SMZ yatenga Sh34 bilioni posho ya nauli kwa wafanyakazi

Unguja. Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Zanzibar (Zatuc), limewasilisha changamoto nane mbele ya Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi likiomba kufanyiwa kazi ili kuongeza ufanisi kwa wafanyakazi.

Wakati Zatuc ikiwasilisha changamoto hizo, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) imetenga Sh34 bilioni kwa ajili ya posho ya nauli kwa wafanyakazi, kila mtumishi atapewa Sh50,000.

Akisoma risala leo Mei Mosi, 2024 katika Uwanja wa Gombani Mkoa wa Kusini Pemba zilikofanyika sherehe za Siku ya Wafanyakazi ‘Mei Mosi’ kitaifa, Katibu Mkuu wa shirikisho hilo, Khamis Mwinyi Mohammed amezitaja baadhi ya changamoto kuwa ni kucheleweshwa utekelezaji wa hoja ya kiwango kikubwa cha makato ya mishahara yao.

Pia, ametaja matatizo ya mikataba ya wafanyakazi katika mabaraza ya manispaa ambayo huwa ya muda mfupi na isiyokidhi mahitaji yao.

Bila kutaja, Katibu huyo amemuomba Dk Mwinyi kuwapa pole wafanyakazi, kwani kuongezeka kwa kima cha mishahara inadaiwa kuna baadhi ya mambo yameondoshwa jambo ambalo si sahihi.

“Tunaomba unapoongeza hii mishahara utoe ufafanuzi kwa utumishi kwani tukienda kuomba baadhi ya vitu tunaambiwa tumeongezewa mishahara, hivyo baadhi ya mambo yameondoshwa. Tunanyanyaswa hatuna raha hata ya kuomba kitu chochote,” amesema Khamis.

Ametaja changamoto nyingine ni wafanyakazi wanaostaafu kabla ya miaka 10 hawapati pensheni kama inavyotakiwa.

Ameomba kurekebishwa pensheni za wastaafu kwani wanazipokea na kiinua mgongo cha kima cha chini ambacho hakiendani na hadhi zao kulingana na walivyotumikia Taifa.

“Baadhi ya viongozi wakiwemo wakurugenzi, makatibu na ofisa mdhamini wanatumia lugha zisizo nzuri na wanaturudisha nyuma kutokana na kauli zao,” amesema Khamis.

Ametaja changamoto nyingine ni kuchelewa kufanyiwa kazi suala la kikokotoo cha Mfuko wa Hifadhi ya Jamii Zanzibar (ZSSF), akieleza baadhi ya wafanyakazi hawajalipwa fedha zao.

Amesema Mfuko wa Bima ya Afya una changamoto ya mgongano wa masilahi baina ya Wizara ya Afya na mfuko huo, kwani vituo vilivyosajiliwa havikidhi haja na vinawatoza fedha tasilimu wanapohitaji huduma.

Tatizo lingine amesema ni wakati wa utungaji wa sheria na sera Zatuc hawashirikishwi, hivyo kukosekana mawazo ya wafanyakazi.

Wafanyakazi wakiwa kwenye siku ya wafanyakazi duniani (Mei Mosi) ambapo kitaifa Zanzibar zimefanyika katika Uwanja wa Gombani Mkoa wa Kusini Pemba.

“Tunaiomba Serikali zinapokuja hoja kama hizo mtuulize kwani viongozi wanachenga mambo mengi,” amesema Khamis.

Akijibu hoja hizo, Rais Dk Mwinyi amesema changamoto zilizowasilishwa ni nyingi na hawezi kuzitolea ufafanuzi kulingana na muda lakini atazifanyia kazi.

Dk Mwinyi ameagiza Wizara ya Nchi Ofisi ya Rais, Kazi, Uchumi na Uwekezaji kukutana na shirikisho hilo mara nne kwa mwaka kusikiliza changamoto zao ili ikifika Mei Mosi, itoe taarifa ya hoja zilizofanyiwa kazi badala ya kusubiri kilele na kutoa changamoto.

Amesema Serikali itaendelea kuwathamini na kuwajali wafanyakazi na itahakikisha inatatua changamoto.

Dk Mwinyi ametoa mfano wa baadhi ya changamoto zilizowasilishwa mwaka jana na zimepatiwa ufumbuzi kuwa ni kupandisha pensheni kwa wastaafu kutoka Sh90,000 hadi Sh180,000.

