Dar es Salaam. Jeshi la Polisi nchini Tanzania limepiga marufuku maandamano yaliyopangwa kufanyika Septemba 23, 2024 jijini Dar es Salaam ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).
Hata hivyo, Chama hicho kimejibu kikisema ni haki yao kuandamana kwa mujibu wa Sheria ya Vyama vya Siasa.
Chadema imepanga kufanya maandamano hayo kuishinikiza Serikali ya Tanzania kueleza hatua iliyofikia juu ya matukio ya watu kutekwa, kupotea na kuuawa kwa wananchi na makada wake.
Leo Ijumaa, Septemba 13, 2024, Msemaji wa Jeshi la Polisi Tanzania, David Misime amewaeleza waandishi wa habari, akiwa Moshi mkoani Kilimanjaro kuwa maandamano hayo hayatafanyika.
Misime ametoa onyo kwa viongozi wa Chadema kuacha kuhamasisha uvunjifu wa amani na kuwa atakayekaidi hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yake.
Misime amesema tayari Rais Samia Suluhu Hassan amekwishaagiza vyombo vya dola kufanya uchunguzi wa matukio mbalimbali na taarifa kukabidhiwa kwake, hivyo Chadema wanapaswa kutulia ili wasiharibu uchunguzi huo.
Hata hivyo, katika mkutano huo na waandishi, Misime hakuruhusu kuulizwa maswali na waandishi.
Alipoulizwa kuhusu kauli hiyo, Makamu Mwenyekiti wa Chadema, Tundu Lissu amesema kwa mujibu wa Sheria ya Vyama vya Siasa, Chadema ina haki ya kufanya mikutano ya hadhara na maandamano.
“Sheria hiyo inalitaka Jeshi la Polisi kutoa ulinzi na msaada kwa vyama vya siasa wakati wa mikutano na maandamano iwe ya amani na tulivu.
“Jeshi la Polisi linatakiwa kuheshimu sheria hiyo na kuheshimu haki za Chadema kufanya mikutano na maandamano kwa mujibu wa sheria,” amesema Lissu.