Bao la mshambuliaji Crispin Ngushi, limetosha kuipa ushindi wa pili Mashujaa, ikiendeleza makali yake kwenye Ligi Kuu Bara ikiwalaza Coastal Union ya Tanga.
Ngushi amefunga bao hilo pekee dakika ya 14 akipokea pasi ya beki Abderhman Mussa, kisha mfungaji kuwatoka kiakili mabeki na kipa bora wa Ligi Kuu msimu uliopita, Ley Matampi wa Coastal Union.
Ushindi huo unaifanya Mashujaa kupaa hadi nafasi ya pili kwenye msimamo wa ligi ikifikisha pointisaba kwa kushinda mechi mbili na sare moja.
Kipigo hicho cha Coastal Union kinaifanya timu hiyo kufikisha mechi mbili bila ushindi ikibaki nafasi ya 13 na pointi moja iliyotokana na sare ya bao 1-1 iliyoipata dhidi ya KMC.
Kwenye mchezo huo uliopigwa Uwanja wa KMC Complex jijini Dar es Salaam Coastal ikiwa mwenyeji  imeonyesha kiwango cha kawaida ikikosa makali kwenye safu ya ushambuliaji.
Ngushi ambaye ametua Mashujaa akitokea Coastal Union, ameendelea kuwa usajili  mzuri kwa Wanajeshi hao akifunga bao la pili msimu huu ambapo kwenye mechi mbili alizofunga timu yake umeibuka na alama tatu.
Licha ya Coastal Union kimrejesha uwanjani beki wake, Lameck Lawi kwenye mechi ya leo, bado ukuta umendelea kuruhusu mabao kwenye mechi ya pili msimu huu.