Alikiba azindua rasmi Crown TV, chaneli ya wasanii wote

Na Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital

Msanii maarufu wa Bongo Fleva, Ali Kiba, amezindua rasmi kituo chake cha televisheni, Crown TV, ambacho kitakuwa kinapatikana kupitia Azam TV chaneli namba 415.

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo leo, jijini Dar es Salaam, Ali Kiba alibainisha kuwa Crown TV ni jukwaa mahsusi kwa wasanii wa aina zote za sanaa, na kwamba kituo hicho kitakuwa nyumbani kwa wasanii waliowahi kukabiliwa na changamoto za kutangaza kazi zao.

“Wasanii wote wanaobanwa sehemu mbalimbali, mfamle anawaambia hapa ndio kwenu. Karibuni kufanya kazi zenu na kutangaza,” alisema Ali Kiba kwa kujiamini, akisisitiza kuwa lengo la Crown TV ni kuwa jukwaa huru kwa kila msanii.

Ali Kiba, ambaye pia anajulikana kama Mfalme wa Bongo Fleva, anamiliki vyombo vingine vya habari ikiwa ni pamoja na Crown FM 92.1 na Crown Digital, huku akilenga kuleta mapinduzi katika tasnia ya sanaa nchini Tanzania.

“Hii ni fursa kwa wasanii wote nchini na nje ya nchi kutumia Crown TV kama jukwaa lao la kuonyesha vipaji na kazi zao kwa hadhira kubwa kupitia Azam TV,” aliongeza.

Related Posts