salaam. Katikati ya sherehe ya Siku ya Wafanyakazi Duniani ‘Mei Mosi’ Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (Tucta) limetaja mambo tisa yanayowasibu wafanyakazi nchini na kupendekeza utatuzi wake.
Miongoni mwa mambo hayo ni kupandishwa kwa mishahara, usuluhishi wa migogoro, ajira za mikataba, likizo ya uzazi kwa wanawake na marekebisho katika kikokotoo.
Katika sherehe hizo Rais Samia Suluhu Hassan aliyealikwa kuwa mgeni rasmi, amewakilishwa na Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango.
Kwa mujibu wa Tucta, kuwepo kwa changamoto hizo kunakwaza ari na shauku ya ufanyaji kazi miongoni mwa wafanyakazi nchini, ikisisitiza Serikali ichukue hatua kuleta suluhu.
Hayo yameelezwa jijini Arusha leo Jumatano, Mei Mosi, 2024 na Katibu Mkuu wa Tucta, Henry Mkunda aliposoma risala kwa niaba ya vyama vya wafanyakazi kwenye maadhimisho hayo.
Kauli mbiu ya kitaifa ya maadhimisho hayo ni ‘Nyongeza ya mishahara ni msingi wa mafao bora na kinga dhidi ya hali ngumu ya maisha.’
Risala hiyo kwa mujibu wa Mkunda, iliakisi maneno ya kauli mbiu ikikumbusha nafasi na mchango wa mishahara katika kufikia maisha bora ya wafanyakazi.
Amekiri maboresho ya mishahara yamefanyika kwa sekta binafsi na umma, ambayo hata hivyo amedai hayajakidhi hali ngumu ya maisha iliyopo.
Kwa sababu hiyo, Mkunda amesema wafanyakazi wanashindwa kukidhi mahitaji yao na familia.
“Mishahara nadhifu (mizuri) ina uhusiano mkubwa na upatikanaji wa mafao stahiki ya wastaafu, kwani kadri mshahara unavyokuwa mdogo na ndivyo mafao yanavyokuwa finyu,” amesema.
Kuboreshwa kwa viwango vya mishahara, amesema ndiyo namna pekee itakayowezesha kuondokana na mafao kiduchu kwa wastaafu.
Amesema utaratibu wa kupitia upya kima cha chini cha mshahara wa sekta binafsi kila baada ya miaka mitatu unapaswa kuendelezwa.
Katika risala hiyo, Mkunda amesema dhamira ya Serikali kuongeza posho kwa wafanyakazi inaathiriwa na kodi zinazotozwa kwenye mapato yasiyo ya mshahara.
“Tumeshuhudia wafanyakazi wakikatwa kodi ya mshahara (Paye) kwenye posho zote wanazolipwa, nyumba, usafiri, maji, umeme, mawasiliano, samani na muda wa ziada, hizi zinapunguza uwezo wa mtumishi anapokuwa anatumia fedha hizo,” amesema.
Akijibu hilo, Dk Mpango amesema Bodi ya Kima cha Chini cha Mshahara kwa sekta binafsi na umma zipo na zinaendelea na kazi.
Amesema bodi hiyo hasa kwa sekta binafsi ndiyo iliyochangia kufikia uamuzi wa kima kipya cha chini cha mshahara kwa sekta binafsi kilichotangazwa Novemba 2022 na kuanza kutumika Januari, 2023.
Ameeleza sheria inaitaka bodi ifanye majukumu yake kila baada ya miaka mitatu na ni amri ya kupitia kima cha chini cha mshahara.
Dk Mpango amesema utafiti wa kina wa kima cha chini cha mshahara kwa sekta binafsi utakaojumuisha sekta ndogo-ndogo unafanyika.
“Nawasihi wajumbe wa bodi kutoka Tucta mshiriki ili kupata matokeo yatakayoendana na muda sahihi,” amesema.
Mkunda amesema kumekuwa na migogoro isiyo ya lazima baada ya Serikali kufuta baadhi ya vifungu vya mikataba ya hali bora kwenye taasisi za umma kwa kutumia waraka, bila kujali mikataba inayofutwa kwa makubaliano ya pande mbili.
Ametaka mikataba hiyo iendelee kuheshimiwa na kutumika kwa mujibu wa makubaliano ya awali na iwapo kuna mabadiliko uzingatiwe utaratibu wa pamoja.
Dk Mpango amesema hakuna ukiukwaji wa sheria uliofanywa na Katibu Mkuu Utumishi katika kuvunja vifungu hivyo vya mikataba.
Amesema kilichofanyika ni kwa mujibu wa sheria, inayotaka utekelezwaji wake uzingatie masuala ya kibajeti.
Hata hivyo, amesema ni muhimu kuwepo masilahi kidogo lakini yanayotekelezeka kuliko kuweka makubwa yasiyotekelezeka.
Katika risala, Mkunda aliibua hoja ya uwepo wa wafanyakazi katika halmashauri wanaolipwa kwa mapato ya ndani, badala ya mfuko mkuu wa Serikali.
Utaratibu huo, amesema unawafanya baadhi yao kukosa haki za msingi kwa sababu baadhi ya halmashauri zina uwezo mdogo wa kukusanya mapato.
