Sakata la Kakolanya lachukua sura mpya Singida Fountain Gate

SAKATA la kipa namba moja wa Singida Fountain Gate, Beno Kakolanya limechukua sura mpya ikiwa ni siku chache tangu nyota huyo wa zamani wa Tanzania Prisons, Yanga na Simba kufichua kuwa baada ya kuijibu barua ya kutokwenda katika Kamati ya Nidhamu, Ijumaa iliyopita, akaondolewa kwenye ‘group’ la WhatsApp wachezaji, huku nyumba yake akipewa mchezaji mwingine.

Kakolanya amesema hayo baada ya kuulizwa hatma yake ni ipi, kutokana na mgogoro uliopo baina yake na timu na kujibu kwa kifupi;

“Sijapewa barua yoyote hadi sasa ya kuonyesha kusimamishwa ama kufukuzwa, maana nilitegemea baada ya barua yangu, wangenijibu.”

Kisha kaongeza kwa kusema; “Wangenijibu barua yangu, ningeelewa nini napaswa kukifanya, hivyo ukiniuliza hatma yangu ni ipi, viongozi ndio wanajua hatima yangu ni nini.”

Hata hivyo, Ofisa Habari wa Singida FG, Hussein Massanza alitoa sababu ya Kakolanya kutolewa kwenye group la WhatsApp, akisema inatokana na mchezaji huyo kuwa nje ya kazi, ila atakaporejea atarudishwa.

“Anatakiwa arudi kazini, bado ana mkataba na timu, akirejea ataungwa kwenye group, nyumba yake na vitu vyake vipo salama, ama kama anataka kuondoka afuate taratibu zinazotakiwa.”

Massanza amesema bado wanamheshimu Kakolanya kama mchezaji wao, hivyo wanamtarajia arejee ili akendeleze majukumu yake.
“Bado tunahitaji aendelee na majukumu yake, hatuwezi kusema kila kitu kwenye vyombo vya habari.”

Mgogoro wa Kakolanya na timu hiyo ulianza muda mchache kabla ya mechi yao dhidi ya Yanga ambapo aliondoka kambini, jambo lililolalamikiwa na uongozi kuwa ni utoro, lakini mchezaji huyo akaja akajibu baadaye kwamba alimuaga meneja, hivyo alishangazwa kuhukumiwa bila kuulizwa.

Katika mechi hiyo iliyopigwa kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, jijini Mwanza, Yanga ilishinda mabao 3-0, mawili yakifungwa na Joseph Guede, huku jingine likitiwa kambani na kinara wa mabao wa Ligi Kuu, Stephane Aziz KI kwa shuti la mbali akimalizia asisti ya Clement Mzize.

Related Posts