“Kwa madhumuni ya kuimarisha hifadhi ya jamii wakiwamo wafanyakazi, Serikali imefanya uamuzi wa kutoa mafao manane kati ya tisa yanayotambulika na Shirika la Kazi Duniani (ILO) ili kuhakikisha wananchi wanapata haki zao pindi wanapopatwa na maafa, maradhi au kukosa ajira,” amesema Dk Mwinyi na kuongeza:

“Napenda niwahakikishie kuwa, Serikali ina dhamira ya dhati ya kuendelea kuimarisha mazingira ya kazi na utoaji wa masilahi bora kwa wafanyakazi.”

Katika utekelezaji wa dhamira hiyo, Dk Mwinyi amesema Serikali itachukua hatua za kuanza kutoa posho ya nauli za kwenda kazini na kurudi nyumbani ya Sh50,000 kwa watumishi wote wanaostahiki kulipwa posho.

Amesema Sh34 bilioni zimetengwa na Serikali kwa ajili ya posho ya usafiri.

Pia amesema Serikali imedhamiria kuhakikisha inaongeza fedha kwa ajili ya posho ya likizo, zikiwa zimetengwa Sh2.5 bilioni katika bajeti mpya ya mwaka 2024/25.

Kwa madhumuni ya kuimarisha hifadhi ya jamii wakiwemo wafanyakazi, Serikali imefanya uamuzi wa kutoa mafao manane kati ya tisa yanayotambulika na ILO ili kuhakikisha wananchi wanapata haki zao pindi wanapopatwa na maafa, maradhi au kukosa ajira.

Mafao hayo ni kukosa ajira, uzeeni, ajali kazini, mafao ya uzazi, mafao ya ulemavu na mafao ya urithi.

Amesema Serikali imeanza mchakato wa kuanzisha kituo maalumu cha utoaji wa huduma za afya kwa wafanyakazi nchini.

Amesema kupitia mfumo wa Sema na Rais (SNR) jumla ya malalamiko 1,903 ya wafanyakazi yamepatiwa ufumbuzi sawa na asilimia 97 ya malalamiko yaliyowasilishwa yakihusisha madai ya posho, marekebisho ya mishahara na mafao ya kiinua mgongo.

Amesema malalamiko 224 yamewasilishwa na wafanyakazi wa sekta binafsi ambayo asilimia 88 kati ya hayo yamepatiwa ufumbuzi.

Malalamiko hayo yalihusisha madai ya mishahara, fedha za ZSSF, fidia, wafanyakazi kutokupatiwa mikataba na kutokufuatwa sheria, kanuni na miongozo ya ajira.

Amesema Sh3.9 bilioni zilitumika kulipa stahiki zao.

Kwa mujibu wa Dk Mwinyi, Serikali inaendelea na hatua za kuangalia uwezekano wa kuridhia na kusaini mikataba sita mipya ya kazi ikiwamo ya kulinda haki za wafanyakazi wa majumbani, na wa hifadhi ya jamii.

Mingine ni mkataba wa Sera ya Ajira, miwili inayohusu usalama na afya kazini, na wa kinga kwa wanaopata majanga ya ajali, maradhi na vifo katika kazi.

Kusainiwa kwa mikataba hiyo amesema kutaweka mazingira mazuri zaidi ya kazi na masilahi bora kwa wafanyakazi.

Katika kipindi cha miaka mitano Serikali imepanga kutengeneza ajira 300,000 kwa wananchi, lakini ndani ya kipindi cha miaka mitatu, Dk Mwinyi amesema tayari Serikali kupitia shughuli mbalimbali za utekelezaji wa miradi ya maendeleo, imefanikisha upatikanaji wa ajira 180,000.

Amesema Serikali imeimarisha upatikanaji wa ajira nje ya nchi, akisema Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imesaini mkataba wa ushirikiano na nchi za Qatar, Saudia na ipo katika hatua za mwisho za kusaini mkataba na Oman.

Amesema upatikanaji wa ajira za nje umeongezeka kwa asilimia 35 kutoka ajira 1,080 kwa mwaka 2022/23 hadi ajira 3,078 kwa mwaka 2023/24.

Kwa ajira za ndani, amesema zimeongezeka kwa asilimia 65.9 kupitia mikataba iliyothibitishwa kutoka ajira 6,348 mwaka 2022/23 hadi 9,630 kwa mwaka 2023/24.

Kwa upande wa Serikali Kuu amesema jumla ya ajira 6,735 zimetolewa kwa ajili ya watumishi wapya wa umma katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita.

Mwakilishi wa Jumuiya ya Waajiri Zanzibar (Zanema), Ali Msalaha amesema wanaamini mazungumzo baina ya wafanyakazi na waajiri ndiyo njia pekee ya kupata suluhu ya changamoto zao.

Related Posts