“Mara nyingi wanakosa haki za msingi zikiwemo huduma za afya, mafao ya kustaafu na hata kushindwa kuwasilisha michango yao,” amesema.
Amependekeza Serikali kubadili utaratibu huo na kutoa haki kwa kila mfanyakazi alipwe na mfuko mkuu.
Katika hilo, Dk Mpango amesema Serikali inaendelea na utekelezaji wa kuwaondoa watumishi wanaolipwa kwa vyanzo vya ndani.
Kuanzia Julai, 2024 amesema watumishi 473 kutoka halmashauri 101 zilizobainika kutokuwa na uwezo wa kulipa mishahara watumishi wake watalipwa na mfuko mkuu wa Serikali.
Amesema Sh3.5 bilioni zimetengwa kwa ajili ya kazi hiyo, huku tathmini ya mara kwa mara ikitarajiwa kufanyika kubaini uwezo wa kifedha wa halmashauri husika.
Hata hivyo, amesema anatarajia halmashauri zitasimamia vema fedha za mapato ya ndani na kutekeleza huduma za kijamii, huku akizitaka kubuni vyanzo vipya na kusimamia matumizi yake.
Mkunda pia iliibua hoja ya kurudishwa kwa Mamlaka ya Usimamizi wa Sekta ya Hifadhi ya Jamii (SSRA), iliyofutwa tangu mwaka 2018.
Amesema tangu ilipofutwa, kumeundwa kitengo chini ya wizara husika na ajira kwa ajili ya kudhibiti na kusimamia mifuko ya hifadhi ya jamii, akisema si jambo jema.
Tucta inapendekeza kurudishwa SSRA kwa kuwa ilikuwa na manufaa kwa wafanyakazi.
“Utaratibu wa sasa haukidhi malengo yaliyokusudiwa kwa kuwa Serikali ni mfadhili wa mifuko na wakati huohuo inakuwa mdhibiti na msimamizi wa mifuko,” amesema.
Kwa mujibu wa Mkunda, mwaka 2022 yalifanyika mabadiliko kwenye kanuni za kukokotoa mafao ya wafanyakazi wastaafu wa umma na binafsi.
Katika hilo, ameishukuru Serikali kwa hatua ya kuwashirikisha wafanyakazi katika mchakato huo, tofauti na ilivyofanyika awali.
Pamoja na hayo, amesema miaka miwili tangu utekelezwaji ulipoanza, tathmini ndogo imeonyesha wafanyakazi hawaridhishwi na kanuni mpya za kukokotoa mafao ya wastaafu.
Kwa kuwa mifuko inaonekana kuimarika sasa, amependekeza kanuni hizo ziboreshwe na kuleta mafao bora kwa wastaafu bila kuathiri mifuko hiyo.
Tucta pia imezungumzia ajira za mikataba zinazotolewa kinyume cha matakwa ya sheria ya ajira na mahusiano kazini.
Amesema ajira hizo ni za mikataba ya miezi mitatu na nyingine mwaka mmoja na zimekuwa zikitolewa mfululizo.
Mkunda amesema wanaoajiriwa katika ajira hizo si wale wataalamu na mameneja pekee kama walivyotambuliwa na sheria, bali makundi mengine mbalimbali huajiriwa.
“Tumeshuhudia katika taasisi za umma na sekta binafsi zikitoa ajira za mikataba ya miezi mitatu au mwaka mmoja kwa wafanyakazi kwa kipindi kirefu mfululizo kwa mtumishi,” amesema.
Amesema uwepo wa ajira za mikataba hiyo mifupi kwa mtumishi kwa kipindi kifupi unaonyesha upo uhitaji wa ajira za kudumu, au za muda mrefu katika eneo husika.
Mkunda ameeleza uwepo wa malalamiko ya wafanyakazi juu ya kutoshirikishwa katika maboresho ya kitita cha mafao, yaliyofanyika tangu mwaka 2023 na kuanza kutumika mwaka huu.
Amesema utaratibu wa mfuko kusitisha huduma za bima ya afya kwa wachangiaji na wategemezi pale mwajiri anapochelewesha mchango ni makosa.
Makosa yanatokana na kile alichoeleza, mfanyakazi anakuwa ameshakatwa mshahara wake na makato yote ya kisheria, hivyo jukumu la kufikisha michango ni la mwajiri.
Tucta inapendekeza mfanyakazi aendelee kupata huduma na asiathiriwe kwa kosa la mwajiri la kutowasilisha michango.
Amesema kuna haja ya kuboresha sheria na taratibu za kusuluhisha migogoro ya wafanyakazi ili waendelee kuzalisha, badala ya ilivyo sasa muda mwingi hutumika bila matatizo kuisha.
Ametaka kuongezwa kwa bajeti na kuwezeshwa kwa Tume ya Usuluhishi na Uamuzi (CMA), ili iwe na uwezo wa kutatua migogoro hiyo haraka.
Mkunda amemuomba Dk Mpango kuongeza miezi mitatu ili iwe sita kwa ajili ya likizo ya uzazi kwa wanawake wanapoenda kujifungua.
Amesema kufanya hivyo kutajenga afya ya akili ya mfanyakazi na malezi bora ya mtoto, tofauti na sasa ambapo mwanamke akienda likizo ya uzazi anakuwa na hofu ya kibarua chake.