Mdamu afanyiwa upasuaji | Mwanaspoti

HATIMAYE aliyekuwa mshambuliaji wa Polisi Tanzania, Gerald Mathias Mdamu, amefanyiwa upasuaji wa mguu wa kulia ambao ulikumbwa na changamoto ya jipu la kwenye mfupa.

Mdamu alipata ajali ya kuvunjika miguu Julai 9, mwaka 2021, akiwa na wenzake katika basi la timu ya Polisi Tanzania likitokea mazoezini katika Uwanja wa TPC wakienda kambini, ambapo alifanyiwa upasuaji katika Hospitali ya Taifa Muhimbili.

Hivi karibuni, Mwanaspoti liliibua hali yake kuwa mbaya na alipofanyiwa vipimo vya X-ray katika hospitali hiyo aligundulika kuwa na jipu katika mfupa.

Kwa mujibu wa mkewe, Juliana, mumewe amefanyiwa upasuaji leo Ijumaa, hivyo ataendelea na matibabu mengine chini ya madaktari wa hospitali hiyo.

“Namshukuru Mungu aliyewapa moyo Watanzania wote waliojiotolea kuhakikisha Mdamu anatibiwa, madaktari hasa nakumbuka jinsi Dk Kennedy Nchimbi alivyompokea kwa mara ya pili, alivyomjenga kiakili kuchukulia ni hali ya kawaida na inatibika, TFF chini ya Rais Karia, makamu wa Rais wa Yanga, Arafat Haji, Bakari Mwamnyeto na Zawadi Mauya,” amesema mke wa mchezaji huyo.

“Shukrani za kipekee, nalishukuru gazeti la Mwanaspoti kwa kuibua hali yake maana ndiyo sababu ya Mdamu kupata msaada wa kuchangiwa matibabu yake. Familia yangu kwa sasa itakuwa na amani maana akipona atakuwa anafanya shughuli zake mwenyewe.”

Juliana amesema kwamba kabla ya kupata msaada wa kuchangiwa pesa za matibabu walikuwa wamekata tamaa, lakini kwa sasa anafurahia kuona wataendelea na mapambano ya maisha.

Related Posts